• HABARI MPYA

    Wednesday, May 23, 2012

    NCHUNGA AJIUZULU KUINUSURU YANGA


    TANGU aondoke Mangara Tabru (sasa merehemu) katika klabu ya Yanga 1976, hapana shaka Imani Mahugila Madega ndiye Mwenyekiti pekee aliyefanikiwa kukaa madarakani hadi kumaliza muda wake, akiitisha uchaguzi na kumkabidhi madaraka kiongozi mwingine, Wakili mwenzake, Lloyd Baharagu Nchunga (pichani kushoto), Mei 18, 2010.
    Kuna dalili za kutosha kabisa, Nchunga ameshindwa kuvunja rekodi ya Madega na kwa hali ilivyo wakati wowote anaweza kutangaza mwenyewe kujiuzulu, kwa nia nzuri tu ya kuinusuru Yanga.
    Wanachama wanaodai idadi yao ilifika 700 wa Yanga walikutana Jumapili makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na kufikia uamuzi wa kumng’oa madarakani Mwenyekiti, Wakili Lloyd Bahargu Nchunga.
    Mapinduzi haya yaliongozwa na Mzee Ibrahim Akilimali, ambaye kihistoria nilishasema siku nyingi ni mzee kinara wa migogoro na mvuruga amani klabuni, aliyetukuka.
    Huyu alishiriki mapinduzi ya kumng’oa marehemu Rashid Ngozoma Matunda na akashiriki kumnyima amani Madega katika utawala wake, ingawa alichemsha. Mzee huyu alijaribu kugombea Uenyekiti wa Yanga dhidi ya Dk Jabir Idrisa Katundu mwaka 1993, lakini akajitoa mapema kwa sababu alikuwa hakubaliki.
    Kweli, kwa sasa Nchunga ameshindwa kumudu kuongoza Yanga kwa ufanisi, na hiyo ni kwa sababu ya kukosa ushirikiano kutoka kwa Wajumbe wenzake wa Kamati ya Utendaji na wadau wengine wa klabu, wakiwemo hao wanaojiita wazee na wafadhili.
    Lakini ukirejea uchaguzi uliomuweka madarakani Nchunga Jumapili ya Mei 18, mwaka 2010, alishinda Uenyekiti baada ya kupata kura 1,437,  akiwaangusha wapinzani wake wanne, Francis Kifukwe aliyepata kura 370, Mbaraka Igangula aliyepata kura 305, Abeid Falcon aliyepata kura 301 na Edgar Chibura aliyeambulia kura 65 katika kura 2,220 zilizopigwa, wakati kura 23 kati ya hizo ziliharibika.
    Kura 370 za Kifukwe na 305 za Igangula kwa pamoja wakichanganya, bado hawawezi kufikia kura za Nchunga- ina maana alishinda kwa kishindo. Inakuwa rahisi kuhisi watu hawa 700 waliokutana Jumapili ni wale wale 700 waliomnyima kura Nchunga PTA Mei 18, 2010.
    Lakini kwa sababu hiki ni kipindi kigumu ambacho Yanga inatakiwa kujipanga upya baada ya msimu mbovu uliopita, tena uliotokana na Nchunga kuhujumiwa na wapinzani wake, hakuna njia nzuri zaidi ya Wakili huyo kuchukua maamuzi magumu kwa maslahi ya klabu. Wala Nchunga hataonekana mjinga- bali ataonekana jasiri na mwenye mapenzi ya kweli kwa klabu.
    Alifanya kosa kubwa kuteua waliokuwa wapinzani wake kwenye uchaguzi katika Kamati zake- hao ndio waliomuumiza. Alifanya kosa kushindwa kuwa bega kwa bega na waliomsimika madarakani wamsaidie. Sasa anavuna matunda ya makosa yake. Aliwaamini sana watu wa Yanga, hakuwajua vizuri. Wengi wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi na ni wanafiki sana.
    Inapofikia hapa, namkumbuka marehemu Syllersaid Salmin Kahema Mziray; aliwahi kusema Simba na Yanga zikifa na watu wengi watakufa kwa sababu maisha yao yote wanazitegemea hizo klabu- kwa Jangwani ndio hao Al Shabaab. Riziki yao inatokana na migogoro.
    Kama nitapata fursa ya kukutana na Nchunga, nitamuambia ajiuzulu Yanga. Atakuwa amechukua uamuzi wa kijasiri na busara na ataheshimika daima milele. Sasa waingie hao Al Shabaab na walipe kisasi cha 5-0 za Simba. Tena wapewe miaka minne.
