• HABARI MPYA

    Saturday, August 24, 2013

    SIMBA YABANWA NA MAAFANDE WA JESHI TABORA, YATOKA 2-2 NA RHINO

    Na Mahmoud Zubeiry, Tabora IMEWEKWA AGOSTI 24, 2013 SAA 1:00 USIKU
    SIMBA SC imelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo. 
    Mabao yote ya Simba SC yalifungwa na kiungo Jonas Mkude dakika za 10 na 38 kwa penalti, wakati ya Rhino yalifungwa na Iman Noel dakika 36 na Saad Kipanga dakika ya 64.
    Mchezo huo ulichelewa kuanza kwa zaidi ya nusu saa kutokana na wachezaji wa Rhino Rangers kutokuwa na leseni za kuchezea Ligi Kuu na baada ya mabishano marefu, timu hizo zikakubaliana wachezaji wapigwe picha ili kuwepo ushahidi kwamba walioshiriki mchezo huo wana leseni.   
    Wachezaji wa Simba SC wakimpongeza Jonas Mkude baada ya kufunga bao la pili leo

    Mchezo ulianza saa 11 na ushei na iliwachukua Simba SC dakika 10 kupata bao la kuongoza baada ya kiungo Jonas Mkude kuunganisha kwa kichwa kona iliyochongwa na Nassor Masoud ‘Chollo’.    
    Simba SC ilizidisha mashambulizi langoni mwa Rhino baada ya bao hilo, lakini leo mshambuliaji Betram Mombeki alidhibitiwa vikali na mabeki wa Rhino kiasi cha kutaka kugombana.
    Mombeki aliyekuwa kinara wa mabao wa Simba SC wakati wa mechi za kujiandaa na msimu alipewa kadi ya njano kwa kucheza rafu kabla ya kugongwa na kuumia kifundo cha mguu, hivyo kutolewa nje akichechemea dakika ya 35 akimpisha William Lucian ‘Gallas’.
    Dakika ya 36 Rhino wakasawazisha bao kwa shuti la moja kwa moja la umbali wa mita 22 la mpira wa adhabu uliopigwa na Noel na kumuacha kipa wa Simba SC, Abbel Dhaira akilaumiana na mabeki wake. 
    Simba SC walikwenda kuanzisha shambulizi la haraka na kiungo Amri Kiemba aliyechezeshwa kama mshambuliaji leo, akaangushwa kwenye eneo la hatari na refa Amon Paul wa Mara akaamuru penalti, iliyokwenda kukwamishwa nyavuni na Mkude.
    Hadi mapumziko, Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-1 na kipindi cha pili, mchezo uliendelea kuwa wa mashambulizi ya pande zote mbili, Rhino ikiongozwa na mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga, Nurdin Bakari aliyeng’ara leo.  
    Kipa Abbel Dhaira alifungwa bao lingine rahisi kwa shuti la umbali wa mita 20 mpira wa adhabu na Saad Kipanga dakika ya 64 na kuwapatia bao la kusawazisha wenyeji.
    Mchezo ulizidi kuwa mkali baada ya hapo, kila timu ikisaka bao la ushindi na angalau Simba SC walipata nafasi nzuri zaidi dakika ya 89, lakini Sino Augustino alishindwa kufunga akiwa amebaki na kipa baada ya kuwatoka mabeki.  
    Kocha wa Simba SC, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ alisikitishwa na sare hiyo na akasema kipa Mganda Abbel Dhaira amewaangusha leo kwa kufungwa mabao rahisi.
    Lakini pia Kibadeni akasema kukosekana Warundi, beki Kaze Gilbrt na mshambuliaji Tambwe Amisi katika mchezo wa leo kwa sababu ya kutokuwa na Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kulimvurugia mipango yake.
    “Nilitegemea sana kuwatumia wale mabwana leo, lakini kwa bahati mbaya, ITC zao zimechelewa kufika na tumeshindwa kuwatumia, kwa kweli imeniangusha sana,”alisema.
    Kocha wa Rhino, Sebastian Nkoma alisema kwamba mchezo ulikuwa mzuri na timu yake ilicheza vizuri pamoja na ugeni wao katika Ligi Kuu. Alisema matokeo ya sare dhidi ya timu kubwa kama Simba ni mazuri kwake na hilo pia onyo kwa timu nyingine zinazokuja Tabora.   
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Miraj Adam, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Chombo ‘Redondo’/Sino Augustino dk65, Said Ndemla, Amri Kiemba, Betram Mombeki na Haroun Chanongo.  
    Rhino; Abdulkarim Mtumwa, Ally Ahmed, Julius Masunga, Laban Kambole, Stanslaus Mwakitosi, Daniel Manyenya, Iman Noel, Victor Hangaya, Nurdin Bakari, Saad Kipanga.
    Katika mechi nyingine zilizochezwa leo, Mtibwa Sugar imelazimishwa sare ya 1-1 na Azam FC kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
    Mtibwa walitangulia kupata bao kupitia kwa Juma Luizio dakika ya nne kabla ya Aggrey Morris kuisawazishia Azam kwa penalti dakika ya 19. 
    Uwanja wa Mkwakwani, Tanga JKT Mgambo ilifungwa 2-0 na JKT Ruvu- mabao ya Bakari Kondo dakika za 80 na 83, wakati mabao ya Abdi Banda dakika ya 11 na Crispin Odula 37 yaliipa Coastal Union ushindi wa 2-0 ugenini, Arusha dhidi ya wenyeji JKT Oljoro.
    Mbeya City ilianza kwa sare ya bila kufungana nyumbani na Kagera Sugar na Ruvu Shooting iliifumua mabao 3-0 Prisons, ambayo yalitiwa kimiani na Laurian Mpalile aliyejifunga dakika ya 23, Elias Maguri dakika ya 46 na Jerome Lambele dakika ya 60.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA YABANWA NA MAAFANDE WA JESHI TABORA, YATOKA 2-2 NA RHINO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top