TIMU ya Pamba Jiji FC imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Fountain Gate FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
Mabao ya Pamba Jiji FC yamefungwa na washambuliaji Mguinea, Abdoulaye Yonta Camara dakika ya 17 na Mganda, John Ben Nakibinge dakika ya 45’+2, wakati la Fountain Gate limefungwa na mshambuliaji Mnigeria, Mnigeria Chukwunonye Obasi dakika ya 34.
Kwa ushindi huo, Pamba Jiji FC inafikisha pointi 29 katika mchezo wa 20 na kurejea nafasi ya tano, ikiizidi tu wastani wa mabao Singida Black Stars ambayo pia ina mechi moja mkononi.
Kwa upande wao Fountain Gate hali inazidi kuwa mbaya baada ya kupoteza mchezo huo, ikibaki na pointi zake 19 za mechi 20 nafasi ya 13 kwenye Ligi Kuu inayoshirikisha timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja na mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment