• HABARI MPYA

    Monday, August 12, 2013

    KAMA TUNATAKA MAFANIKIO TAIFA STARS, KAULI YA STEWART IFANYIWE KAZI

    IMEWEKWA AGOSTI 12, 2013 SAA 1:11 ASUBUHI 
    KATIKATI ya wiki iliyopita, kocha wa klabu ya Azam FC, Stewart John Hall, alikaririwa akieleza masikitiko yake juu ya kushuka kwa kiwango cha golikipa wake Mwadini Ali.
    Muingereza huyo alieleza hayo baada ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa, kati ya timu yake na Kaizer Chiefs uliochezwa huko Afrika Kusini, ambapo Azam ililala kwa mabao 3-0.
    Stewart alidai kuwa, pamoja na uzuri wake, Mwadini amejikuta akicheza chini ya kiwango kinachotarajiwa, kwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars Kim Poulsen, hampangi katika mechi za kimataifa.
    Masikitiko ya Stewart, ni kwamba kwa muda wote tangu aitwe Taifa Stars, Mwadini hajawahi kucheza hata mechi moja ya kimataifa na badala yake Poulsen amekuwa akimtegemea zaidi Juma Kaseja pekee, hata kama mara nyengine ameruhusu kufungwa mabao mengi na rahisi.

    Katika mechi dhidi ya Kaizer Chiefs, Stewart amesema mabao yote matatu ambayo timu yake ilifungwa, yalitokana na makosa ya mlinda mlango wake Mwadini, na chanzo ni golikipa huyo Mzanzibari kukosa mechi za kimataifa akiwa na Taifa Stars.
    Tunapenda kuunga mkono kauli hiyo ya kocha Stewart kuhusu utaratibu mzima wa Poulsen katika kuwatumia wachezaji wote alionao katika kikosi chake.
    Na hilo haliko kwa upande wa mlinda mlango pekee, bali pia kwa wachezaji wa nafasi nyengine kwani kwa muda sasa, Taifa Stars inaonekana kama timu ya wateule wachache na wengine ni wasugua benchi tu.
    Hatukatai kwamba katika timu yoyote ile mwalimu ndiye mwenye maamuzi ya mwisho kupanga wachezaji anaohisi wanafaa kwa wakati fulani kutegemea mazingira ya mechi husika.
    Aidha, ni ukweli usiofichika kwamba timu lazima iwe na kikosi cha kwanza cha kudumu ambacho wadau wa mpira wa miguu hukiita ‘First Eleven’.
    Lakini pamoja na uhuru wa kocha kupanga wachezaji anaowataka, tunadhani nasi kama wadau tuna haki ya kumpa ushauri pale tunapoona mambo hayaendi vyema, na pengine hilo husababishwa na uchovu au uzee walionao wachezaji hao anaopenda kuwapanga.
    Hivi karibuni, Taifa Stars ilikosa nafasi ya kucheza michuano miwili ya kimataifa, ile ya Kombe la Dunia ambalo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Brazil, na CHAN ambayo inatarajiwa kuchezwa mwakani pia, huko Afrika Kusini.
    Japo katika soka kuna matokeo ya kushinda na kushindwa, lakini pale inapotokea timu ikawa ni ya kufungwa tu na kuwa mshindikizaji wa kudumu wa timu nyengine, lazima tuzinduke kwani kutakuwa na sababu iliyojificha.
    Ingawa tunakubaliana na kanuni ya ‘First Eleven’, lakini kwa hapa tulipofika Poulsen anapaswa kubadili mfumo ikiwemo pia kuwapa nafasi wachezaji wengine ambao wao wamekuwa wa kusugua benchi tu.
    Yumkini hao wenye namba za kudumu katika benchi, ndio ambao wangeweza kuivusha Tanzania kama wangelipewa nafasi kuonesha uwezo wao katika mechi za kimataifa.
    La kusikitisha, wapo baadhi ya wakalia benchi ambao hawapewi hata nafasi ya kuingia uwanjani kuchukua nafasi za wenzao wanaotolewa kupumzika au wanapoumia, kwani tayari kocha amejenga mfumo wake kwamba ameshajipangia  mchezaji gani aingie iwapo fulani atatoka.
    Lazima benchi la ufundi la Taifa Stars lijifunze kwa nchi nyengine, mathalan Zambia ambayo kikosi chake cha sasa kinaundwa na wachezaji vijana ambao wameonesha uwezo mkubwa na kuisaidia sana timu yao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KAMA TUNATAKA MAFANIKIO TAIFA STARS, KAULI YA STEWART IFANYIWE KAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top