    Siku zote nasema migogoro hii ya Simba na Yanga, serikali inaikumbatia, kwa sababu ukizama ndani ya historia ya timu hizi ni kama mali za umma tu hazina mwenyewe. Hivyo kila mwenye kadi anajifanya ana sauti na maamuzi, bila kuzingatia ana mchango gani.
    Kwa misingi ya klabu hizi, ni vigumu kufa, ila migogoro haitaisha, hasa Yanga- kwa sababu kuna kigogo pale ana azma yake na inaweza kuwa nzuri, lakini njia anazotumia kutaka kuitimiza ndio shubiri kwa klabu hiyo.
    Ni yule Yule aliyemnyima raha Madega katika utawala wake- sasa amepiga hatua kubwa. Kujaribu kupambana na migogoro ya Yanga kwa kupambana na akina Akilimali na Bakili Makele ni kazi bure- lazima litafutwe shina la matatizo klabuni- hawa ni matawi tu.
    Sitaki kuamini eti pale alipo Leonard Thadeo, Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo au Leodegar Tenga, Mwenyekiti wa TFF hawajui kiini cha mgogoro huu wa Yanga- kama hawajui wakiniita nitawaleleza na kuwapa vielelezo au ushahidi, labda wakijua wataisaidia klabu hiyo.
    Kuyumba kwa Yanga au Simba ni kuyumba kwa maendeleo ya soka ya nchi hii kwa ujumla pia- lakini pia Kilimanjaro Beer waliowekeza mamilioni yao pale Jangwani wanaupokeaje mgogoro huu?
    Tazama kwa sasa kikosi cha timu ya taifa kuna mchezaji mmoja tu wa Yanga, hivi kweli kama klabu hiyo ingekuwa vizuri, leo sura ya Taifa Stars ingekuwaje? Ni kiasi gani kwa sasa mchango wa Yanga unakosekana timu ya taifa? Huu ni mfano mdogo tu.
    Wanasema ni kidogo- japo mimi naona hakitoshelezi kulingana na bajeti yao wanachokipata kutoka TBL, lakini kisingekuwepo hali ingekuwaje Yanga?
    Kama hakuna msaada wa serikali, au TFF ina maana Nchunga atasababisha matatizo makubwa zaidi Yanga- tu kwa kutokubali kujiuzulu katika vita ambayo tayari amekwishashindwa.
    Madega alishinda vita hiyo kwa sababu kwanza alikuwa mzoefu wa siasa za Yanga na soka ya Tanzania kwa ujumla- akianzia kwenye ngazi za chini za uongozi mwaka 2000. Lakini Nchunga alikuwa mchanga katika siasa za soka za nchi na klabu hiyo kwa ujumla, nami nilijua hatafika mbali, hasa baada ya Davis Mosha kujiuzulu.
    Alikubali kuhitilafiana na Mosha na akaridhia ajiuzulu, lakini hakuona athari zinazoweza kutokea mbele yake. Kama angekuwa ana Makamu wake Mwenyekiti leo na wapo kitu kimoja, angalau leo kidogo angekuwa ana nguvu.
    Kile kimkutano cha nyuma ya jukwaa la Mkutano wa Uchaguzi na wagombea wenzake wa nafasi ya Mwenyekiti, leo ndio kinammaliza Nchunga. Alikubali ushauri ambao hakuufanyia kazi kwanza.  Ndio, wahenga walisema mchawi mpe mwanao, lakini si katika dunia ya leo, anamuua kweli na anakuambia macho makavu; “Kazi ya Mungu”. Utafanya nini?  
    Madega alisimama kidete kupigana, alisimamisha wachezaji waliotumiwa na adui zake kuisaliti Yanga- alipambana na wazee, wafadhili na wanachama bila woga wala kuwatazama usoni. Ndio maana aliwaaga wana Yanga, akipigiwa makofi Mei 18, 2010 pale PTA tena akisema; “Mtanikumbuka”. Kweli, mimi ni mmoja wa wanaomkumbuka leo.
    Madega hakuwa mnafiki, ukimkosea alikuwa anakuchana, na kesho mkikutana anakuwa wa kwanza kukusalimu. Ukikasirika shauri yako, ila yeye hakuwa wa kulea maradhi. Lakini naye aliwindwa kwa mikakati mizito ang’olewe, wakashindwa.   
    Unakumbuka alivyompa vidonge Manji? Nitakukumbusha;  
    “Habari hizo alizosema Manji juu ya uongozi wangu ni uongo mtupu, ukweli ni kwamba ujio wa Manji ndani ya Yanga unaonekana kama ni ukombozi wa kifedha, lakini ukweli ni kuwa amekuja kwa lengo moja tu, la kuiangamiza klabu ya Yanga kabisa na hatimaye kuunda kampuni ambayo kinadharia yeye ndio atakayekuwa mmiliki mkuu.” Kauli hii aliitoa Oktoba 11, mwaka 2007 baada ya kutokea kutoelewana kati yake na mfadhili wa klabu hiyo, Yussuf Manji.
