• HABARI MPYA

  Sunday, January 01, 2017

  SIMBA YAMALIZANA VIZURI NA ANGBAN, NDUSHA WAREJEA KWAO LEO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIPA Muivory Coast wa Simba SC, Vincent Paul Angban  anatarajiwa kuondoka nchini leo kurejea kwao, baada ya kumalizana na klabu ya Simba.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online jana, Angban alisema kwamba baada ya kumalizana na Simba SC ataondoka Jumapili kurejea kwao.
  “Natarajia kuondoka Jumapili baada ya kukutana na uongozi wa Simba na kukamilishiana malipo. Nawashukuru wapenzi wote wa Simba kwa sapoti yao kwangu kipindi chote, maisha yanaendelea,”alisema.
  Vincent Angban  anatarajiwa kuondoka nchini leo kurejea kwao, baada ya kumalizana na klabu ya Simba

  Simba ilimuacha Angban na kiungo Mussa Ndusha kutoka Jamhuriya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika dirisha dogo Desemba ili kupata nafasi ya kusajili Wathana, Kipa Daniel Agyei na kiungo James Kotei. 
  Lakini haikuweza kuwapatia haki zao wachezaji hao mapema hadi ilipofanya hivyo juzi – na sasa wote wanaondoka kurejea kwao kuendelea na maisha mengine.
  Kipa huyo aliibukia katika klabu ya vijana ya Rio Sport d'Anyama kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza mwaka 2005, ambako hata hivyo miaka miwili baadaye aliondoka na kwenda kujiunga na Sawe Sports msimu wa 2006/2007.
  Mwaka 2007, Angban akajiunga na ASEC Mimosas ambako alikuwa kipa wa kwanza hadi mwanzoni mwa msimu wa 2009 alipoumia na nafasi yake kuchukuliwa na Daniel Yeboah. 
  Yeboah akawavutia zaidi makocha wa timu hiyo kwa ubora wake wa kuokoa michomo na akaendelea kudaka hata Angban alipopona.
  Baada ya kumaliza Mkataba wake ASEC, Angban akarejea Jeunesse na baadaye akaenda London kudakia U21 ya Chelsea.
  Amewahi kudakia timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Ivory Coast katika michuano ya Afrika nchini Benin mwaka 2005 na aliiwakilisha pia nchi yake katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2008.
  Amedakia pia timu ya taifa ya wakubwa ya Ivory Coast ‘Tembo’ katika michuano ya CHAN ikiwemo ile ya mwaka 2009 na ndiye aliyesimama langoni katika mechi na Tanzania, Taifa Stars ikishinda 1-0 bao pekee la Mrisho Ngassa.   
  Na anaondoka Simba SC baada ya kuidakia jumla ya mechi 56 na kufungwa mabao 25 huku mechi 34 akisimama langoni bila kuruhusu nyavu zake kuguswa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YAMALIZANA VIZURI NA ANGBAN, NDUSHA WAREJEA KWAO LEO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top