• HABARI MPYA

  Thursday, August 01, 2013

  SAKATA LA AZAM NA BANDARI LAFIKA PATAMU, ZFA WAIENGUA MALINDI LIGI KUU

  Na Salum Vuai, Zanzibar, IMEWEKWA AGOSTI 1, 2013 SAA 6:48 USIKU
  CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA), kimetoa ratiba ya ligi kuu ya Grand Malt msimu wa 2013/2014, huku kikiiengua timu ya Malindi SC ambayo imenunua daraja la Bandari SC, hadi chama hicho kitakapolipwa shilingi milioni saba kwa mujibu wa kanuni zake. 
  Rais wa ZFA Ravia Idarous Faina, ameliambia gazeti hili kuwa, kanuni ya chama hicho imeelekeza kuwa, timu inayouza nafasi yake ya ligi kuu kwa klabu nyengine, inalazimka kukilipa chama hicho shilingi milioni saba, vyenginevyo mauziano hayo hayatatambuliwa. 
  Bilionea; Mfanyabiashara bilionea, Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa aliinuanua Bandari iwe mali ya kampuni yake, Azam Marine, lakini uongozi wa Bandari ukawekwa vikwao. 

  Wiki kadhaa zilizopita, uongozi wa Malindi SC ulimalizana na Shirika la Bandari kwa kulilipa shilingi milioni tano, kwa ajili ya wakongwe hao wa mtaa wa Funguni kushiriki ligi kuu baada ya awali kuteremka daraja.
  Hata hivyo, alipoulizwa Katibu Mkuu wa Malindi juu ya hatua ya ZFA kutokuipanga timu yake kwenye ratiba hiyo ambapo imeweka alama ya 'X' kuonesha kuwa nafasi hiyo haina mwenyewe, kiongozi huyo hakuwa tayari kuzungumzia hali hiyo, zaidi ya kumwambia mwandishi wa habari hizi aandike atakavyo.
  "Nyie si mliandika Bandari imeiuzia daraja Azam, basi andika hivyo hivyo, hiyo alama ya 'X' ni nafasi ya Azam FC' sio ya Malindi, alisema Masoud kwa ghadhabu. 
  Naye Katibu wa Bandari SC Silima Makame Silima, alisema suala la mauziano ya nafasi yao limemalizika, na kwa mujibu wa makubaliano yao, waliitaka Malindi kubeba dhima ya masharti yote mengine yatakayotakiwa na ZFA.
  “Sisi na Malindi tumemalizana, na timu yetu haishiriki ligi kuu, kama kuna jengine watatambuana na ZFA”, alisema Silima.
  Ratiba ya ligi hiyo iliyotolewa na ZFA, inaonesha kuwa itaanza Septemba 5, mwaka huu kwa michezo miwili, ambapo maafande wa Mafunzo watawavaa maustaadh wa Chuoni kwenye uwanja wa Amaan, huku zulia la Gombani likiyakaribisha madaluga ya Chipukizi na Fufuni SC.
  Ligi hiyo itafunguliwa kwa mchezo wa Ngao ya Hisani Septemba 1, 2013 utakaowapambanisha mabingwa watetezi KMKM na makamu bingwa timu ya Chuoni.
  Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Septemba 6, itakuwa zamu ya Kizimbani na Jamhuri katika uwanja wa Gombani Chake Chake Pemba, na katika uwanja wa Amaan kutakuwa na mchezo kati ya maafande wa Polisi waliorudi baada ya kuteremka msimu uliopita, na Malindi ambayo hadi sasa hatima yake haijulikani kutokana na ZFA kudai ada ya shilingi milioni saba, fedha za mazuiano ya nafasi ya Bandari.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SAKATA LA AZAM NA BANDARI LAFIKA PATAMU, ZFA WAIENGUA MALINDI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top