• HABARI MPYA

    Thursday, May 31, 2012

    DK TAMBA AOMBWA KUGOMBEA UENYEKITI YANGA


    Dk Tamba

    WANACHAMA wa klabu ya Yanga, wakiwemo wazee kadhaa wa Dar es Salaam wamemuomba, mwanachama mwenzao maarufu, Dk. Maneno Tamba kujitokeza kuwania nafasi ya Uenyekiti wa klabu hiyo katika uchaguzi wa klabu hiyo, uliopangwa kufanyika Julai 15, mwaka huu.
    Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka kwa mtu wa karibu wa Dk. Tamba, zimesema kwamba wanachama wa klabu hiyo, walifika mapema Jumatatu wiki hii ofisini kwa Dk. Tamba, Magomeni Mikumi, Dar es Salaam na kumuomba agombee, wakimpa moyo ana sifa na uwezo.
    “Walikuwa kama wanane hivi, kati yao watatu walikuwa wazee kabisa, walifika hapa. Wakaomba kumuona Dk Tamba, msaidizi wa Dk Tamba akaenda kumuambia. Dk akawaambia waingie, walipoingia sasa, nasikia yule msaidizi wake wakati anawapelekea kahawa, ndio akasikia hayo mazungumzo,”kilisema chanzo hicho.
    BIN ZUBEIRY iliwasiliana na Dk. Tamba juu ya habari hizo na uamuzi wake, lakini akasema ni mapema mno kwa sasa kuzungumzia chochote juu ya hilo, kwa sababu hakuwahi kufikiria suala hilo hata siku moja, hivyo inabidi naye alifanyie kazi kwanza.
    “Sheikh haya mambo mazito, wewe umepata habari hizi? Wewe naye hatari sana,” alisema Dk. Tamba na kuanguka kicheko kabla ya kuendelea; “Wamekuja wiki hii kweli, lakini inabidi nipate muda kwanza wa kulitafakari hili jambo na kuwasiliana na wadau wangu kushauriana nao, klabu kubwa ile kaka,”alisema.
    Kama kweli Dk Tamba ataamua kugombea Uenyekiti wa Yanga, anaweza akapita kutokana na sifa zake.
    Pamoja na kuucheza mpira wa miguu, kuwa na elimu nzuri, pia Dk. Tamba ni mtu anayeheshimika mno na watu mbalimbali nchini, wakiwemo viongozi wakubwa wa serikali, kutokana na shughuli za utabibu.
    Ni mwadilifu na muumini safi wa dini ya Kiislamu, ambaye anasali sala tano. Ana hekima, busara na anaijua soka kindakindaki- kwa sababu ni mpenzi haswa wa mchezo huo. Dk Tamba anamiliki timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Mburahati Queens, inayotoa wachezaji wengi timu ya taifa.
    Sifa za ziada za Dk Tamba ni mbunifu, kwani pamoja na shughuli zake za tiba za kijadi, ambazo humfanya aende kutoa huduma hadi nje ya nchi, pia ni mfanyabiashara na ni miongoni mwa watu wa awali kabisa nchini kutayarisha filamu ya Kitanzania na kuziingiza sokoni, ambazo zilifanya vizuri mno, kama Nsyuka na Soka la Bongo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DK TAMBA AOMBWA KUGOMBEA UENYEKITI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top