• HABARI MPYA

  Monday, October 01, 2018

  MAMBO YALIVYOKUWA KATIKA MECHI YA SIMBA NA YANGA JANA TAIFA

  Na Lulu Ringo, DAR ES SALAAM
  ULE msemo wa “Sisi Na Wao Lini”  umetimia jana baada ya miamba miwili ya Jiji la Dar es Salaam, Simba na Yanga kushuka kwenye Uwanja wa Taifa na kutunishiana misuli ndani ya dakika 90, kila mmoja akimuonyesha mwenzake nani zaidi.
  Watani hao wa Dar es Salaam waliona isiwe kesi, wakaamua kumaliza mchezo kama walivyoanza kwa kutoka suluhu.
  Mchezo wa Simba na Yanga maarufu kama Watani wa Jadi wa Dar es Salaam, ama Kariakoo Derby (Makao Makuu wa Simba yapo Kariakoo na Yanga ilianzishwa Kariakoo kabla ya kuhamia Jangwani) kwa kawaida tumezoea kukutana na vituko na mambo mengi ya kushangaza katika mchezo huu, hii ni kutokana na uhasimu mkubwa ulio katika klabu hizi.
  Ukitaka kufurahia mchezo huu, wahi kufika uwanjani usisubiri wakati wa mtanange kuanza, mimi nilijitahidi kuwahi mapema kabla ya mchezo nikawa Uwanja wa Taifa kushuhudia mambo ya nje ya uwanja kabla ya mchezo wenyewe uwanjani.
  Mshambuliaji wa Simba SC, Meddie Kagere akimpita beki wa Yanga, Abdallah Shaibu 'Ninja' katika mchezo wa jana

