• HABARI MPYA

    Wednesday, November 16, 2016

    KAMA TATIZO NI WACHEZAJI, KWA NINI TUHANGAIKE NA MAKOCHA KILA SIKU?

    TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars Jumapili ilifungwa mabao 3-0 na Zimbabwe katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Uwanja wa Taifa, Harare, Zimbabwe.
    Kwa ujumla Taifa Stars, inayofundishwa na Nahodha wake wa zamani, Charles Boniface Mkwasa ilicheza ovyo siku hiyo na ilistahili kipigo hicho.
    Mshambuliaji wa K.V. Oostende ya Ubelgiji, Knowledge Musona aliifungia Zimbabwe bao la kwanza dakika ya tisa, kabla ya mshambuliaji wa Helsingborgs IF ya Sweden, Matthew Rusike kufunga bao la pili dakika ya 53 na mshambuliaji wa Dalian Yifang ya China, Nyasha Mushekwi kufunga la tatu dakika ya 56.
    Nahodha wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji alidhibitiwa vikali sawa na mchezanji mwenzake wa zamani wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu. 
    Baada ya matokeo hayo, nyumbani Tanzania wenye nchi yao wamecharuka wengi wao wanalia na kocha na wana msemo wao maarufu siku hizi wa kushinikiza kocha aondoke; “Uwezo wake umefika mwisho”.
    Wanasema Mkwasa uwezo wake umefika mwisho aondoke na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litafute mwalimu mwingine.
    Jumapili Mkwasa aliiongoza Taifa Stars katika mechi ya 13 tangu achukue nafasi ya Mholanzi, Mart Nooij Julai mwaka jana, kati ya hizo akiwa ameshinda mechi mbili, kufungwa sita na sare tano.
    Nooij aliondoka baada ya Taifa Stars kufungwa mechi tano mfululizo, kufuatia kurithi mikoba ya Mdenmark Kim Poulsen Aprili mwaka 2014.
    Kwa ujumla, Nooij ameiongoza Stars katka mechi 18 tangu arithi mikoba ya Poulsen, kati ya hizo akishinda tatu tu, sare sita na kufungwa tisa- akifunga mabao 17 na kufungwa 28.
    Nooij aliaga katika mkutano na Waandishi wa Habari Juni 23, mwaka jana hoteli ya Tansoma eneo la Gerezani, Dar es Salaam, akisema anawashukuru Watanzania wote, Serikali, wadau wa mpira wa miguu nchini na TFF kwa sapoti waliyompatia wakati akiwa kazini.
    Alisema alifurahia maisha yake akiwa Tanzania kwa kipindi chote alichokua akifundisha timu ya Taifa, lakini kwa sababu imefikia mwisho wa ajira yake hana jinsi anaondoka, lakini ataendelea kuikumbuka Tanzania na watanzania wote kila siku kwa ukarimu wao.
    Na TFF iliamua kumtoa Nooij baada ya Taifa Stars kufungwa 3-0 na Uganda Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika mchezo wa kuwania tiketi ya CHAN. 
    Ilibidi siku hiyo Nooij atolewe nje kwa msaada wa Polisi Uwanja wa Amaan, Zanzibar baada ya mashabiki kutaka kumpiga. Na ndiyo maana hakuwa na sababu zaidi ya kuaga.
    Mapema wakati Nooij anaaga, Rais wa  TFF, Jamal Malinzi alisema wameamua kuagana nae mbele ya vyombo ya habari kama iliyofanyika pia wakati wa utambulisho wake wakati wa kuanza kazi.
    “Mpira wa miguu unachangamoto nyingi, Watanzania tuna safari ndefu kufika katika mafanikio ndio maana TFF imeanza kuwekeza katika soka la vijana, sababu ndio msingi wa kuwa na timu bora ya Taifa,” alisema Malinzi.
    “Duniani kote chimbuko la timu bora ni soka la vijana na watoto, tukiwa na vijana wengi walioanza kucheza mpira katika umri mdogo wanapofikia umri wa kuchezea timu ya Taifa tutakua na kikosi bora,”.
    “Nchi za wenzetu inapofikia kocha kuita wachezaji wa timu ya Taifa anakuwa na wigo mpana, kwetu sisi wachezaji wanocheza soka nje ya nchi wanahesabika, hivyo ni lazima tuanze kuwekeza kwenye soka la vijana,”alisema Malinzi.
    Nami pia, wakati Watanzania wengi wanamkandia Mkwasa naitazama Taifa Stars yetu nikiilinganisha na Zimbabwe – nagundua ni vitu viwili tofauti.
    Sisi tulikuwa na Nahodha wetu tu Samatta aliye katika mwaka wake wa kwanza katika soka la kulipwa Ulaya – lakini kikosi cha Zimbabwe kilisheheni wachezaji wanaocheza nje watupu ukiondoa Bruce Kangwa wa Azam FC ya nyumbani Tanzania.
    Ni kweli timu yetu ilicheza chini ya kiwango na hiyo ilitokana na kukosekana kwa baadhi ya wachezaji katika safu ya ulinzi kama Kevin Yondan, ambaye yeye siku hizi hataki tu kuchezea timu ya taifa.
    Lakini bado tatizo la msingi la ujumla ni kutokuwa na wachezaji wa kiwango cha kuunda Taifa Stars ya ushindani. Hata aletwe kocha gani hapa Tanzania, naye atazungumziwa kufukuzwa tu baada ya mwaka mmoja.
    Najua Mkwasa mwenyewe ataondoka kwa sababu amekwishakubaliana na Yanga anarejea huko – lakini kwa kocha ajaye, tujitajidi kuweka subira na uvumilivu.
    Wakati umefika sasa tujifunze kukumbuka sababu za makocha waliotangulia kuondoka na ili tuweze kuwapa muda zaidi makocha waliopo kazini.
    Kwani tatizo la msingi la soka ya Tanzania si walimu, bali ni wachezaji. Na kama tatizo ni wachezaji hatuwezi kuanzia kujadili makocha. Jumapili nitazungumzia njia za kufanya kujaribu kukuza uwezo wa wachezaji wetu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMA TATIZO NI WACHEZAJI, KWA NINI TUHANGAIKE NA MAKOCHA KILA SIKU? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top