• HABARI MPYA

    Sunday, May 27, 2012

    MUSTAKABALI WA YANGA UTAZAMWE UPYA


    Mmoja wa waasisi wa Yanga, Mzee Mangara Tarbu (kulia) akipokea Kombe la ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1975 kutoka kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Tambwe Leya (kushoto), wote sasa marehemu. Wengine nyuma ni wachezaji wa klabu hiyo enzi hizo walioleta taji hilo, kwa kuifunga Simba Zanzibar. 

    HATIMAYE wiki hii, Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga ametangaza mwenyewe kujiuzulu wadhifa wake, baada ya vita kubwa aliyokuwa akipigwa na wapinzani wake.
    Nchunga anastahili sifa, ameonyesha yeye ni Yanga damu. Si mroho wa madaraka. Ni mtu aliyeweka maslahi ya Yanga mbele. Huyu ni mfano wa kuigwa. Lakini baada ya Nchunga kujiuzulu, pamoja na kwamba mfanyabiashara Yussuf Manji ameahidi kuihudumia timu kwa mwaka mmoja, bado ipo haja sasa ya mustakabali wa klabu hiyo kutazamwa kwa kina.
    Nasema mustakabali wa klabu kutazamwa kwa kina, kwa sababu imeonekana ni vigumu mno Katiba kumlinda kiongozi aliye madarakani, iwapo kundi fulani litaamua kwa dhati kuingia msituni kumng’oa.
    Mfano ni hii vita aliyopigwa Nchunga- ilikuwa kali na ikafikia lazima aondoke kwa maslahi ya klabu. Alitengenezewa zengwe zito. Alipigwa kila upande- hakuwa na namna yoyote zaidi ya kujinasua.
    Walioongoza mapambano dhidi ya Nchunga, akina Ibrahim Akilimali, Bakili Makele na wengine- ni wale wale ambao kwa zaidi ya miaka 10 wamekuwa mstari wa mbele katika vurugu na migogoro kwenye klabu hiyo.
    Kumbukumbu zipo, Bakili na Akilimali walishiriki kikamilifu kumng’oa Mzee Rashid Ngozoma Matunda mwaka 1999 na hawa hawa walimtia kashikashi nzito Wakili Imani Omar Madega, ingawa huyo walimshindwa.
    Sioni kwa sababu gani hawa watakoma kwa mtu mwingine yeyote atakayekuja baada ya Nchunga, kwa sababu wamekwishazoea. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kutoa mfano mmoja enzi za uhai wake kuhusu ubaguzi.
    Alisema dhambi ya ubaguzi ni sawa na dhambi ya kula nyama ya mtu, ukishakula nyuma ya mtu, hutaacha utaendelea kula.
    Naweza kuuleta mfano huu katika hii desturi ya mapinduzi kwenye klabu ya Yanga- naona kuna dalili za kutosha itaendelea tu hata ije katiba ya aina gani.
    Tena watu hawa wamepiga hatua kubwa, kiasi cha kuona bora Yanga ife, lakini kiongozi fulani ang’oke madarakani. Inasikitisha.
    Mapendekezo ya Manji kuhusu mabadiliko ya Katiba hata yafanyiwe kazi- lakini kuna uwezekano likaibuka kundi la kumpinga na kupambana naye kikamilifu. Hiyo ndio tabia ya Yanga.
    Kwa ‘uhuni’ aliofanyiwa Nchunga, hakuna hakika kama atatokea mtu mwingine mwenye hekima na kujiheshimu kufikiria kuongoza Yanga- inatia woga. Lakini kwa nini ifikie huko, kweli tutegemee kuiona Yanga bora na ya kisasa bila mtu mwenye hekima na upeo mkubwa?
    Kwa Nchunga, dalili niliziona tangu wakati wa uchaguzi uliomuweka madarakani mwaka 2010 kwamba hatakaa kwa raha Yanga na kwa wasomaji wa makala zangu tangu naandikia magazeti, watakuwa wanakumbuka nilisema sina uhakika hata kama atamaliza muda wake madarakani.
    Yametimia. Njia nzuri ya kuwateka wananchi ni kuwaridhisha tu na hiyo ndio demokrasia. Nchunga alitakiwa ashinde uchaguzi wa Yanga, bila kuwapo mizengwe na wale ambao hawakwenda ukumbini kwa ajili ya kumpigia kura, wakubali kwamba huyo ndiye chaguo la wana Yanga.
    Lakini kwa picha iliyojitokeza siku ile, hata yule ambaye alikwenda maalum kwa ajili ya kumpigia kura Nchunga, aliondoka na picha kwamba kiongozi huyo amepita kimizengwe. Hiyo peke yake ni mbaya sana.
    Sasa kosa hilo linataka kujirudia- staili iliyotumika kumng’oa Nchunga si nzuri na watu wengi hawajaridhika nayo, maana yake hakuna demokrasia pale. Hata huyo anayekuja baada yake, hakika hawezi kukaa kwa raha Yanga.
    Zaidi, aliyofanyiwa Nchunga yamewakera watu wengi tu na yeyote atakayekuja baada yake, ataonekana alikuwa nyuma ya mpango huo haramu. Watu hawawezi kusahau, kwamba ili kumuondoa Nchunga madarakani, ilibidi Yanga ifungwe 5-0 na Simba. Matusi makubwa hayo kwa wana Yanga.
    Dhambi hii peke yake, itamuhukumu yeyote atakaytekuja baada ya Nchunga. Lakini hata Nchunga naye hajajiuzulu kwa kupenda, amelazimika kutokana na hekima na busara yake kumtuma kufanya hivyo, ili kuinusuru klabu.
    Marehemu baba yangu alikuwa Yanga mzuri sana, na alifariki mwaka 2001 akiwa ana umri wa 98. Nakumbuka aliwahi kuniambia; “Tangu ule mgogoro uliomkimbiza Mzee Mangara, klabu yetu haijawahi kutulia na sijui kama haya yataisha,”.
    Wakati huo anasema hivyo ilikuwa kipindi ambacho kuna mgogoro wa kumuondoa madarakani Matunda. Marehemu baba yangu alikuwa Yanga yule, ambaye starehe yake kufungwa Simba tu, hata timu ifungwe ligi nzima, lakini yeye anataka mnyama auwawe tu.
    Nakumbuka miaka ya 1990, wanachama fulani walikwenda kumuangukia mzee Mangara na wakamrejesha Jangwani, lakini umri ulikuwa umekwishaenda sana. Hata alipofariki dunia, alizikwa vizuri na wana Yanga.
    Lakini bado kuna maneno ya pembeni pembeni yanazungumzwa kwamba Yanga ina laana ya waasisi wake, akina Mangara. Najua hapa kuna baadhi hawatanielewa, acha nizame ndani kidogo;
    Mwaka 1975, Yanga ilitwaa kwa mara ya kwanza ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame, ikiifunga Simba kwenye fainali mabao 2-0 visiwani Zanzibar. Wafungaji wa mabao hayo walikuwa wale wale wauaji wa fainali ya Klabu Bingwa ya Taifa mwaka 1974, Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza, Sunday Manara na Gibson Sembuli (marehemu), katika ushindi wa 2-1, bao la Simba likifungwa na Adamu Sabu (sasa marehemu).
    Lakini kwa sababu wachezaji wengi waliitumikia Yanga tangu miaka ya 1960, Mangara akawasilisha mchakato wa mapinduzi katika timu, akiamini wachezaji walipo wamezeeka, ila hakueleweka kwa sababu timu ilikuwa ina matokeo mazuri.
    Kipindi hicho wakongwe wa Yanga walikuwa akina Elias Michael 'Nyoka Mweusi', Muhidini Fadhili na Patrick Nyaga, wote makipa, mabeki Boy Iddi Wickens, Athumani Kilambo 'Baba Watoto', Badi Saleh, Hassan Gobbos, Omar Kapera, viungo Abdurahman Juma, Abdurahman Lukongo, Sunday Manara 'Computer', Leonard Chitete, na washambuliaji Gibson Sembuli, Kitwana Manara 'Popat' na Maulid Dilunga. 
    Wakati huo huo, kulikuwa kuna kundi la vijana wanategenezwa pale Yanga, akina Juma Pondamali, Mohamed Rishard ‘Adolph’, Mohamed Yahya ‘Tostao’, Leodegar Chilla Tenga, Jellah Mtagwa, Juma Matokeo, Kassim Manara na wengineo, maarufu kama Watoto wa Dk Victor Stanslescu, ambao ilikuwa ndio warithi mikoba ya wakongwe.  
    Lakini pamoja na ubishi huo, baada ya kushindwa kutetea Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki mjini Mombasa, Kenya, uliibuka mgogoro mkubwa na wa kihistoria ndani ya klabu hiyo.
    Yanga ilianza vizuri tu katika kundi lake B, ikiifunga 2-1 Mseto SC ya Morogoro, kabla ya kuitandika Green Bufalloes ya Zambia 2-0, Bata Bullets ya Malawi 3-1, iliongoza kundi hilo, ikifuatiwa na Mseto, mabingwa wa Tanzania mwaka 1975.
    Katika Nusu Fainali, Yanga iliifunga 3-0 Express ya Uganda wakati Mseto iliona cha mtema kuni kwa Luo, baada ya kutandikwa 5-0. Yanga iliuacha ubingwa Mombasa, baada ya kulala 2-1 kwa Luo kwenye fainali.
