• HABARI MPYA

    Thursday, July 17, 2014

    SERENGETI BOYS ILIVYO TAYARI TAYARI KUWAADHIBU WAAFRIKA KUSINI CHAMAZI KESHO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kesho inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Afrika Kusini ‘Amajimbos’ katika mchezo wa kwanza Raundi ya Kwanza kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika.
    Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na Amajimbos tayari wapo Dar es Salam tangu juzi, wakiwa wamefikia katika hoteli ya Sapphire Court, Kariakoo.
    Katika mahojiano na BIN ZUBEIRY leo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam baada ya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo, Kocha wa Serengeti Boys, Hababuu Ali anasema ana matumaini ya matokeo mazuri kesho. 
    Jeshi la Ushindi; 11 wa kwanza wa Serengeti wanaoanza kesho

    Hababuu ‘Mwana Zanzibar’ anasema kwamba hiyo inatokana na maandalizi waliyofanya, tangu walipoingia kambini Juni 23, mwaka huu na kuanza rasmi mazoezi siku iliyofuata.
    “Kwa kweli maandalizi ni mazuri na morali ya vijana pia iko juu, hamasa ni kubwa, jana Rais wa TFF (Jamal Malinzi) alitutembelea na kuzungumza nasi, kutupa moyo, kwa kweli tupo vizuri,”anasema.
    Kocha Hababuu Ali hana wasiwasi 

    Hababuu anasema katika kipindi chote cha kuwa kambini, pamoja na programu nzuri za mazoezi, lakini pia alipata mechi tatu za kujipima nguvu dhidi ya timu za wakubwa.
    Anasema mechi ya kwanza walicheza na Polisi Moro iliyorejea Ligi Kuu msimu huu na kufungwa mabao 5-0 kabla ya kuifunga U20 ya Azam mabao 2-1 na kufungwa 2-1 na timu ya Daraja la Kwanza, Friends Rangers.
    Baraka Yussuf anatarajiwa kuibeba Serengeti Boys kesho 
    Omar Wayne tegemeo la Serengeti Boys

    “Katika maandalizi yetu kwa kweli timu imekuwa ikiimarika siku hadi siku, tumekuwa tukiona mabadiliko hata katika mechi tunazocheza, kutoka ile tuliyofungwa 5-0, tukashinda 2-1 na kufungwa 2-1, timu imeimarika sana na iko tayari,”anasema.
    Kuhusu wapinzani wao, Hababuu anasema wakati timu ya taifa ya wakubwa ya Tanzania, Taifa Stars ilipokuwa kambini Botswana na Amajimbos walikuwa kambini pia nchini humo na kucheza mechi za kirafiki.
    “Hivyo kupitia kocha wa Taifa Stars (Mholanzi Mart Nooij) tumepata taarifa za wapinzani wetu. Lakini na jana tuliwaona hapa wakifanya mazodezi, hatuna wasiwasi nao. Kikubwa katika timu ni mipango yenu, hayo ya wapinzani yanafuatia,”anasema.
    Hababuu anawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kesho Chamazi kuisapoti timu yao ya taifa iweze kushinda mchezo huo, kwani kufanya hivyo kutawatia moyo wa kujituma zaidi vijana wake.
    Kikosi kamili cha Serengeti kilichokuwa kambini

    “Shabiki ni mchezaji wa 12, mimi ninaomba sana kwa kweli, Watanzania, wake kwa waume wajitokeze kwa wingi kesho kuisapoti timu,”amesema mwalimu huyo anayesaidiwa na Manyika Peter, kocha wa makipa na Muingereza Stewart Hall ambaye ni Mshauri wa Ufundi.  
    Hababuu kesho anatarajiwa kuwaanzisha; Mitacha Mnacha langoni, beki ya kulia Abdallah Jumanne, kushoto Issa Baky, katikati Adolph Mutasingwa na Martin Kiggi, kiungo mkabaji Omar Wayne, kiungo wa kulia Athanas Mdam, wa katikati Ali Mabuyu, washambuliaji Abdul Bitebo, Prosper Mushi na Baraka Yussuf.
    Kwenye benchi wanatarajiwa kuwapo Abdulatif Hamidu, Mashaka Said, Badru Haji, Seif Said, Nazir Abdul, Hatibu Yassin, Amini Mohamed, Mussa Shaaban na Omar Ame.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERENGETI BOYS ILIVYO TAYARI TAYARI KUWAADHIBU WAAFRIKA KUSINI CHAMAZI KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top