• HABARI MPYA

  Thursday, July 04, 2019

  KMC YAMSAJILI BEKI WA ZAMANI WA SIMBA SC, MAZEMBE NA ESPERANCE, JANVIER BOKUNGU

  Na mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya KMC ya Kinondoni imemsajili beki wa zamani wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Janvier Besala Bokungu.
  KMC itakayoshiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza Jumamosi mjini Kigali, Rwanda imemtambulisha rasmi leo mchezaji huyo ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja.
  Taarifa ya KMC leo imesema kwamba, Bokungu anayeweza kucheza beki wa kati, pembeni kulia na kiungo wa ulinzi, anajiunga na timu hiyo akitokea Groupe Bazano ya Ligi Kuu ya kwao, DRC na amesafiri na timu kwenda Kigali.

  Beki Mkongo, Janvier Besala Bokungu amejiunga na KMC kutoka Groupe Bazano ya DRC

  Bokungu mwenye umri wa miaka 30 sasa, aliibukia klabu ya DC Virunga mwaka 2004 kabla ya kuhamia TP Mazembe mwaka 2005 ambako alidumu hadi 2008 alipohamia Esperance ya Tunisia.
  Mwaka 2011 alirejea Mazembe, lakini bila kufuata taratibu za kuvunja mkataba na Esperance – jambo ambalo liliiponza klabu ya DRC kuadhibiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
  TP Mazembe iliitoa Simba SC ya hapa katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 6-3, ikishinda 3-1 Lubumbashi na 3-2 Dar es Salaam, lakini kwa kumtumia Bokungu akiwa bado anatambulika kama mchezaji wa Esperance ikaondoshwa mashindanoni. 
  Simba ilirudishwa mashindanoni baada ya kushinda rufaa waliyomkatia Bokungu, aliyevunja mkataba kinyume cha taratibu na klabu ya Esperance ya Tunisia na ikacheza mechi ya mkondo mmoja na Wydad Casablanca ya Morocco mjini Cairo, Misri na kufungwa 3-0, hivyo kuangukia kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako ilitolewa na DC Motema Pembe ya DRC kwa mabao 2-1. 
  Mwaka 2016 Bokungu alijiunga na Simba SC baada ya kuachewa na Mazembe na akacheza kwa msimu mmoja timu ya Dar es Salaam kabla ya kutupiwa virago akarejea kwao na sasa anaibukia KMC chini ya kocha Mganda, Jackson Mayanja. 
  Pamoja na Bokungu, KMC imemsajili kiungo wa ulinzi, Melly Sivirwa raia wa DRC pia kutoka Vital'O ya Burundi.
  Awali ya hao, KMC ilitangaza kuwasajili Kenny Ally Mwambungu kutoka Singida United, viungo washambuliaji Mohamed Samatta kutoka Mbeya City, mabeki Amos Charles kutoka Mbao FC, Abdallah Mfuko, washambuliaji Vitalis Mayanga wote kutoka Ndanda FC, Ramadhan Kapela kutoka Kagera Sugar na Salim Aiyee kutoka Mwadui FC.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KMC YAMSAJILI BEKI WA ZAMANI WA SIMBA SC, MAZEMBE NA ESPERANCE, JANVIER BOKUNGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top