• HABARI MPYA

    Monday, August 26, 2013

    KIPRE TCHETCHE HATARINI KUWAKOSA RHINO JUMATANO...STEWART ASEMA HALI NI MBAYA SASA

    Na Mahmoud Zubeiry, Tabora IMEWEKWA AGOSTI 26, 2013 SAA 8:16 MCHANA
    WAKATI John Raphael Bocco ‘Adebayor’ bado majeruhi, safu ya ushambuliaji ya Azam FC inakabiliwa na hatari ya kumkosa kinara wake wa mabao, Kipre Herman Tchetche katika mchezo wake wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara keshokutwa dhidi ya wenyeji Rhino Rangers, Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini hapa ambaye ni mgonjwa.
    Kocha Muingereza, Stewart John Hall ameiambia BIN ZUBEIRY leo mjini hapa kwamba, Tchetche raia wa Ivory Coast ni mgonjwa na hajui kama atakuwa kwenye nafasi ya kucheza Jumatano.
    Gonjwa; Kipre Tchetche anaumwa na anaweza kukosekana Azam ikimenyana na Rhino Jumatano

    “Nipo katika wakati mgumu sana, tayari ninawakosa wachezaji watatu wazuri sana, (Humphrey) Mieno, Brian (Umony) na (John) Bocco. Wakati huo huo, Jabir (Aziz) atakuwa anaendelea kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye mechi ya mwisho msimu uliopita. Na (Samih) Hajji (Nuhu) pia anasumbuliwa na maumivu ya goti,”alisema Stewart.
    Stewart alisema pamoja na kwamba anakabiliwa na matatizo hayo katika timu yake atajipanga kulingana na wachezaji anaobaki nao, kuhakikisha anashinda mchezo wa Jumatano.
    Tegemeo la mabao; Kipre Tchetche ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita

    Kikosi cha Azam FC kiliwasili usiku wa jana mjini Tabora, kikitokea Morogoro tayari kwa mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
    Azam ilifika majira ya saa 4:30 tangu iondoke asubuhi ya jana mjini Morogoro na imefikia katika hoteli ya Mwafrika, jirani kabisa na Uwanja wa Mwinyi. 
    Baada ya mapumziko ya kutwa ya leo, jioni Azam itafanya mazoezi, kujiandaa na mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na wakazi wa mjini hapa.
    Azam ilianza Ligi Kuu kwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar juzi kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
    Mtibwa walitangulia kupata bao kupitia kwa Juma Luizio dakika ya nne kabla ya Aggrey Morris kuisawazishia Azam kwa penalti dakika ya 19. 
    Bado hajawa fiti; John Bocco aliumia kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC

    Baada ya mechi hiyo, Azam ilikwenda kulala mjini Morogoro na asubuhi ikaondoka na basi lake kubwa la kisasa kuja Tabora, walipofika usiku wa jana.
    Rhino, inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) iliyopanda Ligi Kuu msimu huu, nayo ilianza Ligi Kuu kwa sare ya kufungana 2-2 na Simba SC juzi Mwinyi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIPRE TCHETCHE HATARINI KUWAKOSA RHINO JUMATANO...STEWART ASEMA HALI NI MBAYA SASA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top