• HABARI MPYA

    Friday, February 19, 2016

    BOCCO: HATUKUJA KUUZA SURA MBEYA, TUMEFUATA POINTI SITA

    Na Mwandishi Wetu, MBEYA
    NAHODHA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo, akiwaambia kuwa walichofuata jijini Mbeya ni kuondoka na pointi sita katika mechi mbili dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons.
    Kauli ya nahodha Bocco imekuja baada ya Azam FC kupoteza mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Coastal Union (1-0) na kuhitimisha rekodi yao ya kutopoteza mechi ya ligi tokea Mei 2, mwaka jana ilipofungwa na Simba mabao 2-1.
    Azam FC itaanza kusaka pointi tatu muhimu jijini Mbeya kesho saa 10.00 jioni (Februari 20) kwa kuvaana na Mbeya City, ambao kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza walifungwa mabao 2-1 katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
    Nahodha wa Azam FC, John Bocco amesema wamefuata pointi sita Mbeya dhidi ya Mbeya City na Prisons

    Mabingwa hao wa Kombe la Kagame watamalizia mtihani wa mwisho jijini Mbeya Jumatano ijayo (Februari 24) kwa kucheza mechi ya kwanza ya kiporo dhidi ya Tanzania Prisons, ambao walikubali kichapo cha mabao 2-1 kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.
    Bocco alisema wamejiandaa vizuri kuchukua pointi tatu katika kila mchezo licha ya ugumu watakaokutana nao.
    “Mechi zote zitakuwa ngumu, tunaiheshimu Mbeya City ni timu nzuri imeleta ushindani mzuri hata hivi sasa ipo nafasi nzuri, wanajitahidi kusema kweli, lakini naamini tumejiandaa vizuri na tutachukua pointi tatu katika kila mechi dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons,” alisema.
    Bocco alimalizia kwa kuwaambia mashabiki wa Azam FC wazidi kuwaamini na wasahau yote yaliyopita kwenye mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union kwani mpira ndio ulivyo siku nyingine unaweza kupata matokeo unayoyatarajia na siku nyingine ukayapata usiyoyatarajia.
    “Lengo letu lilikuwa ni kushinda lakini tuliweza kupoteza mchezo huo uliopita, ya nyuma tunayaacha na tunafikiria ya mbele ili kuweza kupata pointi tatu,” alisema.
    Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB ikifanikiwa kushinda mechi hizo mbili, itaweza kurejea kileleni kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 48 na hii ni kama wapinzani wake Simba na Yanga walio juu yake watatoka sare kesho katika mchezo wao.
    Lakini matajiri hao wa Azam Complex bado watakuwa wamebakiwa na kiporo cha mchezo mmoja dhidi ya Stand United utakaofanyika Machi 16, mwaka huu jijini Dar es Salaam, ambao wakiushinda utawafanya kujikita zaidi kileleni kama mahesabu yatakwenda vizuri. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BOCCO: HATUKUJA KUUZA SURA MBEYA, TUMEFUATA POINTI SITA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top