• HABARI MPYA

    Sunday, August 25, 2013

    HIZI NI SALAMU ZANGU KWENU KUTOKA TABORA, RHINO BONGE LA TIMU

    IMEWEKWA AGOSTI 25, 2013 SAA 3:30 ASUBUHI
    MJI wa Tabora jana ulizizima kwa mchezo mkali wa soka wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya wenyeji Rhino Rangers inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Simba SC ya Dar es Salaam, uliomalizika kwa sare ya 2-2.
    Takriban siku tatu kabla ya mchezo huo, gumzo kubwa kwenye vijiwe, ofisi, maskani, sehemu za starehe na maeneo ya kibiashara lilikuwa ni mechi hiyo. Na kweli, umati uliomiminika uwanjani jana ulidhihirisha ni kiasi gani Tabora wanapenda soka.
    Tabora wanapenda mpira na wana hamu nao sana, baada ya miaka zaidi ya 14 ya kuikosa Ligi Kuu tangu  kushuka kwa Milambo ya Tabora, wenyewe wana Tabora walikuwa wanaiita Taifa Teule.

    Kuna baadhi ya vijiwe ilikuwa ukipita hadi raha, namna mabishano yanavyoendelea- inaleta picha ya moja kwa moja ni kiasi gani wana Tabora wamekosa raha kwa muda mrefu.
    Simba na Yanga ni timu za wananchi, popote zina mashabiki na jana wapo wakazi wa Tabora waliondoka majumbani kwao wamevalia nguo nyekundu kwenda kuishangilia Simba SC.
    Ni kama tu enzi zile, mkagua tiketi, maarufu kama TT wa treni ya Reli ya Kati, Mzee Moshi Shaaban alipokuwa anatoka nyumbani kwake kavalia nguo za kijani na njano kwenda kuishangilia Yanga ikicheza na Milambo.
    Basi jana pia ilikuwa raha- wana Simba wa Tabora walitengeneza hadi mabango kuonyesha sapoti kwa timu yao- ingawa walipata upinzani mkali kutoka kwa watu wenye msimamo, mashabiki wa Rhino waliokuwa wakiongezewa nguvu na mashabiki wa Yanga.
    Niliupenda wimbo; “Kama siyo juhudi zako, Rhino, hiyo Simba tungeiona wapii, ooh kama siyoo, kama siyo juhudi zako Rhino, Ligi Kuuj tungeiona wapiii ”- hayo yalikuwa masimango tosha kwa wana Tabora wengine ambao jana walikuwa dhidi ya timu hiyo ya nyumbani kwao.
    Mechi ilikuwa safi ukiondoa dosari za hapa na pale- kama wachezaji wa Rhino kukosa leseni hali iliyosababisha mchezo kuchelewa kuanza. Imezoeleka, unapocheza ugenini, tarajia kuonewa na refa, lakini jana Ally Hassan Mwinyi haikuwa hivyo, ni Simba SC ndiyo walionekana kupendelewa na refa Amon Paul anayetoka mkoa mmoja na Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itang’are ‘Kinesi’, Mara.
    Rhino ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri, wengi wao vijana wadogo na wengi nawafahamu kwa kuwa wameibukia katika mfereji mzuri wa soka- nilikuwa ninakutana nao kwenye mashindano ya Copa Coca Cola Dar es Salaam. Niliwasifu na kuwatabiria kuwa wachezaji wazuri tangu wakati huo na jana waliionyesha kazi Simba SC.
    Kwa wenye kuifahamu historia ya Tabora, ni moja kati ya mikoa iliyokuwa inatoa wachezaji wazuri wa timu ya taifa, tangu enzi za akina Yunge Mwanasali, baadaye akina Said Nassor Mwamba ‘Kizota’, akina Mwinyimkuu, Said John, akina Moshi. 
    Na sababu kubwa ya Tabora kuwa na wachezaji wazuri ni kuwa na shule na vyuo vya elimu ya juu vinavyokusanya vijana kutoka mikoa tofauti, ambao wanapofika hapa pamoja na kusoma wanajiendeleza kimichezo.
    Kwa upande mwingine, Tabora ni kimbilio la watu wa Rukwa na Kigoma hata mikoa mingine jirani kama Singida na Dodoma- kwa hivyo inakuwa rahisi kupatikana vipaji- hapa na wazi kwa miaka 14 ambayo mkoa huu umekosa timu Ligi Kuu, taifa limepoteza sana.
    Vipaji vya mwisho mwisho kutokea Tabora ni akina Wilfred Kidau, Renatus Njohole, Mohamed Banka, Qureish Ufunguo, Haruna Moshi, Aman Mbarouk, Majuto Komu kama wapo na wengine niliowasahau, basi hao ni baadhi.
    Nimeona wachezaji wa timu ya taifa kutoka kikosi cha Rhino- akipatikana mchezaji Tabora ni mchezaji kweli, unasemaje kuhusu Kizota au Boban? Au unamkumbuka yule Said John Msonge aliyetokea Amka ya Nzega kwenda Milambo?
    Vipi kuhusu mabeki kama Jobe Ayoub ‘Kwasa Kwasa’, Ally Manyanya, Mikidadi Jumanne ‘Bubu’ na kipa wao Peter Poka? Au niambie kuhusu mshambuliaji Feruzi Telu ‘Pele’- sasa jiandae kwa majina majina ya mastaa wapya wa soka Tabora kutoka Rhino Rangers.
    Muziki ni huu; Golini, Abdulkarim Mtumwa, kulia Ally Ahmed, kushoto Julius Masunga katikati Laban Kambole na Stanslaus Mwakitosi, dimba la chini Daniel Manyenya, wingi ya kulia Iman Noel, dimba la juu Victor Hangaya, mkongwe Nurdin Bakari anacheza kama mshambuliaji wa pili na Saad Kipanga anakimbiza kushoto, jana Baba Ubaya aliipata habari yake.
    Noel na Kipanga jana walifunga mabao kwa mashuti ya umbali wa zaidi ya mita 20 wakimtungua mmoja wa makipa bora kabisa Afrika Mashariki na Kati, Abbel Dhaira. Wakati ambao tunafurahia kupatikana kwa timu nyingine ya Ligi Kuu mkoani Tabora, tunaweza kujiuliza kiasi gani tunakosa vipaji kutoka mikoa mingine ya kisoka haswa kama Kigoma na Shinyanga? Kwa leo, hizi ndizo salamu zangu kutoka hapa Tabora. Asanteni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HIZI NI SALAMU ZANGU KWENU KUTOKA TABORA, RHINO BONGE LA TIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top