• HABARI MPYA

    Thursday, July 11, 2019

    MECHI YA TAIFA STARS NA HARAMBEE YASOGEZA MBELE ‘SIKU YA MWANANCHI’ YANGA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KILELE cha Siku ya Mwananchi, tamasha maalum la kutambulisha kikosi kipya cha Yanga SC lililopangwa kufanyika Julai 27, limesogezwa mbele.
    Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga SC, Dismass Ten katika mkutano wake na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani mjini Dar es Salaam.
    Ten amesema kwamba sababu za kusogezwa mbele kwa Siku ya Mwananchi ni kupisha mchezo wa kufuzu Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) mwaka 2020 Cameroon kati ya Tanzania na Kenya.
    Taifa Stars watakuwa wenyeji wa Harambee Stars Julai 27 katika mchezo wa kwanza Raundi ya kwanza ya mchujo wa kuwania fainali za CHAN 2020, michuano inayoshusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee kabla ya timu hizo kurudiana Agosti 2 mjini Nairobi.
    Na kwa sababu hiyo, tarehe mpya ya kilele cha Siku ya Mwananchi itatangazwa upya, lakini tayari kikosi cha Yanga SC kipo kambini mjini Morogoro chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Msambia Noel Mwandila kikijiandaa na msimu mpya. 

    Kipa Ramadhani Kabwili (kulia) akiwa na mchezaji mpya, Patrick Sibomana kambini Morogoro

    Tayari Yanga SC imeimarisha kikosi chake kwa kusajili wachezaji wapya 14 ambao ni kipa Metacha Boniphace Mnata kutoka Mbao FC ya Mwanza alipokuwa anacheza kwa mkopo kutoka Azam FC, mabeki Muharami Salum Issa ‘Marcelo’ kutoka Malindi ya kwao, Zanzibar, Ally Mtoni 'Sonso' kutoka Lipuli FC ya Iringa, Ally Ally kutoka KMC ya Kinondoni, viungo wa ulinzi, Abdulaziz Makame kutoka Mafunzo ya Zanzibar na Mapinduzi Balama kutoka Alliance FC ya Mwanza, 
    Wengine saba wote wa kigeni ambao ni kipa Farouk Shikalo kutoka Bandari ya kwao, Kenya, Sadney Urikhob kutoka Namibia, Lamine Moro kutoka Ghana, Juma Balinya kutoka Uganda, Issa Bigirimana, Patrick Sibomana wote wa Rwanda, Mustapha Seleman kutoka Burundi na Maybin Kalengo kutoka Zambia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MECHI YA TAIFA STARS NA HARAMBEE YASOGEZA MBELE ‘SIKU YA MWANANCHI’ YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top