• HABARI MPYA

    Monday, August 12, 2013

    NOMVETHE ASEMA AZAM INATISHA, AITABIRIA KUFIKA MBALI AFRIKA...ASEMA MWAIKIMBA KIWANGO CHA PSL

    Na Mahmoud Zubeiry, Soweto, Afrika Kusini
    IMEWEKWA AGOSTI 12, 2013 SAA 3:52 USIKU
    MSHAMBULIAJI mkongwe wa kimataifa wa Afrika Kusini, Siyabonga Eugene Nomvethe amesema kwamba Azam FC ni timu nzuri na inaweza kufika mbali katika michuano ya Afrika mwakani na pia hata kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo baada ya mchezo baina ya timu hizo Uwanja wa Volkswagen Dobsonville mjini Soweto, Nomvethe alisema kwamba amecheza na Azam amegundua ni timu nzuri sana.
    Nomvette akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Azam leo baada ya mechi

    “Ni timu nzuri, inacheza kama timu, imetupa ushindani mzuri leo, kwa kweli kama wataendelea hivi, watafika mbali. Nasikia watacheza Kombe la Shirikisho, wanaweza kufika mbali. Hata kwenye Ligi yao, wanaweza kuwa mabingwa,”alisema.
    Alipoulizwa kuhusu uwezo wa wachezaji mmoja mmoja kama wanaweza kuhimili vishindo vya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), Nomvethe alisema wanaweza.
    Akasema ameona watu kadhaa katika safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji wenye uwezo wa kucheza PSL, ingawa alikataa kuwataja majina.  
    Wakati anazungumza na BIN ZUBEIRY akatokea mshambuliaji wa Azam FC, Gaudence Mwaikimba na Nomvette akamtolea mfano; “Huyu mwenye mwili mkubwa muhimu sana”alisema Nomvethe huku akicheka.
    Mwaikimba alifurahia mno kauli hiyo ya Nomvethe na akamtaka mwandishi wa BIN ZUBEIRY aende kuwapa ujumbe huo Watanzania, wanaomuona yeye hawezi.
    “Unamsikia, Nomvethe anasema mimi kifaa, lakini bongo naonekana galasa, haya kawaambie Watanzania, kwamba watu wenye kujua soka wamenipitisha, wao wabaki na majungu yao,”alisema Mwaikimba.
    Nomvethe aliyezaliwa Desemba 2, mwaka 1977 amecheza Ligi kadhaa Ulaya kabla ya kuamua kuja kumalizia soka yake Moroka Swallows. Nomvethe ameichezea Bafana Bafana tangu Mei 6, 1999 na amecheza Fainali za Kombe la Dunia 2002 na 2010.
    Aliibukia African Wanderers ya kwao, 1997 kabla ya mwaka 1998 kuhamia Kaizer Chiefs alikocheza hadi 2001 akahamia Udinese ya Italia, alikocheza hadi 2004 akahamia Salernitana ya nchini humo kwa mkopo na mwaka huo huo akahamia Empoli kwa mkopo pia kabla ya 2005 kutua Djurgarden ya Sweden na mwaka 2006 akarejea Orlando Pirates alikocheza hadi 2009 akahamia AaB alipocheza kwa muda mfupi kabla ya kutua Moroka Swallows.
    Azam le imehitimisha ziara yake ya Afrika Kusini kwa kipigo cha bao 1-0 mbele ya wenyeji, Moroka Swallows kwenye Uwanja wa Volkswagen Dobsonville mjini Soweto.
    Huo ulikuwa mchezo wa tatu kwa washindi hao wa pili wa Ligi Kuu Bara misimu miwili mfululizo kufungwa hapa, baada ya awali kuchapwa 3-0 na Kaizer Chiefs, 2-1 na Orlando Pirates, wakati mchezo pekee iliyoshinda ni dhidi ya Mamelodi Sundowns 1-0. 
    Katika mchezo wa jana, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika bila bao, huku wageni ndiyo wakipoteza nafasi tatu za kufunga, mbili kupitia kwa Khamis Mcha ‘Vialli’ na moja Himid Mao.
    Ilikuwa dakika ya 40, wakati Mcha alipopewa pasi nzuri na Jabir Aziz, lakini akiwa amebaki na kipa akagongesha mwamba na mpira ukarudi uwanjani, ukamkuta Himid Mao kwenye nafasi nzuri, akapiga juu ya lango.
    Awali ya hapo, Mcha tena alipewa pasi nzuri na Waziri Salum, lakini akiwa amebaki na kipa akapiga shuti lililomlenga kipa, akadaka dakika ya 37.   
    Kipindi cha pili, Moroka walibadilisha karibu timu nzima na miongoni mwa walioingia ni mshambuliaji mkongwe wa kimataifa wa Afrika Kusini, SIyabonga Nomvette.
    Nomvette ambaye pamoja na kuonekana kasi yake imepungua, ameonyesha bado ana uwezo na alipata nafasi nzuri ya kufunga akiwa amebaki na kipa dakika ya 75, lakini shuti lake likapanguliwa na kipa Aishi Manula na kuwa kona, ambayo haikuzaa matunda.  
    Moroka ilipata bao lake pekee dakika ya 70, mfungaji Mnigeria, Felix Obada aliyetokea pembeni na kufumua shuti akiwa nje ya 18.
    Azam ambayo nayo pia ilibadilisha karibu timu nzima iliyoanza, ilijitahidi kusaka bao la kusawazisha, lakini bahati haikuwa yao.
    Kocha Mreno wa Moroka, Zeka Marquees aliisifu Azam baada ya mechi hiyo kwamba ni timu nzuri na akaitabiria kufika mbali katika Kombe la Shirikisho mwakani.
    Muingereza Stewalt Hall wa Azam alisema timu yake ilicheza vizuri na ilishindwa kutumia nafasi ilizopata, wakati wapinzani walitumia nafasi yao. 
    Baada ya mchezo wa jana, Azam inaondoka leo kurejea nyumbani, Dar es Salaam na Agosti 17, itacheza mechi ya kuwania Ngao, dhidi ya Yanga SC Uwanja wa Taifa. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NOMVETHE ASEMA AZAM INATISHA, AITABIRIA KUFIKA MBALI AFRIKA...ASEMA MWAIKIMBA KIWANGO CHA PSL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top