• HABARI MPYA

  Monday, October 01, 2018

  RUVU SHOOTING YAIPAPASA MBAO FC MABATINI, YAIPIGA 1-0 NA KUIONDOA KILELENI LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, MLANDIZI
  TIMU ya Ruvu Shooting imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC ya Mwanza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  Shukrani kwa mfungaji wa bao hilo pekee jioni ya leo, Said Dilunga dakika ya 33 na sasa Ruvu Shooting inafikisha point inane baada ya kucheza mechi saba na kujiinua kidogo hadi nafasi ya 13 kutoka ya 18 kwenye Ligi Kuu nay a timu 20.
  Mbao FC sasa inaondoka kileleni mwa Ligi Kuu baada ya kipigo hicho cha pili katika mechi zake saba jumla hadi sasa, nyingine tano wakishinda nne na sare moja.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Deogratius Anthony dakika ya 36 limewapa ushindi wa 1-0 wenyeji, Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

  Naye Abdulrahman Mussa akaifungia bao pekee JKT Tanzania dakika ya 56 ikiilaza 1-0 African Lyon Uwanja wa Meja Isamuhyo huko Mbweni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
  Nayo Mbeya City ikachomoza na ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji Stand United Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga, mabao ya Eliud Ambokile yote mawili mawili.  
  Mapema katika mchezo uliotangulia mchana wa leo, Mtibwa Sugar ilirejea kileleni baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Biashara United Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
  Mtibwa Sugar inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Zuberi Katwila imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi nane, ikifuatiwa na Mbao FC yenye pointi 14 za mechi saba na Yanga SC pointi 13 za mechi tano.
  Mabao ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa leo yamefungwa na Salum Kihimbwa dakika ya 41 na Haroun Athumani Chanongo dakika ya 82, wakati la Biashara United iliyopanda Ligi Kuu msimu huu limefungwa na Daniel Manyeye dakika ya 29. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RUVU SHOOTING YAIPAPASA MBAO FC MABATINI, YAIPIGA 1-0 NA KUIONDOA KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top