• HABARI MPYA

    Friday, November 30, 2012

    KAPOMBE NA MWINYI BADO

    Kapombe na Mwinyi kulia
    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    WACHEZAJI wawili tegemeo wa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, beki Shomary Kapombe na kiungo Mwinyi Kazimoto jana walishindwa kufanya mazoezi na wenzao, baada ya kuumia juzi kwenye mechi dhidi ya Burundi.
    Wawili hao, wako hatarini kuikosa mechi ya mwisho ya Kundi B, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge dhidi ya Somalia kesho.
    Wachezaji hao wa klabu ya Simba, wote waliumia kipindi cha pili na kutolewa, nafasi ya Kapombe ikichukuliwa na Issa Rashid wa Mtibwa Sugar nay a Mwinyi ikichukuliwa na Shaaban Nditi wa Mtibwa pia.
    Wote walitoka wakichechemea, kuashiria wamepata maumivu makali kidogo na Kocha Mkuu wa Stars, Mdenmark, Kim Poulsen alisema ataendelea kuangalia hali zao.
    Kim pia alisema kwamba sasa imetosha kuzungumzia suala la washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kama watajiunga na timu hiyo au la.
    “Kwangu sasa lazima ifikie wakati iwe inatosha, sitaki kuwazungumzia tena wachezaji hao, waulizeni TFF,”alisema Poulsen baada ya kuulizwa kama mawasiliano na klabu yao kama yanaendelea juu ya kuombea ruhusa.
    Mazembe imekataa kuwaruhusu wachezaji hao kwa sababu michuano ya Challenge haimo kwenye kalenda ya FIFA.
    Kutokana na kukosekana kwa washambuliaji hao, Stars sasa inabaki na mshambuliaji mmoja tu kikosini, John Bocco ‘Adebayor’ wa Azam FC, ambaye Watanzania wanatakiwa kumuombea dua asiumie ili aendelee kuibeba timu yao ya taifa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KAPOMBE NA MWINYI BADO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top