• HABARI MPYA

  Sunday, October 14, 2018

  BANDA: CAPE VERDE WALIJIPANGA WAKATUPIGA KWAO, NA SISI TUNAJIPANGA TUWAPIGE KWETU JUMANNE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI wa Tanzania, Abdi Hassan Banda amesema kwamba wanajipanga kulipa kisasi kwa Cape Verde baada ya kufungwa mabao 3-0 katika mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Uwanja wa Taifa mjini Praia juzi.
  Taifa Stars watakuwa wenyeji wa Papa wa Bluu Jumanne Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam wakitoka kuchapwa 3-0 kwenye mchezo wa kwanza Ijumaa.
  Na akizungumza kwenye mahojiano maalum na Azam TV, wakati anarejea nchini akiwa kwenye ndege, Banda alisema kwamba walichokosea ni kutowaheshimu wenyeji wao, ambao hata kwenye orodha ya viwango vya soka ya FIFA wapo nafasi ya 67, wakati Tanzania ni ya 140.

  Abdi Banda amesema kwamba wanajipanga kulipa kisasi kwa Cape Verde Jumanne

  “Lakini sisi ni kama tulikwenda na matokeo yetu kutokana na mechi ya Uganda, lakini na kingine ambacho tulikosea ni kutokuheshimu zile mbinu zetu za uchezaji, kitu ambacho kimetugharimu. Lakini nahisi ni mchezo, kwa sababu wao wamejipanga nyumbani na sisi tunarudi zetu nyumbani tunakuja kujipanga trena nyumbani,”alisema Banda. 
  Katika mchezo wa juzi, huo uliochezeshwa na marefa wa Mali, Boubou Traore, Drissa Kamory Niare na Baba Yomboliba, mabao ya Cape Verde yalifungwa na mshambuliaji wa klabu ya Partizan ya Ligi Kuu ya Serbia, Ricardo Jorge Pires Gomes na beki wa MOL Vidi FC ya Hungary Ianique dos Santos Tavares maarufu kama Stopira.
  Huo unakuwa mchezo wa tatu wa Taifa Stars katika kundi bila ushindi, baada ya awali kutoa sare za 1-1 na Lesotho Dar es Salaam na 0-0 na Uganda mjini Kampala na wa pili tu kwa kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike tangu aanze kazi Agosti.

  Abdi Banda (kulia) katika mchezo na Cape Verde mjini Praia Ijumaa Taifa Stars wakifungwa 3-0 

  Mchezo mwingine wa kundi hilo jana, Uganda, The Cranes ilijiimarisha kileleni baada ya ushindi wa 3-0, mabao ya Emmanuel Okwi  anayechezea klabu ya Simba ya Tanzania aliyefunga mawili dakika za  11 na 63 na Faruku Miya wa Farouk Miya wa HNK Gorica ya Croatia kwa penalti dakika ya 36.
  Uganda sasa ina pointi saba baada ya kucheza mechi tatu, ikishinda mbili na kutoa sare, sasa ikifuatiwa na Cape Verde pointi nne za mechi tatu pia, wakati Tanzania na Lesotho zina pointi mbili kila moja.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BANDA: CAPE VERDE WALIJIPANGA WAKATUPIGA KWAO, NA SISI TUNAJIPANGA TUWAPIGE KWETU JUMANNE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top