• HABARI MPYA

    Wednesday, November 07, 2012

    SIMBA SC WAGOMA KUCHEZA NA TOTO SIKU TOFAUTI NA YANGA NA COASTAL

    Simba SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    KLABU ya Simba imesema haiko tayari kucheza mechi yake ya mwisho ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara siku tofauti na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana limetangaza kuzirudisha nyuma kwa siku moja mechi zote za mwisho za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, kutoka Jumapili wiki hii hadi Jumamosi, kasoro mechi ya Yanga na Coastal Union pekee, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    Na sababu za kutorudishwa nyuma kwa mechi ya Yanga ni kwa kuwa Jumamosi kutakuwa na mchezo mwingine wa ligi hiyo, Uwanja wa Mkwakwani, kati ya Mgambo JKT na Azam FC.
    Lakini Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba hawako tayari kucheza siku tofauti na Yanga kwa sababu ya upinzani uliopo baina yao katika mbio za ubingwa, kwani wanahofia mchezo mchafu.
    “Unajua bwana ligi hii ilipofikia ni pabaya, haiwezekani uzichezeshe Simba na Yanga siku tofauti, hivyo sisi tunawaandikia barua TFF kuwataarifu kwamba hatuko tayari kwa mabadiliko hayo,”alisema Kamwaga.
    Kulingana na mabadiliko hayo, Simba sasa itamaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Toto Africans, wakati Yanga itamaliza na Coastal Mkwakwani.     
    Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa mechi tatu za viporo kuchezwa kwenye viwanja vitatu tofauti.
    Wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Simba, Mtibwa Sugar leo wataikaribisha JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
    Coastal Union nao watashuka kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kumenyana na Polisi Morogoro, huo ukiwa mchezo wa kwanza tangu wafungwe mabao 4-1 na Azam wiki iliyopita
    Azam FC, wakiwa na kumbukumbu ya kutandikwa mabao 2-0 tena wakichezewa soka ambayo hawajawahi kuiona kwa timu nyingine yoyote ya Tanzania, wao watakuwa kwenye Uwanja wao wa Chamazi, kumenyana na JKT Oljoro
    Mechi nyingine za Jumamosi ni Mgambo JKT na Azam FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, African Lyon na Mtibwa Sugar Chamazi, Dar es Salaam, Prisons na JKT Ruvu Sokoine, Mbeya, Kagera Sugar na Polisi Morogoro, Kaitaba, Bukoba na JKT Oljoro na Ruvu Shooting Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC WAGOMA KUCHEZA NA TOTO SIKU TOFAUTI NA YANGA NA COASTAL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top