• HABARI MPYA

    Thursday, May 31, 2012

    KAMBI TIMU YA TAIFA ZANZIBAR MATATIZO MATUPU HADI MISOSI MIGOGORO


    Wachezaji mazoeini jioni ya leo, Uwanja wa Amaan jioni ya jana
    KAMBI ya timu ya taifa ya Zanzibar, inayojiandaa na michuano ya Kombe la dunia kwa nchi zisizo wanachama wa FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa), inakabiliwa na hali ngumu mno na zaidi inaendelea kwa sababu ya uzalendo wa wachezaji pekee.
    BIN ZUBEIRY  jana imetembelea kambi hiyo visiwani hapa na kufanya mahojiano na Kocha Mkuu, Ahmad Morocco, ambaye amesema kama si uzalendo wa wachezaji, basi safari ya Uzbekistan kwenye mashindano hayo yanayoanza Juni 4, mwaka huu ingekufa.
    Morocco amesema vijana wapo kambini Bwawani Hotel, lakini hata chakula ni cha matatizo. “Hawapati chakula cha kutosha, yaani wanapewa chakula kwa kiwango ambacho wamepanga wenye hoteli, si lishe ya kula mchezaji, lakini tutafanyeje na hiyo ndio hali halisi,”amesema Morocco.

    CHANZO CHA MATATIZO:
    Nikiwa kwenye mazungumzo na kocha Morocco
    Morocco anasema kwamba chanzo cha matatizo ni timu kutokuwa na mdhamini wala wafadhili na anasikitika japo Zanzibar kuna wafanyabiashara wakubwa na maarufu, lakini wote wamekaa kimya kipindi hiki na hawajitokezi kusaidia timu.
    “Wao wanasubiri matokeo mabaya waje kulaumu tu, lakini katika hali kama hii, ukifanya vizuri basi unastahili sifa sana, mimi nakuambia hata dawa tu hapa ni tatizo, timu haina dawa wala nini,”amesema.
    Morocco anasikitika kwamba hata wachezaji wa timu hiyo wapo kambini kwa zaidi ya siku 10, lakini hawapati posho na anaamini Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) hakina uwezo kwa sababu hakina wafadhili zaidi ya kutegemea serikali.
    “ZFA wanasema wamekwishapeleka bajeti yao Wizarani, lakini ajabu hadi sasa wanasema hawajajibiwa chochote, na hali inazidi kuwa mbaya kambini, maana yake wachezaji wanatumia chao cha mfukoni hadi wanaishiwa, sasa hata familia zao watazisaidiaje,”amesema.

    SMZ IMEISUSA TIMU?
    Selembe kushoto na Gulam kulia wakijiandaa kuingia mazoezini
    Lakini katika hali ya kustaajabisha zaidi, wachezaji wa timu hiyo wanastaajbu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekaa kimya kabisa na wala haijaonyesha dalili za kusaidia timu. “Sisi tunashangaa, kwa sababu matatizo yetu yanajulikana, lakini serikali imekaa kimya, yaani kila siku mazoezini ni kama unavyotuona, sisi na makocha wetu tu na daktari wetu. Hatumuoni hata kiongozi wa ZFA wala serikali, ila sisi tutakwenda kupigana na tutaleta Kikombe hapa wao washerehekee,”alisema Nadir Haroub ‘Cannavaro’, beki wa timu hiyo.  

    PAMOJA NA YOTE, VIJANA UZALENDO MBELE:
    Abdi Kassim kushoto na Abdulhalim Humud kulia wakipasha
    Pamoja na matatizo yote, kocha Morocco amesema wachezaji wana morali kutokana na hali yao ya uzalendo. “Wachezaji wako vizuri na wanaendelea vizuri na wako tayari kwa mashindano. Wameonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kweli.
    Morocco amesema timu itaondoka Juni 2, kupitia Dar es Salaam tayari kwa mchezo wa kwanza dhidi ya Tehran na anasema kwa ujumla wamepania kurejea na Kombe hilo. “Sisi kwa pamoja, azma yetu ni kurejea na Kombe, ili tuwadhihirishie wananchi wa Zanzibar uzalendo wetu,”amesema.

    SABRI, FAROUK WATEMWA SAFARINI, CANNAVARO CHUPUCHUPU
    Cannavaro na mkewa wakiwa jukwaani wanaangalia mazoezi
    Katika kikosi cha wachezaji 18 wanaoondoka na timu, wachezaji wawili tegemeo, kipa namba moja Farouk Ramadhan Mzee na kiungo Sabri Ramadhan ‘China’ wametemwa kutokana na kuchelewa kuwasilisha pasipoti zao kwa ajili ya kuombewa viza.
    Bado kikosini watakuwepo wachezaji wengine hodari tu wakiongozwa na nyota wa Azam FC, viungo Abdi Kassim ‘Babbi’, Abdulhalim Humud ‘Gaucho’, Suleiman Kassim ‘Selembe’, beki wa Yanga, Cannavaro, ambaye naye chupuchupu akose safari kutokana na majeruhi na mshambuliaji wa Canal Suez ya Misri, Ally Badru.
    Cannavaro ameshindwa kufanya mazoezi leo kutokana na kufanyiwa upasuaji mdogo wa jipu kwenye goti, lakini daktari wa timu amethibitisha anaendelea vizuri na kesho ataaanza tena mazoezi.
    Katika kikosi hicho atakosekana pia beki Aggrey Morris Ambroce, ambaye yuko kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinachokwenda kucheza na Ivory Coast mwishoni mwa wiki, kikiondoka alfajiri ya kesho Dar es Salaam.
    Morocco amesema pengo la Morris limezibwa vema na beki Salum Tall anayecheza soka ya kulipwa Oman, ambaye alicheza soka nzuri mno katika mechi ya kujipima nguvu na Malawi jana iliyoisha kwa sare ya 1-1. Malawi pia ilicheza na Taifa Stars Jumamosi wakatoka 0-0.
         
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMBI TIMU YA TAIFA ZANZIBAR MATATIZO MATUPU HADI MISOSI MIGOGORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top