• HABARI MPYA

    Thursday, October 18, 2018

    JKT TANZANIA YAAMUA KUZIPELEKA MKWAKWANI MJINI TANGA MECHI ZAKE DHIDI YA SIMBA NA YANGA LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya JKT Tanzania imehamishia mechi zake mbili za nyumbani za Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya vigogo SImba na Yanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. 
    Uamuzi huo unatokana na Uwanja wake wa nyumbani inaotumia sasa wa Meja Jenerali Isamuhyo ulioko Mbweni Dar es Salaam, kutokuwa na uwezo wa kuhimili wingi wa mashabiki wa timu hizo mbili vigogo nchini Tanzania.
    Na Bodi la Ligi (TPLB) imebariki uamuzi huo JKT Tanzania kutumia Uwanja wa Mkwakwani Jijini kama Uwanja wake wa nyumbani kwa mechi zinazoihusu Simba na Yanga. 
    Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo Boniface Wambura anaeleza sababu za uamuzi huo na kusisitiza kuwa timu zote zimekwishapewa taarifa.


    Baada ya kucheza mechi nane, JKT Tanzania inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 14, sawa na mabingwa watetezi Simba SC waliocheza mechi saba na Mbao FC waliocheza mechi tisa. 
    JKT Tanzania inatarajiwa kuteremka tena dimbani Uwanja wa Mkwakwani kumenyana na wenyeji, Coastal Union katika mfululizo wa Ligi Kuu.
    Kwa ujumla Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho baada ya mapumziko ya wiki mbili kupisha mechi za kimataifa kwa mechi tatu kuchezwa viwanja tofauti.
    Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara Ndanda FC wataikaribisha Mbeya City ya Mbeya, Uwanja wa Mwadui Complex huko Kishapu mkoani Shinyanga, MwaduiFC wataikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani na Azam FC watakuwa wenyeji wa  African Lyon Saa 1:00 usiku Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Jumamosi kadhalika kutakuwa na mechi tatu, Tanzania Prisons wakianza na Singida United ya Singida Saa 8:00 mchana Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Coastal Union na JKT Tanzania ya Dar es Salaam Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga na Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Yanga SC watakuwa wenyeji wa Alliance FC ya Mwanza. 
    Mechi nyingine tatu zitafuatia Jumapili, mabingwa watetezi, Simba SC wakiwakaribisha Stand United Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Lipuli FC wakiwakaribisha Kagera Sugar ya Bukoba Saa 8:00 mchana Uwanja wa Samora mjini Iringa na Mbao FC wakiwa wenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro Saa 10: 00 jioni Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Hadi sasa Azam FC ndiyo inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 18 za mechi nane, ikifuatiwa na Mtibwa Sugar pointi 17 mechi tisa, Yanga SC pointi 16 mechi sita, Singida United pointi 16 pia mechi tisa na mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 14 za mechi saba.
    Hali ni mbaya kwa Mwadui FC ambao baada ya mechi nane, wana pointi tano, nyuma ya Alliance FC pointi sita mechi tisa, sawa na African Lyon na Tanzania Prisons. Biashara United ya Mara, nayo pia ina pointi sita, lakini za mechi nane.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JKT TANZANIA YAAMUA KUZIPELEKA MKWAKWANI MJINI TANGA MECHI ZAKE DHIDI YA SIMBA NA YANGA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top