• HABARI MPYA

    Wednesday, July 09, 2014

    YANGA SC WAJARIBU KUFANYA KINACHOWEZEKANA, WASILAZIMISHE MAMBO AMBAYO HAYAWEZEKANI

    WAKATI Simba SC wanaendelea taratibu na mradi wa ujenzi wa Uwanja wao eneo la Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, watani wao Yanga SC wanaendelea na jitihada za kuomba kibali kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa kisasa eneo la Jangwani.
    Desemba mwaka 2012, Yanga Ilitangaza mpango wa ujenzi wa Uwanja wa kisasa utakaokuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 40,000, makao makuu ya klabu hiyo makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani mjini Dar es Salaam.
    Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alisema klabu hiyo ina mikakati wa kujenga Uwanja wake wa Kaunda ili uwe wa kisasa na walipanga kuanza ujenzi huo Juni mwaka jana ukiwa na gharama ya dola za Marekani milioni 21 (Sh. bilioni 32).

    Alisema ujenzi huo utafanyika chini ya usimamizi wa Kampumi ya Beijing Constructinon Engineering ya China iliyojenga pia Uwanja wa Taifa na pia kuukarabati Uwanja wa Uhuru jijini hapa.
    “Ramani ya Uwanja ambayo tumepatiwa na Wachina inaingia sehemu ya nje ya Uwanja wetu wa Kaunda ambayo ni eneo la wazi la Serikali. Tangu mwaka jana tumeandika barua kwa Manispaa ya Ilala na wizara yenye dhamana ya ardhi kuomba kibali cha ujenzi na kuongezwa eneo la ziada, lakini bado hatujajibiwa, ndiyo maana tumesimama kusubiri majibu ya Serikali,” alisema Sanga.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Uwanja huo, Francis Kifukwe kwa upande wake alisema uongozi wa klabu hiyo uliandika barua mara mbili zenye kumbukumbu namba YAC/Ardhi/MWA/46/2012 na YAC/Ardhi/MWA/ 47/ 2012 na mpaka sasa anadai hawajajibiwa.
    Awali, Uwanja wa Kaunda pamoja na hosteli ya klabu hiyo vilijengwa mwaka 1973 kwa gharama ya Sh. Milioni 3, sehemu ya fedha hizo zikitoka kwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume (sasa marehemu) na nyingine wanachama wakijichangisha.
    Lakini kwa sasa Uwanja huo umeharibika kwa kutosa matunzo na hali huwa mbaya zaidi wakati wa mvuo zinazosababisha mafuriko ya maji eneo lote la Jangwani.
    Baada ya kupewa kibali cha ujenzi na Serikali, Sanga alisema uongozi wa Yanga unatarajia kusaka benki ambayo itaikopesha klabu hiyo kongwe nchini fedha kwa ajili ya mradi huo. 
    Sanga pia anasema uongozi utawaomba wanachama wao 210,000 kuchangia Sh. 250 kwa wiki ili kwa mwaka zipatikane Sh. bilioni nane kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Uwanja huo.
    Hata hivyo, akizungumza katika mahojiano maalum na BIN ZUBEIRY kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini hapa wiki iliyopita, Ofisa mazingira wa ofisi hiyo alisema Serikali haitakuwa na papara kutoa kibali cha ujenzi wa Uwanja wa Jangwani kwa vile eneo hilo ni njia kuu ya maji.
    Baada ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathmini ya mradi huo, Ofisa huyo anasema Kurugenzi ya Mazingira ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itashauriana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kabla kutoa uamuzi.
    “Eneo la Jangwani ni njia kuu ya maji katika jiji la Dar es Salaam, kumekuwa kukitokea mafuriko kutokana na baadhi ya watu kuvamia eneo hilo na kuendesha shughuli za ujenzi, hivyo kusababisha kuziba kwa njia za maji.”
    Ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji wa kurugenzi hiyo, anasema kuruhusu ujenzi wa Uwanja kwenye eneo hilo kutasababisha maafa zaidi jijini kutokana na mafuriko.
