• HABARI MPYA

    Tuesday, October 02, 2018

    WALIOWAPINGA TULLY, SURU NA KAJUNA KUGOMBEA SIMBA WAUMBULIWA…WAAMBIWA WAKAJARIBU NA TFF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya uchaguzi ya klabu ya Simba imetupilia mbali mapingamizi yaliyowekwa na Jackson John Sagonge na Said Mohamed Bedui dhidi ya wagombea wa nafasi za Ujumbe wa Bodi, Mwina Mohamed Kaduguda, Iddy Noor Kajuna, Said Tully, Ally Suru na Jasmine Badar.
    Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi Simba SC, Boniface Lihamwike amesema katika taarifa yake leo kwa vyombo vya Habari kwamba, mapingamizi hayo yametupwa kwa sababu hayana mashiko.
    Katika mapingamizi yao waliyoyawasilisha Septemba 22 na 23, Sagonge na Bedui waliwatuhumu Kaduguda, Kajuna, Tully, Suru na Jasmine kushindwa kuwasilisha hesabu zilizokaguliwa mbele ya mkutano mkuu wa wanachama katika kipindi chao cha uongozi.

    Pingamizi dhidi ya Said Tully (kulia) limetupiliwa mbali na Kamati ya Uchaguzi ya klabu

    “Mnamo tarehe 27/09/2018 na 28/09/2018 kamati ilisikiliza mapingamizi yote, na baada ya kusikiliza pande zote na kufanya uchunguzi wa kina kamati ilibaini mapingamizi yote hayana mashiko na manamo tarehe 29/09/2018 kamati ilitoa maamuzi na kuyatupilia mbali mapingamizi yote,”.
    Aidha, Lihamwike amewaambia wote walioweka na kuwekewa pingamizi haki ya rufaa iko wazi na asiyeridhika ana haki ya kukata rufaa mbele ya kamati ya Rufaa ya TFF ndani ya siku tatu tangu maamuzi kutolewa.
    Amesema Kamati pia inawaarifu Wajumbe wote kuwa nakala za uamuzi za mapingamizi husika zinapatikana makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi mjini Dar es Salaam.
    Uchaguzi wa Simb SC unatarajiwa kufanyika Novemba 3, mwaka huu mjini Dar es Salaam na mbali ya Kaduguda, Kajuna, Tully, Suru na Jasmine wagombea wengine wa nafasi za Ujumbe ni Hussein Kitta Mlinga, Mohamed Wandi, Suleiman Haruob Said, Abdallah Rashid Mgomba, Christopher Kabalika Mwansasu, Alfred Martin Elia, Juma Abbas Pinto, Hamisi Ramadhani Mkoma, Abubakari Zebo, Patrick Paul Rweyemamu, Zawadi Ally Kadunda na Asha Ramadhani Baraka.
    Waliopitishwa kuwania nafasi ya Uenyekiti wa Bodi ni Swedy Nkwabi aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji enzi za Rais Alhaj Ismail Aden Rage na mchezaji wa Simba SC miaka ya 1980, Mtemi Ramadhani.
    Uchaguzi wa Simba SC unakuja baada ya uongozi uliopita ulioingia madarakani juni 30, mwaka 2014 chini ya Rais, Evans Elieza Aveva, Makamu wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Wajumbe Iddi Kajuna, Said Tully, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmine Badour kumaliza muda wao.
    Lakini Aveva na Kaburu hawakufanikiwa kumalizia muda wao madarakani, kufuatia kuwekwa rumande katika gereza la Keko tangu Juni 29, mwaka jana kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kesi ambayo bado inaendelea katika Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam.
    Na Julai 1, mwaka jana, Kamati ya Utendaji iliwateua Salum Abdallah ‘Try Again’ na Iddi Kajuna kukaimu nafasi za Aveva na Kaburu na hao ndiyo waliosimamia mchakato mzima wa mabadiliko ya klabu kuelekea uchaguzi Mkuu ujao.
    Katiba mpya ya Simba SC inaelekea Rais wa klabu awe na elimu ya kiwango cha Shahada ambaye ataongoza Bodi ya Wakurugenzi itakayokuwa na Wajumbe wanane chini yake.
    Na Mwenyekiti huyo atakuwa na mamlaka ya kuteua Wajumbe wengine wanne, kati yao mmoja lazima awe mwanamke ili kukamilisha Bodi ya Ukurugenzi ya watu wanane.
    Hiyo ni baada ya mfanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini, kukubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye awali katika mkutano Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
    Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WALIOWAPINGA TULLY, SURU NA KAJUNA KUGOMBEA SIMBA WAUMBULIWA…WAAMBIWA WAKAJARIBU NA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top