• HABARI MPYA

    Monday, October 01, 2018

    TAIFA STARS YAINGIA KAMBINI ‘HOTELI YA SIMBA’ KUJIANDAA NA MECHI DHIDI YA CAPE VERDE KUFUZU AFCON

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinatarajiwa kuingia kambini leo kwenye hoteli ya Sea Scape iliyopo Kunduchi mjini Dar es Salaam kujiandaa na mechi mbili za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Cape Verde.
    Hoteli ya Sea Scape ndiko Simba SC walitokea jana kwenda kutoa sare ya bila mabao na mahasimu wao, Yanga SC katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara. 
    Taifa Stars watakuwa wageni wa Cape Verde katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON Oktoba 12 mjini Praia kabla ya kurejea Dar es Salaa kwa mchezo wa marudiano na wapinzani wao hao Oktoba 16.
    Kambi hiyo inayoanza leo itaanza na wachezaji wanaocheza ndani kabla ya kuungana na wale wanaocheza nje ya Tanzania.
    Mazoezi ya Taifa Stars yanatarajiwa kuanza kesho asubuhi kwenye Uwanja wa JKM Park, Mnazi Mmoja.
    Maandalizi yatakuwa chini ya Kocha Mkuu Emmanuel Amunike,Wasaidizi Hemed Morocco na Emeka Amadi, Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya
    Kikosi kilichoitwa kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Simba SC), Beno Kakolanya (Yanga SC) na Mohamed Abdulahman (JKT Tanzania).
    Mabeki; Hassan Kessy (Nkana FC/Zambia), Shomari Kapombe (Simba SC), Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Gardiel Michael (Yanga SC), Paulo Ngalema (Lipuli FC), Ally Sonso (Lipuli FC), Aggrey Morris (Azam FC), David Mwantika (Azam FC), Abdallah Kheri (Azam FC), Kelvin Yondani (Yanga SC), Andrew Vicent (Yanga SC) na Abdi Banda (Baroka FC).
    Viungo ni Himid Mao (Petrojet/Misri), Simon Msuva (Difaa Hassan El –Jadida/Morocco), Mudathir Yahya (Yanga SC), Frank Domayo (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Feisal Salum (Yanga SC), Salum Kihimbwa (Mtibwa Sugar) na Farid Mussa (CD Tenerife/Hispania).
    Washambuliaji; Mbwana Samatta (Nahodha, KRC Genk/Ubelgiji), Thomas Ulimwemgu (Al Hilal/Sudan), John Bocco (Simba SC), Yahya Zayd (Azam), Kelvin Sabato (Mtibwa Sugar), Rashid Mandawa (BDF XI/Botswana) na Shaaban Iddi Chilunda (CD Tenerife/Hispania).
    Amunike anasaidiwa na Hemed Suleiman ‘Morocco’ na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi, wakati Mtunza Vifaa ni Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya.
    Tanzania inashika nafasi ya tatu katika Kundi L ikiwa na pointi mbili tu baada ya sare zote katika mechi zake mbili za mwanzo, 1-1 na Lesotho nyumbani mwaka jana na 0-0 na Uganda ugenini mapema mwezi huu.
    Uganda wanaendelea kuongoza Kundi hilo kwa pointi zao nne, wakifuatiwa na Lesotho mbili sawa na Tanzania na mabao mawili ya kufunga, wakati Cape Verde wanashika mkia kwa pointi yao moja. 
    Kihistoria Tanzania imecheza fainali moja tu za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria, tena enzi hizo bado zinajulikana kama Fainali za kombe la Mataifa Huru ya Afrika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS YAINGIA KAMBINI ‘HOTELI YA SIMBA’ KUJIANDAA NA MECHI DHIDI YA CAPE VERDE KUFUZU AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top