• HABARI MPYA

    Wednesday, July 09, 2014

    TIKETI ZA ELEKTRONIKI TAYARI KWA MATUMIZI LIGI KUU MSIMU UJAO

    Na Renatus Mahima, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema tiketi za elektroniki zitatumika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaoanza Agosti 24, mwaka huu.
    Ofisa habari na mawasiliano wa shirikisho hilo, Boniface Wambura amesema wameamua kuanza matumizi ya tiketi hizo za kisasa ili kudhibiti hujuma za mapato zinazofanyika viwanjani.
    Amesema mfumo huo utatumika kwenye viwanja vyote vilivyofungwa vifaa vya utambuzi wa tiketi hizo. 
    Viwanja hivyo ni pamoja na Uwanja wa Sokoine (Mbeya), Uwanja wa Mkwakwani (Tanga), Uwanja wa Kaitaba (Kagera), Uwanja wa CCM Kirumba (Mwanza), Uwanja wa Jamhuri (Morogoro), Uwanja wa Sheikh Amri Abeid (Arusha), Ali Hassan Mwinyi (Tabora) na Azam Complex (Dar es Salaam).
    "Noti bandia zilizofikia Sh. 300,000 zilibainika kutumika katika moja ya mechi zilizochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya msimu huu. Matumizi ya tiketi za elektroniki yataondoa hujuma za matumizi ya fedha feki na tiketi feki," amesema Wambura. 

    Tamko la TFF limetolewa ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya Serikali kuiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuliamuru shirikisho hilo kutumia mfumo wa tiketi za elektroniki (ETS) kwenye viwanja mbalimbali vya soka nchini ili kudhibiti uhujumu wa mapato ya milangoni.
    Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara kuhusu utelezaji wa majukumu ya Wizara ya Fedha na Uchumi kwa mwaka wa fedha 2014/15 Bungeni mjini Dodoma mwezi uliopita, mwenyekiti wa kamati hiyo, Luhaga Mpina aliitaka TRA kutoa sharti kwa TFF kutumia mfumo huo ili kuongeza mapato ya nchi.
    "Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati inashauri TRA iweke sharti la lazima la kuitaka TFF kutumia mfumo wa tiketi za elektroniki katika kuuza tiketi zake ikiwa ni jitihada za kuongeza mapato ya serikali," alisema Mpina.
    Mbunge huyo wa Kisesa (CCM), alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa haipati mapato ya kutosha kutoka katika sekta ya michezo hususani mpira wa miguu ulio chini ya TFF kutokana na mfumo dhaifu wa ukusanyaji fedha kipindi cha kuuza tiketi.
    "Serikali haipati mapato ya kutosha kutokana na mpira wa miguu kwa sababu ya tiketi bandia kuendelea kutumika, kukosekana kwa uwazi katika mapato halisi, uwezo mdogo wa kusambaza tiketi nchi nzima na rushwa kwenye mageti ya viwanja," alisema.
    Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu juu ya uhujumu wa mapato unaofanya na baadhi ya watendaji wa TFF kupitia njia mbalimbali ikiwamo ya kutengeneza tiketi bandia wakishirikiana na baadhi ya wadau wa soka nchini.
    Miongoni mwa viwanja vinavyodaiwa kuwa na uhujumu mkubwa wa mapato ni Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya na Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TIKETI ZA ELEKTRONIKI TAYARI KWA MATUMIZI LIGI KUU MSIMU UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top