  Katika pitapita zangu nikamuona bwana mmoja anayefahamika kwa jina la Frank Yanga ameshika mdoli wenye muonekano wa mnyama Simba kwa kutumia kinywa chake, nikatabasamu kabla sijaondoa macho yangu katika kinywa cha kijana yule aliyekua amejitanda kitambaa kikubwa chenye rangi ya njano na kijani ghafla nikaona kipara kilichoandikwa kwa rangi ya
  kijani 2-0.
  Nikaona hapana jambo hili haliwezi nipita bure nikamfuata kijana yule, nikamuuliza haya yote maana yake nini? Akanijibu hapa mnyama (Simba) keshakufa ndiyo maana nimemning’iniza mdomoni.
  Akaniambia Ibrahim Ajib na Amissi Tambwe ndiyo watakaofanya hayo mauaji, basi mimi nikajua tafsiri ya ule mchoro wa kichwani na mdoli uliokua unaning’inia mdomoni.
  Basi nikaendelea na pepesa pepesa zangu nikapishana na mtu aliepigilia mavazi mekundu mithili ya mtu alijeruhiwa na chui. Sasa ikabidi niwe makini katika kumpekua japo kwa kutumia macho yangu naweza kugundua ni vitu vingapi alivyovaa venye rangi ile.
  Nikaanzia miguuni alikuwa kavaa viatu vyekundu, soksi ndefu hadi magotini nyekundu, suruali nyekundu iliyochomekewa ndani ya zile soksi, fulana kuuuubwa nyekundu iliyochomekewa ndani ya suruali na kofia nyekundu na nyeupe iliyofanana na kawa ya kufunikia chakula ikiwa imefunika kichwa kidogo mithili ya tunda la ubuyu, bwana yule kaona kama haitoshi kaamua kujifunika na shuka kama bendera. 
  Nikasema
  Mungu msaidie kijana wako apate ushindi asije kurudi kwake akiwa mtupu. Zikiwa zimesalia dakika chache sana mtanange kuanza kama ilivyo desturi wageni waalikwa walisogea katika uwanja kusalimia na kutambulishwa kikosi cha Simba na Yanga kilichokuwa kimesimama
  kusubiri filimbi ya Muamuzi.
  Viongozi wote waliosalimia akiwemo Mgeni Rasmi ambaye ni Spika wa Bunge la Jmahuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.
  Vituko ni sehemu ya maisha, basi mwamuzi Jonesia Rukyaa akapuliza kipyenga kuashiria mtanange kuanza. Ibrahim Ajib yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kupiga mpira huo ambapo alipiga pasi ndefu kuelekea upande wa Simba mpira uliotoka nje moja kwa moja bila kuguswa na mchezaji
  yeyote.
  Mpira ukawa wa kurusha kuelekezwa upande wa Yanga na aliyerusha mpira ule alikuwa Shomari Kapombe, ndani ya dakika saba uwanja ukainamia upande wa Yanga kana kwamba mkandarasi wa uwanja angeweza kutafutwa aulizwe hilo bonde hakuliona wakati wa ujenzi wa uwanja au alifanya
  kusudi?
  Dakika ya 11 Mganda Emmanuel Okwi alifanya shambulizi hatari sana lakini ashukuriwe mlinda mlango wa Yanga, Beno Kakolanya aliyesimama imara, Okwi akaona haitoshi dakika ya 18 akafanya shambulizi jingine Beno akaokoa.
  Simba walionekana kusaka alama tatu, dakika ya 26 walishapata kona tatu huku Yanga ikiwa haina ilichopata, nakumbuka shuti moja alilopiga Ajib dakika ya 22 akiwa umbali wa mita 25 kuelekea golini mwa Simba lakini mpira ukapita juu ya lango la Simba.
  Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilikamilika milango yote ikiwa imenuna, zikaanza tena dakika 45 za kipindi cha pili mambo yakawa kama yale ya dakika za kwanza kilichobadilika ni wachezaji na upande wa timu kufungia kubadilika.
  Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera dakika ya 55 alimtoa Ibrahim Ajib akamuingiza Matheo Anthony,  Mbelgiji wa Simba Kocha Patrick Aussems akamjibu Zahera dakika ya 62 akamuingiza Mohamed Ibrahim akamtoa Shiza Kichuya lakini bado mambo yakawa yaleyale.
  Dakika ya 78 Yanga ikamtoka Deus Kaseke akaingia Mrisho Ngassa, Simba wakajibu tena shambulizi hili dakika ya 81 akatoka Clatous Chama akaingia Said Ndemla, Simba wanazidi kukazia dakika ya 89 akatoka Emmanuel Okwi akaingia Adam Salamba, hadi dakika 90 zinakamilika ubao
  wa matokeo ukasoma 0-0.
  Haikuwa rahisi kuelewa Simba wamemalizaje mchezo ule bila kupata bao na Yanga wamemalizaje mchezo ule bila kufungwa, Simba walionyesha soka safi sana yawezekana hawakuwahi kucheza soka kama lile tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara na Yanga walicheza mchezo wa ajabu sana
  yawezekana hakuwahi kucheza mchezo ule tangu kuanza kwa ligi.
  Ngoja nikwambie mwanzo mwisho mpira umechezwa na Simba kama ningekuwa kipimo cha umiliki wa mipira ningetoa asilimia 90 kwa Simba na 10 kwa Yanga, kibarua nilichokuwa nimebakiwa nacho ni kuwatafuta makocha wa timu hizi mbili.
  Safari yangu ilianzia kwa Kocha wa Simba aliyekuwa na maneno machache tuu ya kujieleza japo alionekana kushangazwa na matokeo waliyoyapata licha ya kutengeneza nafasi nyingi
  “Kiukweli sielewi kwa nini hatujashinda tumetengeneza nafasi nyingi sana tumemiliki mpira ndani ya dakika 90 kikubwa tunahitaji kuwa makini ukizingatia wiki mbili zilizopita hatujawa na matokeo mazuri,” anasema Aussems.
  Mambo yakawa tofauti kwa Kocha wa Yanga, Zahera aliyekuwa na mengi sana ya kuzungumza tena alizungumza kiufundi.
   “Wanasema kama huwezi kushinda mechi basi usipigwe hicho ndicho kilichonifurahisha tatizo limekuja wachezaji wengi walipotea sababu nilibadilisha mfumo tuliozoea kucheza katika mechi nne tulizocheza awali.
  “Tuliangalia video ya Simba mara nne vile tulivyoona ndivyo walivyocheza leo (jana) tuliamua kuwaachia wacheze mpira maana wao wana presha tofauti na sisi, tumeshinda michezo minne tofauti na Simba hivyo tukasema tutawaachia watengeneze nafasi nyingi.
  “Wametengeneza nafasi nyingi za kupata magoli kwa sababu sisi dhamira yetu ni kuwaachia wacheze mpira mtu akipoteza mpira unapaswa utoke spidi, ukiangalia Kaseke na Ajib wanalala hilo lilikua tatizo letu ila sare matokeo haya mimi nayafurahia tu,” anasema Zahera.
  Yanga walionekana wakicheza mchezo wa kuzuia zaidi tofauti na Simba waliokua wakitafuta mabao, Simba iliimarika kuanzia safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji ndiyo sababu ya wao kutengeneza mashambulizi mengi zaidi kuliko Yanga.
  Mchezo wa jana umenishangaza sana kama kuna  mchezaji aliyestarehe ndani ya uwanja ni kipa wa Simba, Aishi Manula alistarehe sana alichokifanya ni kukamilisha idadi ya wachezaji 11 kwa kikosi kwani alitulia bila kupata kashikashi nyingi kama kipa wa Yanga.
  Kipa wa Yanga, Beno Kakolanya huyu ndiye mchezaji ambaye hakupata hata muda wa kukumbuka anaitwa nani, muda wote alikuwa akipambana na wachezaji wa Simba waliokuwa wakiagiza mafataki langoni mwake.
  Simba imecheza michezo sita ikishinda mara tatu, ikatoka sare mara mbili na kupoteza mara moja na sasa ina pointi 11, Yanga imecheza mechi tano, imeshinda mara nne na kutoka sare moja hivyo sasa ina pointi 13.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAMBO YALIVYOKUWA KATIKA MECHI YA SIMBA NA YANGA JANA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top