    Timu iliporejea nyumbani, mgogoro ukaibuka, wanachama walikuja juu na kutaka kumpiga Mwenyekiti wao wakati huo, mzee Mangara, ambaye aliokolewa kwa kutoroshewa mlango wa nyuma.
    Vyanzo vinasema kwamba, wanachama walifika na bakora Jangwani wakitaka kumchapa Mangara. Walikuwa wanataka hesabu za mapato na matumizi ya klabu, lakini walikuwa wenye ghadhabu wakifanya fujo, hivyo ili kuepuka balaa hilo, Mangara alitoroshwa na kuwaacha solemba waliokuwa wanamsubiri nje wamchape bakora. Mgogoro wa Yanga Kandambili na Yanga Raizoni uliitafuna Yanga kwa miaka minne.
    Kipindi hicho Yanga ilikuwa safi kiuchumi, ilikuwa ina mabasi matano yaliyokuwa yakiingizia fedha klabu, Uwanja wa Kaunda uliojengwa kwa mkopo wa Sh 500,000 wa Benki ya Nyumba (THB) ulikuwa bado mpya unavutia watu wengi wakati wa mazoezi ya timu hiyo.  Yanga ilisaidiwa pia fedha na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Abeid Karume kiasi cha Sh milioni 2.7 kwa ajili ya ujenzi.
    Aidha, Yanga ilikuwa ina mfadhili wake, aliyekuwa akiwasaidia fedha nyingi, Shiraz Sharrif, ingawa naye baada ya mgogoro alihamia Pan African, kwa sababu alikuwa ana imani na Mangara.
    Kutokana na jinsi Mangara alivyoishi vizuri na wachezaji wa klabu hiyo, alikuwa akiwapenda akiwafanya marafiki, basi wachezaji wote waliamua kumfuata na kuachana na Yanga. Walifikia hatua hiyo, baada ya jitihada za kushinikiza Mangara arejeshwe, ikiwemo kuandamana, kushindikana. Kwa jeuri, Yanga nayo ilisema acha waende na itaunda timu mpya.
    Hadi leo, ukiwauliza watu wa Yanga sababu za kugombana na mzee Mangara, wapo watakaosema wanachama walikuwa wakorofi na wengine watasema mzee huyo alikuwa akinufaika kwa kupitia mgongo wa Yanga.
    Katika sakata hilo, wachezaji wakongwe waliokuwa Yanga ili wasikae bure msimu wa 1976, walikwenda Morogoro kujiunga na klabu iliyokuwa ikiitwa Nyota Afrika, wakafanikiwa kuipandisha daraja, wakati wachezaji chipukizi awali walikwenda kujiunga na timu ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), iliyokuwa ikiitwa Breweries wakati huo.
    Lakini baadaye wachezaji waliokwenda Nyota walirejea Dar es Salaam kuungana na wadogo zao, kuanzisha timu iliyokuja kuwa tishio kwenye soka ya Tanzania, Pan African. Timu hiyo ilianzishwa chini ya Mangara, aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza klabu hiyo.
    Mbali na Mangara, wengine walioasisi timu hiyo ni Omar Muhajji, Sammy Mdee, Shiraz Sharrif, aliyekuwa mfadhili wa Yanga ambaye alihamishia noti zake kwa klabu ya Mtaa wa Swahili.
    Kihistoria huo ulikuwa mgogoro wa kwanza Yanga na tangu wakati huo migogoro imekuwa sehemu ya maisha ya klabu hiyo. Sitaki kuamini kama wanavyoamini wengine, kwamba Yanga ina laana ya waasisi wake. Bali nachoamini, ipo haja ya kuuangalia upya mustakabali wa klabu, ikiwa hata Katiba mpya madhubuti, zilizotayarishwa kutokana na ushauri wa FIFA, haziwezi kuheshimiwa Yanga na watu wapo tayari klabu ife.
    Nilimsikia Mzee Akilimali anasema Yanga itahamia Zanzibar. Kama hajui, hata Zanzibar ipo chini ya FIFA, haina uanachama kwa sababu ni sehemu ya Tanzania- ila kwa kuwa wanachama wa CAF, lazima wafuate mwongozo wa wenye soka yao, FIFA.
    Kwa hiyo asikate kuwadanganya watu kwamba, atakaidi agizo la FIFA kupitia TFF- halafu akawe mwanachama wa ZFA. Hakuna kitu kama hicho.  Wadau, TFF na serikali- umefika wakati sasa mustakabali wa klabu hii utazamwe upya.
    Nasema hivyo kwa makusudi, kwa sababu kuna harakati zinaendelea pale- iwapo watu watatulia na kuacha ziendelee, nahofia zinaweza kufuta historia ya klabu na jengo la klabu pale Jangwani, likabaki kijiwe cha kuchezea dhumna, drafti na kupiga majungu. Wasalaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MUSTAKABALI WA YANGA UTAZAMWE UPYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top