• HABARI MPYA

  Monday, January 02, 2017

  EMMANUEL MARTIN: WINGA MPYA MACHACHARI YANGA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  BAADA ya kusaini mkataba wa kufundisha Yanga mwezi Novemba mwaka jana, kocha Mzambia George Lwandamina aliiongoza timu kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya JKU ya Zanzibar.
  Aliomba mchezo huo ili awajue vizuri wachezaji na kutengeneza kikosi cha kwanza kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Bahati mbaya, Lwandamina alianza vibaya Yanga ikichapwa mabao 2-0 na JKU Uwanja wa Dar es Salaam, mabao yote yakifungwa na chipukizi Emmanuel Martin aliyetumia vizuri makosa ya mabeki wa timu ya Jangwani.
  Winga Emmanuel Martin amesajiliwa Yanga SC kutokqa JKU ya Zanzibar

  Ikaelezwa baada ya mchezo huo, Lwandamina aliwaambia viongozi wa Yanga wafanya kinachowezekana wahakikishe wanamsajili mfungaji wa yale mabao. Na uongozi wa Yanga haukufanya ajizi, kweli ukamsaini mchezaji huyo.
  Martin sasa ni mchezaji wa Yanga na tayari amekwishacheza mechi mbili, ya kwanza akitokea benchi kuchukua nafasi ya Deus Kaseke dakika ya 65 timu yake mpya ikilazimisha sare ya 1-1 na African Lyon Uwanja wa Uhuru.
  Martin alipoingia akaenda kucheza vizuri mno na kuisaidia Yanga kupeleka mashambulizi mengi ya hatari langoni mwa Lyon, ingawa bahati siku hiyo haikuwa yao.
  Kwa kiwango kizuri alichoonyesha kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Lyon, kocha wa Yanga, Lwandamina akazidi kuvutiwa naye na haikushangaza katika mchezo uliofuata dhidi ya JKT Ruvu akamuanzisha kijana hiyo.
  Kwa mara nyingine, Martin akaitumia vizuri fursa hiyo kwa kucheza vizuri tena na kuwafurahisha mashabiki wa Yanga.
  Na Martin anafuata nyayo za chipukizi wengine waliokuwa wana mwanzo mzuri baada ya kusajiliwa Yanga kama Juma Mahadhi, Geoffrey Mwashiuya na Malimi Busungu.
  Wote hao walikuwa wana mwanzo mzuri Yanga baada ya kusajiliwa, lakini baadaye wakapoteza makali yao na sasa wamekuwa wachezaji wa kawaida. 
  Japokuwa maumivu yanahusishwa pia kuwarudisha nyuma, lakini wengine wanaamini hata mabadiliko ya mfumo wao wa kimaisha baada ya kuanza kulipwa vizuri Yanga ndiyo sababu ya kushuka kwao.
  Ajali mbili alizopata Busungu ndani ya miezi miwili mkoani Morogoro zinaibua maswali – je zote zilitokea kwa bahati mbaya, au labda uendeshaji mbaya na ulevi ulichangia?
  Kwa ujumla inaelezwa vijana wanatumbukia kwenye dimbwi la anasa na ulevi baada ya kusajiliwa na timu zinazolipa vizuri na ndiyo maana hupoteza uwezo wao ndani ya muda mfupi.
  Wana Yanga wanakumbuka Septemba 26, mwaka 2015 wakati Malimi Busungu anatokea benchi na kwenda kuseti bao lililofunes na Amissi Tambwe kabla yeye mwenyewe kufunga la pili, au namna Juma Mahadhi alivocheza vizuri akiichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza kwenye mechi na TP Mazembe ya DRC katika hatua ya makundi Kombe la Shirikisho.
  Na baada ya Martin pia kuanza vizuri Yanga, watu wanamfuatilia sasa kujua kama atauendeleza moto wake huo, au atakuwa kama wale wale wanaoanzakwa kisindo, halafu wanapotea baada muda mfupi?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: EMMANUEL MARTIN: WINGA MPYA MACHACHARI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top