    Wakati Yanga ikiwa imekadiria Sh. Bilioni 32 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja huo, bei ya chini ya kulipa fidia kwa mkazi mmoja mwenye nyumba ya kawaida isiyo ya ghorofa eneo la Jangwani inakadiriwa kuanzia Sh. milioni 700.
    Hata hivyo, inaelezwa kuwa Yanga itahitaji kuhamisha zaidi ya wakazi 30 ambao watalazimika kuwalipa fidia ya Sh. bilioni 21.
    Maofisa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wanasema ni vigumu Yanga kupewa eneo la ziada kwa ajili ya ujenzi huo.
    Wanasema kituo cha mabasi yaendayo kasi, ambacho ni cha kudumu, kitajengwa kwenye eneo hilo. 
    Rehema Isengo, Ofisa habari wa wizara hiyo, anasema eneo la Jangwani liko katika mipango ya maendeleo.
    Eneo hilo licha ya kuwa hatarishi kutokana na kufurika maji kipindi cha mvua, pia ni mkondo wa upumuaji wa bahari na ni bonde ambalo Mto Msimbazi hupita. 
    Mabomba ya Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) pia yanapita kwenye eneo la Jangwani, bomba la majisafi likielekezwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na lile la majitaka likielekezwa baharini.
    Aidha, Aprili 5, 2011 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka alisema maeneo yote yanayopitiwa na Bonde la Msimbazi kuanzia Daraja la Salender, Muhimbili, Jangwani hadi Vingunguti hayapaswi kujengwa mradi wowote huku akiwataka watu wote waliokuwa wamejenga katika maeneo hayo kuondoka.
    Alisema Serikali ina mpango wa kulifanya bonde hilo kuwa eneo la wazi la jiji la Dar es Salaam.
    Ombi la Yanga lilijadiliwa katika vikao vya Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Ilala na viongozi wa Yanga waliotaka kushiriki vikao hivyo walizuiwa kuingia ndani ya chumba cha mikutano cha baraza hilo.
    Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuitaka Yanga kuwasiliana na ofisi Manispaa ya Ilala, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Severin Assenga alisema mwishoni mwa mwaka kuwa klabu hiyo haiwezi kupewa eneo la ziada Jangwani kwa vile eneo wanalolitaka ni la wazi.
    Kwa mujibu wa sheria za ardhi nchini, maeneo ya wazi yanaweza kutumika tu pale panapokuwa na mradi wenye maslahi ya umma na si mtu ama taasisi binafsi. 
    Mkurugenzi wa Utekelezaji na Uzingatiaji wa NEMC, Robert Ntakamulenga aliiambia BIN ZUBEIRY mwishoni mwa wiki kuwa ofisi yake ilipata ombi la Yanga na tayari wameiagiza klabu hiyo kufanya tathmini ya athari za mazingira itakayosababishwa na mradi huo.
    Baada ya kupokea ombi hilo, anasema wataalam wa NEMC walikwenda kwenye makao makuu ya Yanga na kuonyeshwa eneo linaloombewa kibali cha ujenzi huo.
    “Wajumbe wa NEMC) tulikwenda Jangwani tukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Said Meckysadick) na Mkuu wa Wilaya ya Ilala (Raymond Mushi)  kuangalia eneo ambalo Yanga wanaliombea kibali. Tulishauambia uongozi wa klabu hiyo ufanye tathmini ya athari za mazingira zitakazotokana na mradi huo,” alisema Ntakamulenga.
    “Wanatakiwa kufanya tathmini kwa kuwatumia wataalam walioidhinishwa na baraza na sisi (NEMC) tutapitia ripoti na kuangalia kama mradi huo unastahili kupelekwa kwa waziri kwa ajili ya kupatiwa cheti.
    “Tunatambua kwamba eneo la Jangwani ni njia kuu ya maji katika jiji hili lakini ripoti ya tathmini ndiyo itatuongoza katika kutoa maamuzi. Kwa sasa hakuna ripoti yoyote iliyoletwa ofisini kwetu kwa ajili ya mradi huo,” alisema zaidi mkurugenzi huyo. 
