• HABARI MPYA

    Saturday, March 07, 2009

    KONDIC: CHUJI NI LULU YANGA




    KOCHA Mkuu wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Profesa Dusan Kondic (KULIA) amesema kwamba atamtumia kiungo Athuman Iddi ‘Chuji’ (KUSHOTO) ipasavyo katika mchezo dhidi ya Al Ahly ya Misri, kwa sababu mchezaji mwenye mchango mkubwa katika timu yake.
    Kondic alisema hayo jana kambini kwao katika Hotel ya Tamal iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam kuwa Chuji licha ya kuwa katika mgogoro na kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo juu ya madai kuwa mchezaji huyo hana nidhamu yeye amesema atasafiri naye kwenda Cairo, Misri.
    Alisema kiungo huyo ni mchezaji wa kawaida tu hivyo hawezi kumwacha kisa ugomvi na Maximo bali ataondoka naye kwani kucheza ugenini haifai kuacha mchezaji muhimu kama huyo.
    “Siwezi kujua ugomvi wao ulianzia wapi ila ninakabiliwa na mchezo mgumu siwezi kumwacha labda litokee lingine awe majeruhi au kuugua na si lingine. Hii ni klabu yake ambayo imemsajili ili aitumikie hivyo atakuwa na wenzake na hivi sasa yupo kambini,”alisema.
    Aliongeza kwamba Al Ahly ni mabingwa hivyo wanaenda kupigana kufa na kupona na tayari amenasa baadhi ya kanda za video zao za michezo mbalimbali waliyocheza hivyo wataweza kuitumia kwa ajili ya kuangalia wachezaji na mfumo wa uchezaji wa timu hiyo.
    “Kuna wachezaji wengi wazuri ambao tumewaona lakini nina imani video zao tulizozipata zitatusaidia,” alisema.
    Chuji na mwenzake Haruna Moshi 'Boban' wa Simba, walitofautiana na Maximo wakati Stars ilipokuwa Ivory Coast, kwenye Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN).
    Wakati Stars ikirejea nchini Chuji na Boban walikuwa kituko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kutokana na kujitenga na wenzao na kuwakimbia Waandishi wa Habari.
    Wachezaji hao walionekana kuwakwepa wanahabari mara baada ya kuwasili uwanjani hapo, ikiwa ni pamoja na kutokea mlango tofauti na wenzao ambao walitokea kwenye lango la wageni maalumu (VIP), wakati wachezaji hao walipita katika mlango wa kutokea wa wageni wa kawaida wanaowasili.
    Waandishi wa habari walipogundua hilo na kuwafuata kutaka kuzungumza nao, wachezaji hao waligoma kuzungumza sababu za kutokuwa pamoja na wenzao, huku kila mmoja akionyesha kutokuwa tayari kuzungumza zaidi juu ya suala hilo na kwenda moja kwa moja kwenye gari aina ya Toyota Hiace iliyokuwa kwenye maegesho ya magari ya uwanja huo na kuingia. Baada ya kuingia kwenye gari hilo, wanahabari waliokuwa na uchu wa kujua nini kinaendelea kutokana na hali hiyo ya kuwakimbia na kutopanda gari la timu pamoja na wenzao, waliwafuata wachezaji hao kwenye gari lenye vioo vya giza (tinted) , ndipo Iddi alipofungua mlango na kusema asingekuwa tayari kusema lolote kwa leo. “Eeh bwana hapa hazungumzi mtu kitu, kama mnataka tuzungumze subirini hadi kesho (leo), ndipo tutazungumza,” alisema na kufunga mlango wa gari hilo. Licha ya Chuji na Haruna, wengine ambao hawakupita mlango wa VIP ni Kelvin Yondani, lakini mchezaji huyo alirudi kuungana na wenzake.
    Wakati hayo yakiendelea, wachezaji wengi wa Stars walikuwa wakipiga picha za pamoja na viongozi waliokuwa kwenye msafara pamoja na Bendera aliyefika kuwapokea na baadaye viongozi hao pamoja na kocha kuzungumza na wanahabari.
    Stars iliaga kwenye michuano hiyo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Zambia na kushindwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya CHAN kutoka Kundi A, ambalo lilikuwa na timu za Zambia na Senegal zilifuzu kwa hatua hiyo zikiwa na pointi tano, Stars ilikuwa na pointi nne ikishika nafasi ya tatu, huku Ivory Coast ikishika nafasi ya mwisho ikiwa na pointi moja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KONDIC: CHUJI NI LULU YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top