• HABARI MPYA

    Sunday, November 25, 2012

    MZUNGU WA CRANES ASEMA KIIZA NA OKWI NDIO KILA KITU KAMPENI ZA UBINGWA TUSKER CHALLENGE

    Okwi wa kwanza kulia waliosimama na Kiiza mbele yake aliyeinama akiwa katika kikosi cha Uganda kilichoifunga Kenya jana 
    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Uganda, The Cranes, Bobby Williamson raia wa Scotland, amesema kwamba wachezaji Hamisi Friday Kiiza na Emmanuel Arnold Okwi ni tegemeo lake katika kampeni za kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mwaka huu mjini hapa.
    Akizungumza katika mahojiano maalum na BIN ZUBEIRY mjini hapa jana, kocha huyo kipenzi cha Waganda alisema anawategemea sana Okwi na Kiiza kutwaa taji la pili mfululizo la Tusker Challenge katika fainali za nyumbani.
    Alisema wachezaji hao wamekuwa wakiimarika siku hadi siku na ndiyo maana ameendelea kuwa nao katika kikosi cha The Cranes tangu ameana nao miaka mitatu iliyopita.
    “Kila siku uwezo wao unazidi kupanda na nadhani wakati au bahati yao ya kucheza Ulaya haijafika tu, wote ni viwango vya kucheza Ulaya au nchi nyingine kubwa kuliko kwetu Afrika Mashariki,”alisema.
    Aliwasifu wana nidhamu na ni wazalendo- wana mapenzi na timu yao ya taifa. “Wanajituma sana nikiwa nao, wana nidhamu na wanapenda nchi yao, nawapenda sana, wananifurahisha,”alisema.
    Bobby alizipongeza pia klabu zao, Simba (Okwi) na Yanga (Kiiza) zote za Tanzania kwa kuwatunza na kuwalea vizuri wachezaji hao, ndiyo maana uwezo wao umekuwa ukipanda siku hadi siku.
    “Unajua mchezaji anatunzwa na klabu, kama klabu haikai vizuri na mchezaji hawezi kuwa katika kiwango kizuri, na kama hana kiwango kizuri siwezi kumchukua timu ya taifa. Kwa hivyo hata klabu zao nazishukuru kwa kunilelea vizuri hawa vijana,”alisema.
    Okwi na Kiiza jana waliiongoza Cranes kuilaza 1-0 Kenya katika mchezo wa ufunguzi wa Tusker Challenge uliopigwa kwenye Uwanja wa Mandela, uliopo Namboole, Kampala, Uganda.
    Shukrani kwake, mshambuliaji wa Saigon Xuan Thanh ya Vietnam, Geoffrey Kizito aliyefunga bao hilo pekee la ushindi dakika ya 74, akiunganisha krosi ya Iguma Dennis.
    Kwa ushindi huo, Korongo wa Kampala anafungana na Ethiopia kuongoza Kundi A, kwa pointi zake tatu kila timu. 
    Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na timu zote zilishambuliana kwa zamu.
    Kenya walianza kwa kasi kwa dakika tano wakicheza soka iliyowasisimua mashabiki wake wachache waliokuwapo uwanjani, lakini Uganda wakazinduka nao na kuanza kuwapa raha mashabiki wao kwa soka safi.
    Mchezo uliendelea kuwa hivyo kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu, kila upande wakicheza kwa kujiamini.
    Lakini sifa ziende kwa safu zote mbili za ulinzi kutokana na kucheza kwa umakini wa hali ya juu.
    Kipindi cha pili timu hizo ziliporejea uwanjani, zililazimika kusimama kwa takriban dakika saba baada ya taa za uwanjani kuzimika na baada ya mafundi kutatua tatizo hilo, ndipo kabumbu likaanza tena.  
    Michuno hiyo itaendelea kesho kwa mechi mbili, Burundi na Somalia saa 10:00 jioni na baadaye Tanzania Bara na Sudan saa 12:00 jioni.
    Katika mchezo huo, kikosi cha Uganda kilikuwa; Abel Dhaira/Hamza Muwonge, Iguma Dennis, Godfrey Walusimbi,Henry kalungi, Isaac isinde, Hassan Wasswa, Geoffrey Kizito, Moses Oloya, Emmanuel Okwi, Hamisi Kiiza na Brian Umony.
    Kenya; Duncan Ochieng, Anthony Kimani, Abdallah Juma, Jockins Atudo, David Owino, David Ochieng, Lama Salim Mohamed, Bernard Wanyama, Humphrey Mieno, Anthony ‘Muki’ Kimani/Enock Obiero na Clifton Miheso/Paul Were.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MZUNGU WA CRANES ASEMA KIIZA NA OKWI NDIO KILA KITU KAMPENI ZA UBINGWA TUSKER CHALLENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top