• HABARI MPYA

    Monday, January 02, 2017

    AZAM YAANZA VYEMA KOMBE LA MAPINDUZI

    Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
    BAO pekee la mshambuliaji chipukizi, Shaaban Iddi Chilunda limetosha kuipa Azam FC ya Dar es Salaam ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Zimamoto katika mchezo wa Kundi B Kombe la Mapinduzi.
    Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar jioni ya leo, Chilunda alifunga bao hilo dakika ya 79 akimvisha kanzu kipa baada ya kuipokea kiufundi kwa kifua pasi ya juu ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’. 
    Ushindi huo unaifanya Azam FC kuongoza Kundi B ikiwa na pointi tatu, ambapo hivi sasa itasubiria mchezo wa pili wa kundi hilo utakazoihusisha Yanga na Jamhuri ili kujua kama itaendelea kukaa kileleni.
    Winga wa kushoto wa Azam FC kutoka Ghana, Enock Atta Agyei, alianza kuichezea mechi ya kwanza ya mashindano timu hiyo tokea aliposajiliwa, hii ni baada ya kushindwa kuitumikia kwenye Ligi Kuu kufuatia kutotimiza umri wa miaka 18, ambapo kwenye ligi ataanza kuonekana baada ya kutimiza umri huo Januari 5 mwaka huu.
    Shaaban Iddi (katikati) akipongezwa na wachezaji wenzake baada ya kufunga jana

    Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii walianza mchezo huo kwa kasi ya chini kabla ya kubadilika dakika 20 za mwisho za kipindi cha pili, ambapo mshambuliaji Samuel Afful, alikaribia kuiandikia bao la uongozi Azam FC dakika ya 30 baada ya kuwatoka mabeki wa Zimamoto lakini shuti alilopiga lilimbabatiza kipa na kuokolewa na mabeki.
    Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu zote ziliweza kutoka nguvu sawa ya bila kufungana, katika dakika 10 za mwanzo za kipindi cha pili Azam FC ilifanya mabadiliko ya kumtoa Afful na kuingia Shaaban ambaye alienda kufunga bao la ushindi.
    Kabla ya kufunga bao hilo, Shaaban huenda angetangalia kufunga jingine kama angekuwa makini kutumia pasi safi ya Enock Atta Agyei dakika ya 59, lakini aliukosa mpira wakati kiwa kwenye harakati za kuupiga mpira.
    Azam FC iliweza kuulinda ushindi huo hadi dakika 90 zinamalizika, ambapo itashuka tena dimbani Keshokutwa Jumatano kucheza dhidi ya Jamhuri mchezo utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar saa 2.15 usiku.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue, Salum Abubakar, Frank Domayo/Mudathir Yahya dk 77, Yahaya Mohammed, Samuel Afful/Shaaban Idd dk 50, Enock Atta/Ramadhan Singano dk 67. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM YAANZA VYEMA KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top