• HABARI MPYA

    Monday, November 26, 2012

    POULSEN BADO AWALILIA SAMATTA NA ULIMWENGU KAMPALA

    Kocha Kili Stars, Kim Poulsen

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    KOCHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen amesema kwamba bado anawahitaji mno washambuliaji Mbwana Ally Samatta na Thomas Emanuel Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na iwapo hawatajiunga kabisa na kikosi chake, watamuweka katika wakati mgumu.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini hapa, baada ya mchezo dhidi ya Sudan wa Kundi B Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge, ambao walishinda 2-0, Kim alisema jitihada za kuwaomba Mazembe wawaruhusu wachezaji hao zinaendelea.
    “Sijui itakuwaje wasipokuja, itanibidi tu niwatumie wachezaji hawa hawa waliopo, najua nina mshambuliaji mmoja, lakini nitawatumia hawa hawa waliopo, Simon Msuva anaweza akawa mshambuliaji, nitafanyeje,”.
    “Siwezi kuita mchezaji mwingine kutoka nyumbani kwa sasa, kwa sababu mtu lazima umuone uwezo wake, huwezi kumuita tu, kwa hivyo naomba Mungu tu Samatta na Ulimwengu waje,”alisema Kim.
    Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, jana ilianza vema kampeni zake za kuwania Kombe la Challenge, baada ya kuichapa mabao 2-0 Sudan kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, Uganda. 
    Ushindi huo, unaiweka Stars katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi B, nyuma ya Burundi inayoongoza kwa wastani wa mabao.
    Hadi mapumziko, Stars walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yote yakipachikwa kimiani na mshambuliaji wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyetumia vema krosi za Mrisho Khalfan Ngassa.
    Bocco alifunga bao la kwanza Bocco aliiwahi vema krosi ya Ngassa aliyewatoka mabeki wa Sudan wingi ya kushoto na kuitumbukiza kimiani dakika ya 14.
    Adebayor wa Chamazi aliwainua tena vitini mashabiki wa Tanzania dakika ya 28, akiunganisha krosi ya Ngassa tena kutoka kule kule kushoto. 
    Kwa ujumla Tanzania Bara walicheza vizuri kipindi cha kwanza, wakishambulia zaidi kupitia pembeni, kulia Simon Msuva ambaye hakuwa na madhara sana na kushoto Ngassa ambaye alikuwa mwiba mchungu haswa kwa Wasudan.
    Pamoja na Bara kutawala kipindi cha kwanza, lakini Wasudan walifanya mashambulizi kadhaa ya kushitukiza na sifa zimuendee mlinda mlango Juma Kaseja, ambaye alioko amichomo miwili ya hatari mno. 
    Kipindi cha pili Stars, inayofundishwa na Mdenmark Kim Poulsen iliendelea kutawala mchezo, lakini safu ya ulinzi ya Sudan iligangamala.
    Kikosi cha Stars jana kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Kevin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar/Amri Kiemba, John Bocco, Mwinyi Kazimoto na Simon Msuva/Shaaban Nditi.
    Sudan; Ebd Elrahman Ali, Moawia El Amin, Sami Abdallah, Faris Abdallah, Hamoda Bashir/Farid Mohamed, Mohamed El Mortada, Sadam Abutalib, Mohamed Mussa Idris, Modathir Mohamed, Adam Sayer/Osama El Rashid na Mohamed Osman/Saed Siddig.   
    Katika mchezo wa awali, Burundi walishinda mabao 5-1, mabao yake yakifungwa na Chris Nduwarugira dakika ya 35 na 88, Yussuf Ndikumana dakika ya 41 na Suleiman Ndikumana dakika ya 84 na 90, wakati la Somalia lilifungwa na Mohamed Jabril kwa penalti dakika ya 55.
    Matokeo hayo yanalifanya Kundi B lizidi kuwa gumu, kwani Burundi inaongoza kwa pointi zake tatu na mabao mengi, Tanzania ya pili kwa pointi tatu na mabao mawili- lakini bado Sudan wanaweza kupata matokeo mazuri katika mechi zijazo.

    MSIMAMO KUNDI B: 

                         P   W  D   L    GF GA GD Pts
    Burundi         1    1    0    0    5    1    4    3
    Tanzania       1    1    0    0    2    0    2    3
    Sudan           1    0    0    1    0    2    -2  0
    Somalia         1    0    0    1    1    5    -4  0
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: POULSEN BADO AWALILIA SAMATTA NA ULIMWENGU KAMPALA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top