    Kifukwe alisema lengo la klabu hiyo ni kujenga Uwanja utakaokuwa na hoteli, kumbi za mikutano, maduka, ofisi, eneo la kuegesha magari na viwanja vingine vidogo kwa ajili ya mazoezi.
    Alisema Yanga ina eneo lenye ukubwa wa hekta 3.59 ambalo inalimiliki kisheria tangu 1972 na inahitaji eneo lenye ukubwa mara tatu zaidi ya lililopo sasa ili kukamilisha ujenzi huo.
    “Kuna watu wamevamia na wanaishi ndani ya eneo letu, baada ya kupatiwa kibali cha ujenzi, itabidi watupishe na tutawaondoa,” anasema Kifukwe na kuongeza:
    “Yanga pia italazimika kuingia mfukoni kuwalipa wanaolizunguka eneo la Uwanja wa Kaunda ambalo Serikali itawaongeza ili kufanikisha ujenzi huo.”
    Kifukwe anasema mradi huo ambao wameupa jina la ‘Jangwani City’, utalifanya eneo hilo kuwa na mandhari nzuri yenye huduma muhimu kwa
    Hapa unaweza kuona ugumu unaoukabili mpango huo wa Yanga SC chini ya Mwenyekiti wake, Yussuf Manji ambaye pamoja na kulitambua hilo, ameendelea kuwatamanisha wana Yanga lisilowezekana.
    Kitu ambacho kitamuingia akilini yeyote kwa sasa ni Yanga kuboresha jengo la makao makuu liwe la kisasa, na kuweza kulitumia hata kibiashara.
    Lakini kwa suala la Uwanja wakati umefika sasa Yanga SC wakaachana na ndoto hizo na kujaribu kufanya kinachowezekana na kitakachokuwa na maslahi na wao kwa sasa.
    Wanunue eneo nje ya mji wafanye mradi wa ujenzi wa Uwanja na hosteli, ambavyo havitawagharimu fedha nyingi na zoezi ambalo halitagubikwa na mizengwe. 
    Yanga SC ni timu kubwa na ina wapenzi wengi kila kona. Kila inapoenda Yanga ndani ya nchi hii, mjini au kijijini basi huko wana Yanga wapo wengi, tena sana.
    Lakini pia wana Yanga wa mjini huifuata timu yao popote inapocheza- huwa tunashuhudia mamia ya wapenzi wa timu hiyo wanasafiri kwenda mikoani kuisapoti timu yao inaopocheza mechi za Ligi.
    Yanga wajenge maskani mpya Mbezi ya barabara ya Morogoro, Bunju, Kongowe, Kisarawe, Mwasonga, Mbutu- popote mashabiki wake wataifuata.
    Yanga SC inapoteza fedha nyingi kwa kutokuwa na Uwanja wake maalum japo wa mazoezi tu. Hivi karibuni, Yanga walipata Uwanja ambao mashabiki walilipa viingilio kwenda kutazama mazoezi, wa Chuo cha Bandari, Tandika na iliripotiwa kwa siku waliingiza hadi Sh. Milioni 2.
    Lakini bahati mbaya ikagundulika ule Uwanja ni mbaya unasababisha wachezaji kuumia na kocha Marcio Maximo akaukataa, hivyo wakarudi Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo ambako pamoja na kulipia, hawaruhusiwi kuingiza mashabiki.
    Dunia ya leo ya sayansi na teknolojia, watu wanatafuta njia rahisi za kupenya- hivyo Yanga SC wanafanane na zama hivi kwa kufanya kile kinachowezekana na si kuendelea kulazimisha kujenga eneo ambalo watalaamu wote wa idara zote wanasema haiwezekani. Ramadhani karim. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAJARIBU KUFANYA KINACHOWEZEKANA, WASILAZIMISHE MAMBO AMBAYO HAYAWEZEKANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top