    Bado, kuna nyingine pia alimpa Manji, ngoja niwakumbushe;
    “Kwa mawazo yangu, fedha hizo zilitolewa (na Manji) kwa lengo la kutugombanisha. Wachezaji wetu walicheza chini ya kiwango kwa kutambua kuwa wanavuja jasho, lakini fedha wanapewa wengine wasiowajibika uwanjani,”.
    Kauli hii aliitoa Oktoba 26, mwaka 2007 akijibu kauli ya Yussuf Mzimba, aliyeutaka uongozi wake kueleza jinsi ulivyotumia shilingi milioni 40 zilizotolewa na mfadhili wao, Yussuf Manji kwa ajili ya kuhakikisha timu hiyo inawafunga watani wao wa jadi, Simba Oktoba 24 mwaka huo mjini Morogoro. Manji pia aliwapa Sh. Milioni 10, wazee wa klabu hiyo chini ya Mzimba, lakini Yanga ililala 1-0, kwa bao pekee la Ulimboka Mwakingwe.
    Hata Yanga waliokuwa wanaamini Yanga bila Manji haiwezekani, aliwapa kitu pia;
    “Lakini pia ni vyema watu, hasa wanachama wa Yanga wakafahamu kwamba, mtoto huzaliwa na kukua, huwezi kutegemea kusaidiwa kila siku. Manji amefanya vitu vingi sana kwa klabu hii. Ametulea katika kipindi kigumu, wakati Uwanja wa Taifa ulipokuwa umefungwa, tulichezea Morogoro ambako fedha za kiingilio zilikuwa ni chache. Sasa tumehamia Dar es Salaam, timu inafanya vizuri mashindano ya ndani na nje, wanachama wanahamasika kuja kuishangilia na fedha zinapatikana. Tunaweza kusimama wenyewe,”.
    Kauli hii aliitoa Februari 3, mwaka huu akizungumzia mustakabali wa klabu hiyo
    Hata TBL nao pia aliwapa kitu, unakikumbuka? Nitakukumbusha;
    “TBL haina uwezo wa kuiingilia Yanga kwa kututaka tuajiri Katibu Mkuu, makubaliano yetu ni kuajiri Mweka Hazina na tunatarajia kutangaza nafasi ya kazi wakati wowote kuanzia sasa, atakayetimiza vigezo tutamuajiri. Haya mambo si ya kukurupuka, nafasi kama ya Katibu Mkuu ni nyeti ambayo mshahara wake hauwezi kuwa Sh200,000, hapa tutaongelea milioni kadhaa, sasa bila kujipanga tutawezaje kumlipa?”
    Kauli hii aliitoa Oktoba 3, mwaka 2008, kufuatia agizo la wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kuwataka waajiri watendaji kama ambavyo mkataba baina yao unaelekeza.
    Hata hawa wazee nao aliwapasha; nitakukumbusha;
    “Mwisho nasema kuwa sitokuwa tayari kuiona Yanga ikiuzwa na kutawaliwa na mtu mmoja kwa nguvu ya pesa, masikini na mwanawe, tajiri na mali zake, Manji baki na mali zako au heshimu Katiba. Vinginevyo baki na mali zako au fadhili timu nyingine. Wazee na wanachama wachache waroho wa Yanga kuweni macho na msiwasaliti wazee wenzenu ambao walifanya juhudi kuifanya Yanga iwe na jina kubwa, mkiendelea kufanya hivyo kwa hakika historia itawahukumu, uongozi uko imara kutetea maslahi ya Yanga,”.
    Kauli hii, Madega aliitoa Oktoba 11, mwaka 2007, kutokana na wazee na wanachama wa klabu hiyo kumuunga mkono Manji katika mgogoro wake na Madega.
    Kwa staili hii Madega alikaa Yanga hadi mwisho wa muda wake wa kuwa madarakani, lakini Nchunga ameonyesha hana ubavu huo- njia nzuri kwake ni kuachia ngazi, wengi wanajua ngoma imemkalia vibaya hii na zaidi akiendelea kuleta ubishi kwa kuwa analindwa na Katiba, atazidi kuiumiza timu.
    Sasa Yanga wanataka kusikia anasajiliwa mchezaji gani hodari wa kuunda kikosi imara cha kurejesha heshima msimu ujao, Nchunga bila msaada wa wafadhili ambao hivi sasa ndio wako dhidi yake, hataweza. Namshauri, aachie madaraka kuinusuru Yanga.


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NCHUNGA AJIUZULU KUINUSURU YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top