• HABARI MPYA

    Tuesday, May 29, 2012

    SHAABAN NDITI ATUA COASTAL UNION, TIMU YAENDA ZIARANI UTURUKI


    MABINGWA wa Ligi Kuu ya Bara mwaka 1988, Coastal Union ya Tanga wanatarajiwa kufanya ziara ya kujiandaa na msimu mpya nchini Uturuki, Julai mwaka huu, huku habari zaidi zikisema wamemsajili kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Shaaban Mussa Nditi (pichani kushoto) aliyewahi kuwika Simba SC.
    Msemaji wa Coastal Union, maarufu kama Wagosi wa Kaya, Edward ‘Edo’ Kumwembe ameiambia BIN ZUBEIRY jioni ya leo kwamba wapo kwenye mchakato wa ziara hiyo na utakapokamilika watatoa ratiba kamili.
    Ingawa Edo, ambaye pia ni Mwandishi wa Habari na Mchambuzi wa soka katika gazeti la Mwanaspoti, hakusema ziara hiyo imefadhiliwa na nani, lakini habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake Barabara ya 13, Tanga zimesema ni mchezaji wao wa zamani, Kassa Mussa.
    Kiungo huyo hodari wa zamani wa Mkoa wa Tanga, aliyekuwemo kwenye kikosi kilichochukua ubingwa wa Bara 1988, kwa sasa anaishi Uturuki ambako inaelezwa amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kimaisha.
    Tayari Coastal imekwishaanza mchakato wa kuunda kikosi ‘baab kubwa’ cha msimu ujao na habari zaidi zinasema wako mbioni kumsajili kiungo wa zamani wa Simba, Mkenya Jerry Santo wakati wachezaji wengine ambao viwango vyao vimeshuka kama Ben Mwalala, Mkenya pia na Ramadhan Wasso, Mrundi, wamekwishaonyeshwa mlango wa kutokea.
    Coastal inatarajiwa kutengeneza ‘bonge la mshituko’ kwa wapenzi wa soka nchini katika usajili wao, kutokana na harakati zao za chini chini za usajili wanazofanya, ikiwemo kumsajili kiungo wa Mtibwa Sugar, Shaaban Mussa Nditi.
    Wengine ambao tayari wamenasa kwenye rada za Coastal ni mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Nsa Job Mahenya ambaye msimu huu alichezea Villa Squad iliyoshuka daraja.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SHAABAN NDITI ATUA COASTAL UNION, TIMU YAENDA ZIARANI UTURUKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top