• HABARI MPYA

    Wednesday, February 03, 2016

    SIKU YANGA SC WATAKAPOGUNDUA MANJI ANAWAPOTEZEA MUDA...

    WAKATI Rais wa Simba SC, Evans Aveva anakata utepe kuashiria kufungua duka la kuuza bidhaa za klabu hiyo juzi eneo la Oysterbay, Dar es Salaam kumbukumbu zilinirudisha miaka mitatu nyuma, wakati Yussuf Manji yupo kwenye kampeni za kuwania Uenyekiti wa Yanga.
    Katika kampeni, moja ya mambo ambayo Manji aliahidi ni kufungua duka kubwa la vifaa vya michezo makao makuu ya klabu, Jangwani ambalo pia lingekuwa linauza na bidhaa za timu yao.
    Manji aliahidi Jangwani kutakuwa na biashara mbalimbali ikiwemo huduma za kibenki na kadhalika- ukiachilia mbali ahadi kuu ya ujenzi ya Uwanja wa Kaunda na kulikarabati jengo liwe la kisasa zaidi.

    Niliikumbuka hadi ramani ya Jangwani City iliyosambazwa kwenye vyombo vya Habari – lakini hilo halikutawala sana kichwa changu zaidi ya kushindwa tu kutekeleza ahadi ya kufungua duka.
    Yanga SC kama klabu hawana fedha, zaidi ya kumtegemea Manji na ufadhili wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL)- ambao wenyewe viongozi wa klabu hiyo wamekwishasema mara kadhaa hautoshelezi bajeti ya klabu hiyo.
    Kwa sababu hiyo unaweza kuona ni kiasi gani Manji ni mtu muhimu sana ndani ya Yanga SC, ambaye hata akosee vipi hakuna anayeweza kupingana naye akaeleweka.
    Ndiyo maana anaamua kufukuza Wajumbe aliochaguliwa nao katika uchaguzi mdogo mwaka 2011 na hata viongozi anaowaajiri atakavyo.
    Dk. Jonas Tiboroha ameingia kwenye orodha ya Makatibu waliofukuzwa Yanga SC chini ya Manji baada ya muda mfupi wa kuajiriwa kwa matumaini, wengine wakiwa ni Lawrence Mwalusako, Benno Njovu na Selestine Mwesigwa.
    Na kwa sababu, wana Yanga walio wengi wanaridhika sana wakiiona timu yao inatamba katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kupamba kurasa za  michezo za magazeti, hawawezi kuona kwa sasa Manji anawakwamisha vipi.
    Sioni cha maana Yanga SC ilichovuna kwa Manji katika kipindi chote cha kuwapo kwake klabuni, zaidi ya kuchangia tu uendeshwaji wa kila siku wa timu.
    Wana Yanga wanaridhika kuona klabu yao haibadiliki ili kuwa yenye hadhi, yenye kujimudu kiuchumi, ikiwa tu Manji anasajili wachezaji hadi wa kigeni na kuhudumia timu, lakini klabu ‘inazidi kuoza’.
    Thamani ya klabu ni rasilimali zake na inavyoweza kuzitumia kujinufaisha kiuchumi- Yanga SC achilia mbali kuwa na mamilioni ya wapenzi na maelfu ya wanachama, ina majengo zaidi ya mawili.
    Wenye kuifahamu historia ya klabu, wanasema Yanga SC mbali na jengo la makao makuu pale Jangwani, wana jengo Mtaa wa Mafia na Tandale. Pia, Yanga SC ina nyumba ya NHC pale eneo la Fire, ambayo wamewahi kuishi kocha Mromania, Victor Stanslescu, marehemu Tambwe Leya na Charles Boniface Mkwasa. 
    Haijulikani nyumba ya NHC kama walipanga au waliuziwa katika maghorofa ya Fire, lakini hadi mwanzoni mwa muongo uliopita ilikuwa bado kwenye himaya ya klabu hiyo.
    Ajabu Yanga SC haipati fedha hata senti moja kutokana na majengo yake yote hayo, angalau jengo la makao makuu wameweka ofisi na wakati mwingine huwa kambi ya wachezaji.
    Kuweza angalau kulitumia jengo la makao makuu kwa ofisi na kambi ni baada ya Manji kulifanyia ukarabati mwaka 2007, lakini kwa zaidi ya miaka 10 kabla ya hapo, lilikuwa halitumiki kwa uchakavu. Lilikuwa kama boma.
    Yanga SC kama klabu, haina uwezo wa kujiendesha bila fedha za Manji kwa sasa na kwa hali halisi huwezi kuona atatokea mfadhili gani mwingine siku za karibuni katika klabu hiyo.
    Na Manji analijua hilo, ndiyo maana hababaishwi na mwana Yanga yeyote, akiamua anatangaza kumfuta uanachama yeyote anayetaka kupingana naye.
    Mikwara ikizidi anatingisha kiberiti hagombei tena, akijua fika wana Yanga wataingiwa na ‘ubaridi’ wakiufikiria mustakabali wa klabu bila yeye.
    Na wana Yanga wanaamua kuwa wapole kwake, kwa sababu wanakumbuka msoto ambao klabu ilipitia tangu kutoweka kwa wimbi la wafadhili wengine wa Kiasia waliomtangulia Manji, akina Abbas Gulamali, Mohammed Viran ‘Babu’ (wote sasa marehemu), Murtaza Dewji na wengineo. 
    Yanga SC ilifikia wakati timu inacheza uwanjani, huku jukwaani watu wanatembeza bakuli kukusanya michango angalau wachezaji wapewe posho, kabla ya Manji kuibuka mwaka 2006 kuokoa jahazi na kubadili taswira nzima ya klabu. 
    Bahati mbaya ambayo Yanga inaipata siku zote, ni kukosa viongozi wabunifu ambao wanaweza kutengeneza mipango ya kuifanya klabu ijitegemee.
    Mara kadhaa tunatoa mifano ya jezi tu za Yanga SC, timu hiyo inapocheza mashabiki hufanana na wachezaji wao uwanjani kwa mavazi, lakini klabu hainufaiki hata kwa senti moja.
    Yanga SC inapoteza si chini ya Sh. Milioni 500 kila mwaka kutokana na mauzo ya jezi pekee- bado ingeweza kupata fedha zaidi kama ingeuza bidhaa nyingine zenye nembo yake kwa mashabiki wake.
    Yanga SC bado ingeweza kuingia ushirika na makampuni kadhaa ya utengenezaji na uuzaji bidhaa kuyaruhusu yatumie nembo ya klabu kwenye bidhaa hizo kwa kulipana.
    Kwa kuwa anasajili, anaongezea fedha za mishahara na makocha kutoka kwenye fungu la TBL, anahudumia timu kwa ujumla ikiwemo suala la kambi hadi Ulaya – hakuna wa kumgusa Manji.
    Kwa tahmini ya juu juu, huwezi kuona ni jinsi gani Manji anawapigisha kwata Yanga SC na hiyo ni kwa sababu wanachama wenyewe wamerdihika na hali hiyo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIKU YANGA SC WATAKAPOGUNDUA MANJI ANAWAPOTEZEA MUDA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top