• HABARI MPYA

    Sunday, November 25, 2012

    KIFAA KIPYA AZAM CHATISHA KAMPALA, NI MKENYA MIENO MREFU BALAA

    Humphrey Mieno

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    MCHEZAJI mpya wa Azam, Humphrey Mieno jana alionyesha uwezo mkubwa katika mechi ya Kundi A, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge dhidi ya Uganda kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, mjini hapa.
    Akicheza kama kiungo mshambuliaji, Mieno alionyesha uwezo mkubwa wa kumiliki mpira kutulia nao, kutoa pasi na kuwazidi nguvu wachezaji wa timu pinzani katika kugombea mipira, haswa ya juu.
    Mieno ambaye ni mrefu, alikuwa akiipa wakati mgumu safu ya ulinzi ya Uganda ambayo ililazimika kumchunga mno.
    Ana akili sana ya mchezo- na wakati wote yupo mchezoni na jana mara mbili alikaribia kufunga kama si jitihada za kipa Abel Dhaira, ambaye baadaye alitoka kufuatia kuumia.
    Mieno anayechezea Sofapaka ya Kenya, ni kati ya wachezaji watatu walio mbioni kusajiliwa na Azam kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la soka Afrika (CAF).
    Wengine ni Eugene Asike kutoka Sofapaka pia na Serge Wawa Paschal raia wa Ivory Coast anayechezea El Merreikh ya Sudan. Azam FC imepania kuboresha kikosi chake katika dirisha dogo, baada ya kufukuza wachezaji wanne mwishoni mwa mzuynguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa tuhuma za kuhujumu timu hiyo.
    Wachezaji hao ni kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Erasto Nyoni, Aggrey Morris na Said Mourad, wanaodaiwa kufanya hujuma katika mechi dhidi ya Simba, Oktoba 27, mwaka huu.
    Azam imekwishasema imelifikisha suala hilo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa ajili ya hatua zaidi ili kukomesha desturi hiyo.
    Wakati Azam ikiwa katika mpango wa kusajili wachezaji watatu wapya wa kigeni, tayari kikosini ina wachezaji wanne wa kigeni, ambao ni mabeki Mkenya Ibrahim Shikanda, Mganda Joseph Owino na viungo washambuliaji Kipre Michael Balou na Kipre Herman Tcheche kutoka Ivory Coast.
    Kwa sababu hiyo, Azam itatakiwa kupunguza wachezaji wawili katika wageni wake wa sasa ili ibaki na wageni watano kulingana na kanuni za Ligi Kuu. Tayari Azam wako katika mpango wa kumuhamishia Simba SC, Owino.
    Azam pia mbali na wachezaji wa kigeni, imejipanga kusajili wachezaji wakali wa nyumbani, waliong’ara katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ili kuimarisha zaidi kikosi chake.      
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIFAA KIPYA AZAM CHATISHA KAMPALA, NI MKENYA MIENO MREFU BALAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top