• HABARI MPYA

    Wednesday, August 14, 2013

    MCHEZAJI WA TANZANIA ANAVYOTIA HURUMA NA TENGA NDIYE RAIS WA TFF

    IMEWEKWA AGOSTI 14, 2013 SAA 4:03 ASUBUHI
    MOJA kati ya njia za kuifanya Ligi Kuu ya Tanzania Bara iwe bora ni kuboresha ushindani, kwa kuwatengenezea wachezaji kujiamini ili waweze kushindana bila woga.
    Namaanisha mchezaji kuwa na bima, ambayo itamfanya ajiamini hata akiumia wakati wowote atatibiwa na atalipwa wakati anajiuguza.
    Katika ligi yetu hilo halipo, ingawa kwa muda mrefu sasa limekuwa likipigiwa kelele kama ilivyo suala la upimwaji vipimo vya dawa za kulevya kwa wachezaji, lakini halipewi uzito wowote.
    Tunataka ligi ya ushindani, lakini wachezaji hawawezi kushindana kwa asilimia zote kwa kuogopa kuumia, wakijua kabisa wakiumia ni mwanzo wa kutelekezwa na klabu zao.

    Shamte Ally anaachwa Yanga hivi sasa akiwa bado ana uwezo wa kuendelea kucheza, sababu tu ni maumivu aliyoyapata akiwa katika klabu hiyo yamepunguza kasi yake ya mchezo.
    Hakuna hakika kama Shamte alipatiwa tiba mwafaka alipoumia- au ilikuwa ya kubabaisha tu ili mradi arejee uwanajani. 
    Sahau kuhusu Shamte, Kiggi Makassy ameumia akiwa anaitumikia Simba SC msimu uliopita, lakini hadi leo suala la kupatiwa tiba na klabu hiyo limekuwa gumu. Kiggi anateseka.
    Lakini kama kungekuwa na kanuni madhubuti katika Ligi yetu za kuwalinda wachezaji wetu, haya yote yasingetokea. Mchezaji baada ya kuumia, bima yake ingefanya kazi. Asingesumbuana na klabu.
    Lakini tumeweza yote na tunashughulikia mengine mengi hadi kuboresha mapato kwa kuleta tiketi za umeme, ila tumeshindwa suala la bima tu kwa wachezaji. Huyu mchezaji wa Tanzania anachukuliwa kama binadamu au punda tu asiye na thamani yoyote?
    Ajabu tunashindwa kumthamini mchezaji, wakati yeye ni ndiye kila kitu katika soka. Bila wachezaji, soka itatoka wapi? Nani ataongoza timu. Nani atakwenda uwanjani kutazama mechi.
    Inasikitisha zaidi, mchezaji hathaminiwi wakati ambao Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ni mwanasoka wa zamani, tena wa kimataifa nchini.
    Na Tenga anayajua machungu ya kuumia, kwani naye pia maumivu ndiyo yaliyomuondoa uwanjani mapema, lakini ajabu amemaliza muda wake kwa vipindi viwili na hajafanikiwa kuwezesha wachezaji kukatiwa bima.
    Bado mashabiki na viongozi wanalalamika, wachezaji wetu hawajitumi ndyo maana timu ya taifa haifanyi vizuri, ajitume ana bima?
    Wakati mwingine mashabiki nao ni wabinafsi kama viongozi wa soka ya nchi hii. Wanajifikiria wao tu, washangilie burudani ya soka nzuri na mabao bila kujua mchezaji ana bima au vipi.
    Leo Kiggi Makassy kaumia akiwa ana rekodi ya kuifungia mabao mazuri hadi Taifa Stars, Simba na Yanga- je, shabiki gani anayemkumbuka wakati huu yeye anateseka na mkewe nyumbani kwake? 
    Wakati umefika sasa, kupanda kwa hadhi ya Ligi Kuu kama hivi sasa imefikia hadi kuuza haki za matangazo ya Televisheni, kuendane na kumthamini mchezaji, kwa kuhakikisha kabla hajaingia uwanjani anakuwa na bima.
    Tuweke sheria na kusimamia utekelezaji wake, kwamba mchezaji ambaye hana bima haruhusiwi kucheza Ligi Kuu na hapo klabu zitalazimika kuwakatia bima wachezaji, vinginevyo wataishia kufanya mazoezi na ligi hawachezi. Jumatano njema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MCHEZAJI WA TANZANIA ANAVYOTIA HURUMA NA TENGA NDIYE RAIS WA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top