• HABARI MPYA

    Sunday, May 17, 2020

    RAIS MAGUFULI ASEMA ATARUHUSU MICHEZO IENDELEE WIKI IJAYO MAAMBUKIZI YA CORONA YAKIENDELEA KUPUNGUA

    Na Mwandishi Wetu, Chato
    RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Joseph Magufuli amesema kwamba maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID19 yamepungua nchini na ikiendelea hivyo wiki ijayo ataruhusu michezo iendelee.
    Mheshimiwa Rais Dk Magufuli ameyasema hayo leo wakati akishiriki Ibada ya Jumapili katika Kanisa la KKKT Usharika wa Chato Mkoani Geita ambayo ilirushwa na Redio, Televisheni.
    “Kama wiki hii tunayoianza kesho (hali) itaendelea hivi, nimepanga kufungua vyuo ili wanafunzi wetu waendelee kusoma na pili nimepanga pia sisi kama taifa kuruhusu michezo iendelee kwa sababu michezo ni sehemu moja ya burudani kwa Watanzania,”.
    Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli leo amesema kwamba maambukizi ya virusi vya corona yamepungua nchini na hali ikiendelea hivyo wiki ijayo ataruhusu michezo iendelee 

    Kauli hiyo inafuatia Mei 3, mwaka huu Rais huyo kipenzi cha Watanzania kusema kwamba anafikiria kuruhusu Ligi Kuu ya Tanzania Bara iendelee kwa sababu hajasikia mwanamichezo hata mmoja kuathiriwa na virusi vya corona.
    Rais Magufuli alisema hayo alipokuwa akihutuba wananchi kupitia Televisheni huko huko Chato siku hiyo na kwamba anafikiria hivyo kwa sababu wanamichezo hawajaathiriwa na corona kuwazuia ni kutaka waugue.
    Mei 3, Rais Magufuli wakati anamuapisha Mbunge wa Iramba Magharibi Mheshimiwa Dk Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria akichukua nafasi ya Dk. Augustine Philip Mahiga aliyefariki duna Mei 1, mwaka huu alisema; 
    “Siku zinazokuja mbeleni ninafikiria hata kuruhusu ligi iendelee, ili watu wawe wanacheza angalau wanaangalia kwenye TV na kadhalika, tuweke utaratibu mzuri, kwa sababu ninaelewa hata walioathirika na corona sijaona mwanamichezo mmoja yeyote ambaye amedhurika sana kwenye hili,”. 
    “Na hii inadhihiridha wazi kwamba kwa wale wanaofanya mazoezi corona inawakwepa sasa kama tunawazuia hata kucheza mpira maana yake tunawaambia waugue corona,”.
    “Najaribu kusubiri wataalamu wangu wanishauri vizuri, kwamba hata ligi tuendelee kuchezwa, inawezekana tunaweza tukaishi na huu ugonjwa kama wanavyoishi watu wenye ukimwi, wenye suruwa, wenye TB na maisha yakaendelea,”.
    Ikumbukwe Machi 17, mwaka huu TFF ilisimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
    Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
    Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAIS MAGUFULI ASEMA ATARUHUSU MICHEZO IENDELEE WIKI IJAYO MAAMBUKIZI YA CORONA YAKIENDELEA KUPUNGUA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top