• HABARI MPYA

    Tuesday, July 23, 2019

    SIMBA DAY SASA NI AGOSTI 6 TAIFA, WATACHEZA NA POWER DYNAMOS YA ZAMBIA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba SC watamenyana na Power Dynamos ya Zambia Agosti 6 Uwanja mjini Dar es Salaam katika mchezo wa kirafiki kwenye tamasha la Simba Day.
    Simba SC imelazimika kurudisha nyuma kwa siku mbili tamasha hilo ambalo kila mwaka hufanyika Agosti 8 baada ya ratiba ya Ligi Mabingwa Afrika kutoka ikionyesha mechi za kwanza za raundi ya Kwanza zitachezwa kati ya Agosti 9 na 11. 
    Simba SC wataanzia ugenini dhidi ya UD do Songo ya Msumbiji kati ya Agosti 9 na 11 kabla ya kurejea nyumbani kwa mchezo wa marudiano kati ya Agosti 23 na 25.
    Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza, Simba itakutana na mshindi kati ya FC Platinum ya Zimbabwe na Nyasa Bullets ya Malawi na ikifuzu mtihani huo pia itaingia tena hatua ya makundi.

    Kwa sasa kikosi cha Simba SC kipo mjini Rusternburg nchini Afrika Kusini ambako kimeweka kambi kujiandaa na msimu mpya na leo kimecheza mechi yake ya kwanza ya kujipima nguvu na kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya timu ya Chuo Kikuu cha Orbit Tvet.
    Mabao ya Simba SC yamefungwa na Nahodha na mshambuliaji tegemeo, John Raphael Bocco dakika ya tisa na 28, kiungo Hassan Dilunga dakika ya 23 na mshambuliaji mpya, Wilker Henrique da Silva kutoka Bragantino ya Daraja la Nne kwao, Brazil dakika ya 30.
    Baada ya mchezo wa leo, Simba itateremka tena uwanjani kesho kumenyana na Platinums Stars ya Rusternburg, Township Rollers ya Botswana Jumamosi na Orlando Pirates ya Johannesburg Julai 30.
    Wakati Simba ni mabingwa wa Bara, Power Dynamos walimaliza nafasi ya sita kwenye Kundi B Ligi Kuu ya Zambia msimu uliopita, ambalo Green Eagles iliongoza na kuingia fainali na kufungwa kwa penalti 3-1 na ZESCO United walioibuka mabingwa wa Zambia baada ya sare ya 0-0.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA DAY SASA NI AGOSTI 6 TAIFA, WATACHEZA NA POWER DYNAMOS YA ZAMBIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top