• HABARI MPYA

    Wednesday, July 24, 2019

    SIMBA SC YAENDELEZA UMWAMBA ‘SAUZI’, YAIPIGA PLATINUMS STARS FC 4-1 RUSTERNBURG

    Na Mwandishi Wetu, RUSTERNBURG
    TIMU ya Simba SC imeendeleza ubabe katika mechi zake za kujiandaa na msimu mpya baada ya leo kuwachapa wenyeji, Platinums Stars FC 4-1 mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
    Mzambia, Clatous Chama leo amefunga mabao mawili dakika za 11 na 58, wakati mabao mengine yamefungwa na viungo wenzake, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman kwa penalti dakika ya 13 na Muzamil Yassin dakika ya 87, wakati la Platinums Stars FC limefungwa na Ruele Modise dakika ya 75 kwa penalti pia.
    Huo ni mchezo wa pili mfululizo katika kambi yake ya Rusternburg kujiandaa na msimu mpya baada ya jana kuichapa 4-0 timu ya Chuo Kikuu cha Orbit Tvet, mabao ya Nahodha na mshambuliaji tegemeo, John Raphael Bocco dakika ya tisa na 28, kiungo Hassan Dilunga dakika ya 23 na mshambuliaji mpya, Wilker Henrique da Silva kutoka Bragantino ya Daraja la Nne kwao, Brazil dakika ya 30.
    Baada ya mchezo wa leo, Simba itateremka tena uwanjani Jumamosi kumenyana na Township Rollers ya Botswana kabla ya kukamilisha ziara yake kwa kucheza na Orlando Pirates ya Johannesburg Julai 30, mechi zote zikipigwa Rusternburg.
    Ikumbukwe mabingwa hao  wa Tanzania Bara, Simba SC watamenyana na Power Dynamos ya Zambia Agosti 6 Uwanja mjini Dar es Salaam katika mchezo wa kirafiki kwenye tamasha la Simba Day.
    Simba SC imelazimika kurudisha nyuma kwa siku mbili tamasha hilo ambalo kila mwaka hufanyika Agosti 8 baada ya ratiba ya Ligi Mabingwa Afrika kutoka ikionyesha mechi za kwanza za raundi ya Kwanza zitachezwa kati ya Agosti 9 na 11. 
    Simba SC wataanzia ugenini dhidi ya UD do Songo ya Msumbiji kati ya Agosti 9 na 11 kabla ya kurejea nyumbani kwa mchezo wa marudiano kati ya Agosti 23 na 25.
    Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza, Simba itakutana na mshindi kati ya FC Platinum ya Zimbabwe na Nyasa Bullets ya Malawi na ikifuzu mtihani huo pia itaingia tena hatua ya makundi.
    Wakati Simba ni mabingwa wa Bara, Power Dynamos walimaliza nafasi ya sita kwenye Kundi B Ligi Kuu ya Zambia msimu uliopita, ambalo Green Eagles iliongoza na kuingia fainali na kufungwa kwa penalti 3-1 na ZESCO United walioibuka mabingwa wa Zambia baada ya sare ya 0-0.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAENDELEZA UMWAMBA ‘SAUZI’, YAIPIGA PLATINUMS STARS FC 4-1 RUSTERNBURG Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top