• HABARI MPYA

    Tuesday, July 30, 2019

    AJIBU AUMIA GOTI, HATARINI KUKOSEKANA MECHI YA MARUDIANO TAIFA STARS NA HARAMBEE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIUNGO mshambuliaji wa Tanzania, Ibrahim Ajibu Migomba yuko hatarini kuukosa mchezo wa marudiano dhidi ya Kenya Jumapili mjini Nairobi kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) baada ya kuumia kwenye mechi ya kwanza.
    Ajibu aliyerejea klabu yake, Simba SC baada ya misimu miwili ya kucheza Yanga, Jumapili aliingia akitokea benchi dakika ya 54 kwenda kuchukua nafasi ya Ayoub Lyanga wa Coastal Union Taifa Stars ikilazimishwa sare ya 0-0 na Harambee Stars.
    Lakini mchezaji huyo kipenzi cha mashabiki alimaliza mechi hiyo ya kwanza ya kuwania tiketi ya CHAN ya 2020 akiwa anachechemea baada ya kuumia, kabla ya jana kupelekwa hospitali kwa matibabu.

    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam, Meneja wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema kwamba Ajibu yuko shakani kushiriki mchezo wa marudiano kutokana na maumivu ya goti.
    “Tunaendelea vizuri na mazoezi, lakini bahati mbaya Ajibu naye ameingia kwenye orodha ya majeruhi, ameumia goti, hivyo hatuna uhakika wa kuwa naye kwenye mchezo wa marudiano,”alisema Cannavaro.   
    Ajibu anafanya idadi ya wachezaji majeruhi Taifa Stars kufika wanne, baada ya kipa Aishi Manula wa Simba SC, beki David Mwantika na kiungo Mudathir Yahya wote wa Azam FC ambao wote walikosa mechi ya kwanza. 
    Taifa Stars italazimika kushinda ugenini baada ya sare hiyo ya nyumbani ili iweze kusonga mbele katika mbio za kuwania nafasi ya kucheza fainali za CHAN.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AJIBU AUMIA GOTI, HATARINI KUKOSEKANA MECHI YA MARUDIANO TAIFA STARS NA HARAMBEE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top