• HABARI MPYA

  Monday, January 02, 2017

  PASTORY ATHANAS ANAYEANDALIWA KURITHI MIKOBA YA HAJIB SIMBA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WAKATI mshambuliaji Ibrahim Hajib akiwa mbioni kuondoka Simba, tayari Wekundu hao wa Msimbazi wamepata mrithi wake.
  Na huyo si mwingine zaidi ya mshambuliaji chipukizi, Pastory Athanas aliyesajiliwa dirisha dogo mwezi huu kutoka Stand United ya Shinyanga.
  Akiichezea kwa mara ya kwanza Simba SC juzi katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Ruvu, Pastory alionyesha kiwango kizuri na kuwavutia maelfu ya mashabiki waliokusanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Alionyesha uwezo mzuri wa kumiliki mpira, kasi, kuwatoka na kuwapita wachezaji wa timu pinzani, kutoa pasi kwa wenzake, krosi nzuri na kwa ujumla kucheza kama mchezaji wa timu.
  Pastory Athanas amesajiliwa Simba dirisha dogo mwezi huu kutoka Stand United ya Shinyanga

  Akiwa amesimamishwa kama mshambuliaji pekee siku hiyo, Pastory aliisumbua ngome ya JKT Ruvu na akashindwa kufanya kitu kimoja tu katika siku yake ya kwanza kabisa ya kuichezea Simba, kufunga.
  Lakini badala yake, akaseti bao pekee la ushindi la Simba siku hiyo lililofungwa dakika ya 45 na kiungo Muzamil Yassin aliye katika msimu wake wa kwanza Msimbazi baada ya kusajiliwa kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro.
  Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog akamuacha Athanas amalizie na kipindi cha pili na kijana huyo akaonyesha uimara wa mapafu yake, kwa kucheza kwa kasi na nguvu ile ile, tena akianza na kumaliza dakika zote 90 kama mshambuliaji pekee.
  Athanas alikuwa anaonekana karibu kila sehemu ulipo mpira kwenye eneo la wapinzani wao– maana yake alikuwa anacheza kwa kujituma mno, jambo ambalo ni adimu kwa wachezaji wengi wa siku hizi.
  Katika siku ya kwanza tu ya kucheza kwake akiwa amevalia jezi ya Simba, Pastory ameonyesha ni mchezaji mzuri na hazina ya taifa baadaye.       
  Ameonyesha uwezo ambao unaweza kumshawishi mtu yeyote kusema kijana huyo ni zaidi ya washambulaiji wengi wa kigeni wanaosajiliwa kwa dola nyingi za Kimarekani nchini.
  Kijana huyo aliyeibuliwa na Stand United anawafanya watu waamini, taifa bado lina kizazi cha wachezaji wazuri, lakini tatizo hawafikiwi kutokana na klabu zetu kuelekeza fikra zaidi katika kusajili wachezaji wa kigeni. 
  Wazi baada ya mchezo mzuri alioonyesha juzi, Pastory Athanas sasa ataanza kusifiwa na vyombo vya habari nchini na kiwango chake cha Jumamosi dhahiri kinamtengenezea nafasi ya kuitwa hadi timu ya taifa.
  Anapaswa kuinamisha kichwa chake chini na kujitafakari baada hayo yote, kwamba yametokana na nini. Bila shaka ni uwezo wake wa kisoka, uliotokana na bidii ya mazoezi bila shaka, nidhamu na kusikiliza kwa makini mafundisho ya makocha.
  Hivyo basi, Pastory Athanas atahitaji kuendelea kuwa yule yule, kijana mtiifu, mwenye bidii ya mazoezi, kujituma na kusikiliza mafundisho wa walimu wake, ili aendelee kuwa mchezaji bora zaidi na kukuza zaidi kiwango chake.
  Simba ilivutiwa na mchezaji huyo baada ya kuwafunga mahasimu wao wa jadi, Yanga SC wakilala 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara – na sasa kijana huyo amehamishia makali yake Msimbazi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PASTORY ATHANAS ANAYEANDALIWA KURITHI MIKOBA YA HAJIB SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top