• HABARI MPYA

  Monday, February 01, 2016

  BONGO FLEVA WAKINUNUA HATA MAHINDI YA KUCHOMA NI HABARI, DANSI JE?

  UPO ukweli mmoja ambao hauna ubishi hata kidogo kuwa baadhi ya mastaa wa filamu na bongo fleva, hupenyeza wenyewe habari zao za udaku kwenye magazeti wakiamini kuwa kuandikwa mara kwa mara kunawaweka ‘hai’ sokoni.
  Na ndio maana kwa sasa wasanii wa bongo fleva na filamu ndiyo wanaoongoza kwa kuandikwa sana magezetini, iwe kwa mema au kwa ubaya.
  Imekwenda hivyo hadi sasa imeanza kuaminika kuwa wasanii hao ndiyo wanaouza zaidi magazeti kuliko wasanii wa muziki wa dansi au hata taarab.
  Hili sio jambo lililokuja kwa bahati mbaya bali ni jambo lililokuja kwa makusudi, wasanii hao wamefanikiwa kujitengenezea himaya kubwa kwenye vyombo vya habari na kuleta athari katika kizazi kijacho ambacho hakitajua sanaa nyingine zaidi ya bongo fleva na filamu.

  Kwa sasa wakati karibu kila nyumba ina mtoto mwenye njozi ya kuwa staa wa bongo fleva, ni rahisi kukuta kitongoji kizima hakina hata mtoto mmoja anayeupenda muziki wa dansi achilia mbali njozi ya kuwa mwanamuziki wa dansi.
  Majuzi niliandika habari moja kwenye mtandao wangu wa Saluti5 iliyomuhusisha mwimbaji wa Mapacha Watatu, Khalid Chokoraa akiendesha boda boda. Mapokeo ya habari ile kwa baadhi ya wadau wa muziki wa dansi yalinishangaza sana.
  Wako walioona kama Chokoraa kadhalilishwa, wako waliona ile haikuwa habari na kustaajabu kuna ajabu gani ya mtu kuendesha boda boda hadi iwe habari.
  Wakati wasanii wa bongo fleva hata wakinunua mahindi ya kuchoma ni habari kubwa, sisi tunashangaa mwanamuziki wa dansi kupigwa picha akiendesha boda boda.
  Hapo ndipo linapokuja somo la KUJIONGEZA kwa wanamuziki wetu wa dansi kuanzia kwenye maisha ya kawaida hadi katika kazi zao.
  Wanamuziki wa dansi wanashindwa kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya kupashana habari - kurasa za mitandao ya kijamii za wasanii wa bongo fleva zimekuwa chanzo muhimu cha habari kwa radio, televisheni na magazeti wakati wanamuziki wengi wa muziki dansi bado wako usingizini juu ya mitandao ya kijamii.
  Sisemi watu watengeneze ‘skendo’ ili waandikwe magazetini, lakini wanamuziki wa dansi wanapaswa kujiongeza sana kwenye kutengeneza habari kuhusu kazi zao na maisha yao ya kila siku. 
  Leo hii msanii wa muziki wa dansi anaweza kuugua na mtu yeyote asijue, msanii wa dansi anaweza kutoa nyimbo mpya hata familia yake isijue achilia mbali mashabiki wake.
  Msanii wa dansi anaingia studio au kwenye show anashindwa kuweka hata picha moja kwenye ukurasa wake wa facebook, lakini usiombe kwa wasanii wa bongo fleva, mbona utakoma kwa promo.
  Wakati Ali Kiba kupanda daladala ilikuwa ni habari iliyotikisa vyombo vya habari, sie tutahamaki tukiona picha ya mwanamuziki wa dansi akila ugali kwa mama ntilie - Tusasema kuna lipi la ajabu, tutasahau kuwa hata Mzee Mamvi alienda kusaka 'promo' kwenye dala dala na kwa mama lishe.
  Chokoraa hakuendesha piki piki ile ya bei poa kwa sababu amefulia, Kiba hakupanda daladala kwa sababu kapigika na wala pengine msanii wa dansi hataenda kula kwa mama ntilie kwa sababu hana pesa ya kwenda hotel ya maana, la hasha! Ni sehemu tu ya kuonyesha mshikamano na jamii iliyomzunguka na sijambo baya jamii hiyo ikijuzwa hilo kwa njia mbali mbali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BONGO FLEVA WAKINUNUA HATA MAHINDI YA KUCHOMA NI HABARI, DANSI JE? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top