• HABARI MPYA

    Tuesday, May 29, 2012

    TETESI ZA USAJILI BARA: NYOSSO, UHURU, JABU KUTUA YANGA



    Nyosso
    KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam inataka kuchukua wachezaji watatu kutoka Simba, ambao mikataba yao inaisha karibuni- hao ni mabeki Juma Jabu, Juma Nyosso na kiungo Uhuru Suleiman.
    Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani ya watu ambao wamepewa jukumu la kufanya usajili Yanga, zimesema kwamba wachezaji wote hao wamekwishafanya nao mazungumzo na wamefikia mwafaka, ingawa bado hawajasaini.
    “Fedha itatoa haraka, watasaini, kwa sababu tunatengeneza timu ya kucheza Kombe la Kagame,” kilisema chanzo chetu kutoka Yanga.
    Aidha, Yanga pia ipo kwenye mpango wa kusajili washambuliaji wawili ‘pacha’ wa timu ya taifa ya Rwanda, Meddie Kegere na Olivier Karekezi, ambao waling’ara sana kwenye Kombe la CECAFA Challenge mwaka jana Dar es Salaam, Amavubi ikifungwa na The Cranes kwenye fainali.
    “Mazungumzo na hao wachezaji wa Rwanda yalikwishafanyika siku nyingi na tumekuwa tukiwasiliana nao kwa kipindi chote hiki, mambo yanaendelea vizuri na watakuja hapa,”kilisema chanzo kutoka Yanga.
    Kiunganishi kuu cha wachezaji wa Rwanda na Yanga ni mfanyabiashara, Abdallah Ahmed Bin Kleb ambaye amewekeza nchini humo. Bin Kleb ndiye aliyemsajili kwa fedha yake, kiungo ‘baab kubwa’ wa APR, Haruna Niyonzima msimu uliopita.   
    Fungu la usajili wa wachezaji Yanga linatoka kwa mfadhili wa klabu hiyo, Yussuf Mehboob Manji ambaye ameteua Kamati Maalum kusimamia Usajili pamoja na ajira ya kocha mpya, atakayerithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic aliyetupiwa virago ‘kiaina’.
    Uhuru

    Jabu
    Baaada ya Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga kujiuzulu, klabu hiyo sasa ipo chini ya Baraza la Wadhamini na Sekretarieti ya klabu chini ya Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa.
    Yanga ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame na wamepania kutetea taji hilo, ili kupoza hasira za mashabiki wao baada ya msimu mbaya uliopita, wakipoteza ubingwa wa Ligi Kuu, sambamba na kukosa hata nafasi ya kucheza michuano ya Afrika, ikiwa ni pamoja na kufungwa 5-0 na wapinzani wao wa jadi, Simba katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TETESI ZA USAJILI BARA: NYOSSO, UHURU, JABU KUTUA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top