• HABARI MPYA

    Tuesday, August 13, 2013

    PROFESA KONDIC AFUNGUKA KUHUSU YANGA, ASEMA MANJI...

    Na Mahmoud Zubeiry, Johannesburg, Afrika Kusini
    IMEWEKWA AGOSTI 13, 2013 SAA 3:54 ASUBUHI
    KOCHA wa zamani wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam, Profesa Dusan Savo Kondic amesikitika mno kusikia klabu hiyo hadi sasa haijafanikiwa kuwa na Uwanja wake- lakini pia amempongeza Yussuf Mehboob Manji kuwa Mwenyekiti wa klabu sasa.
    Manji alikuwa mfadhili tu Yanga wakati Kondic ni kocha wa klabu kati ya mwaka 2007 na 2009, chini ya uongozi wa Wakili Imani Omar Madega. 
    Kutoka kulia Profesa Kondic, Bin Zubeiry, Zoran Micovic na Spaso mjini Johannesburg leo

    Akizungumza na BIN ZUBEIRY mjini Johannesburg leo, Profesa Kondic ambaye kwa sasa ameamua kupumzika baada ya mara ya mwisho kufundisha St. George ya Ethiopia, amesema kwamba Yanga wangemsikiliza leo wangekuwa mbali kimafanikio.
    “Nilikuwa nina mipango mizuri, nilimuonyesha Manji, lakini baadaye sijui kikatokea nini wakaanza kunifanyia mambo ya ajabu. Hawataki kufuata programu zangu, wakaninyima hata kambi.
    Profesa Kondic akiwa katika moja ya gari zake




    Nilifanyiwa visa ili niondoke pale, kwa sababu nilikuwa nataka kuisaidia klabu, na hawakutaka hivyo, mimi ndiyo sababu hata lile jengo (Jangwani) lilikarabatiwa,”.
    “Mimi ndiyo sababu timu ilirudi kuweka kambi klabuni na kufanya mazoezi pale. Nimeondoka, timu imerudi kufanya mazoezi viwanja vya kuazima. Niliwafanyia mpango Yanga kupata nyasi bandia kwa bei rahisi sana waweke Kaunda, lakini Manji nadhani hakuwa tayari kwa hilo. Leo unaniambia hawafanyi mazoezi tena Kaunda, inasikitisha,”alisema.
    “Lakini naomba ufikishe pongezi zangu kwa Manji kuwa Mwenyekiti na Hafidh (Saleh) kuwa Meneja, msalimie na Chuji (Athumani Iddi). Siamini kama anamalizia soka yake Tanzania. Yule angecheza popote Ulaya,”aliongeza Kondic.
    Kondic alisema alikuwa ana mipango madhubuti ya kuisaidia Yanga ili siku moja iweze kujitegemea, lakini anasikitika alikwamishwa na watu ambao hawaitakii mema klabu.
    “Nilipokuwa pale kwa kipindi kifupi wachezaji wa Yanga walikwenda kufanya majaribio dunia nzima. George Owino alikwenda Ujerumani, Boniphace Ambani alikwenda China. Said Maulid aliuzwa Angola,”. 
    “Mimi ni kocha mkubwa, kama hadi leo ningekuwa pale, Yanga ingekuwa ina wachezaji wanacheza Ulaya. Ingenufaika sana. Ningeiunganisha Yanga na watu wa kuisaidia kuiinua kiuchumi. Nilikuwa nina mipangpo ya kuifanya klabu ijitegemee, watu hawakutaka. Shauri yao,”alisema.
    Naye aliyekuwa Msaidizi wa Kondic, wakati akiwa Yanga SC, Spaso Sokolovoski ambaye anaishi na bosi wake huyo Rundburg, Johannesburg katika jumba la kifahari lenye bwawa la kuogelea pia ndani, amesema anaamini wangeifikisha Yanga mbali kama wangepewa ushirikiano.
    “Basi tena, shauri yao. Lakini msalimie Kayuni (Sunday) na Mpangala (Emmanuel),”alisema Spaso.     
    Katika miaka miwili na ushei ya kufundisha Yanga, Kondic aliiwezesha kuipa ubingwa wa Bara mara mbili mfululizo, 2007/2008 na 2008/2009 kabla ya kutimuliwa mwanzoni mwa msimu wa 2009/2010 na nafasi yake kupewa Mserbia mwenzake, Kostadin Bozidar Papic.
    Profesa Kondic akiwa na rafiki yake, Mike Milosevic, Meneja wa Monte Casino Afrika Kusini 

    Papic pia kwa sasa yupo Afrika Kusini anafundisha klabu ya Black Leopard ya Daraja la Kwanza. Papic alifukuzwa akaajiriwa Mganda, Sam Timbe na kurejeshwa kabla ya kufukuzwa moja kwa moja.
    Hata kocha aliyemfuatia, Mbelgiji Tom Saintfiet naye alifukuzwa na sasa klabu inafundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: PROFESA KONDIC AFUNGUKA KUHUSU YANGA, ASEMA MANJI... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top