MWANARIADHA nyota wa Kimataifa wa Tanzania Sajini Alphonce Felix Simbu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) anatarajiwa kushiriki mbio za Boston Marathon nchini Marekani Aprili 20 2026.
Katika mahojiano aliyoyafanya na chombo kimoja cha habari Nchini Marekani, Simbu amesema amejipanga kufanya vyema kwenye shindano hilo na kuendelea kuiletea sifa nchi yake, Tanzania na Jeshi kwa ujumla.
Ikumbukwe mwaka jana, Simbu alishinda Medali ya Fedha kwenye Boston Marathon akitumia muda wa Saa 2:05:04, nyuma ya John Korir wa Kenya aliyemaliza ndani ya Saa 2:04:45, wakati mshindi wa tatu alikuwa ni Cybrian Kotut wa Kenya pia aliyetumia Saa 2:05:04.
Simbu (34) ni Bingwa wa Dunia wa Riadha wa Mbio Ndefu, Marathon aliyeshinda taji hilo katika Mashindano ya mwaka jana, 2025 Jijini Tokyo nchini Japan na kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda Medali ya Dhahabu ya Ubingwa wa Dunia au Olimpiki.
Rekodi nyingine nzuri za Simbu katika Riadha Kimataifa ni kushinda Medali ya Shaba katika Mashindano ya Dunia mwaka 2017 Jijini London, Uingereza na Medali ya Fedha kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 2022 Jijini Birmingham nchini Uingereza, zote kwenye Marathon pia.
Gwiji,Juma Ikangaa na Mwanariadha Mstaafu wa JWTZ ndiye anayeshikilia rekodi nzuri zaidi kwenye Boston Marathon kufuatia kushinda Medali ya Fedha mara tatu mfululizo 1988, 1989 na 1990), mwaka 1988 akitumia muda wa Saa 2:08:44.
Mwanariada mwngine wa Tanzania aliyewahi kushinda Medali kwenye Boston Marathon ni Gabriel Geay ambaye naye alishinda Fedha mwaka 2023 akitumia muda wa Saa 2:06:04.


.png)
0 comments:
Post a Comment