• HABARI MPYA

    Monday, March 16, 2009

    SIMBA UWANJANI NA MORO UNITED LEO


    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea leo wakati Wekundu wa Msimbazi, Simba SC watakaposhuka dimbani, Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam kumenyana na Moro United.
    Simba, ambayo Alhamisi iliyopita kukubali kipigo cha mabao 2 - 1 kutoka kwa timu ya Vancouver Whitecaps ya Canada katika mchezo wa kirafiki, leo imepania kushinda.

    Kocha wa Simba, inayotarajiwa kuongozwa na mshambuliaji wake, Mussa Mgosi (pichani kushoto) Mzambia Patric Phiri amesema kufungwa na Vancouver hakumtii presha katika mchezo wa leo.
    Phiri alisema kufungwa katika mchezo huo ni sehemu ya mchezo na hakuna wa kulaumiwa anachoangali ni kushinda mchezo wa leo hivyo kuwataka mashabiki kufika uwanjani na kuishangilia timu yao.
    "Tuachane na mechi ya kirafiki hayo yamepita, hivi sasa tunaangalia ligi ni jinsi gani tutaweza kuipata nafasi ya pili ambayo tunaisaka kwa kasi kubwa.
    "Kuna makosa kadhaa yalifanyika katika mchezo wa kirafiki, lakini yote nimefuta na nimeyafanyia kazi na nina uhakika leo wa ushindi kwani timu ipo vizuri sana," alisema
    Alisema ushindi katika mchezo wa leo utampa matumaini ya kuendelea kushinda michezo sita iliyobaki na kutwaa nafasi ya pili baada ya ubingwa kutua Yanga.
    "Tukishinda leo tutakuwa tumefungua njia ya ushindi kwa kila mechi, nafahamu Moro ni wazuri na wako katika hali ushindani kuifanya mechi yetu kuwa ngumu, lakini sisi tutaingia uwanjani tukisaka ushindi tu," alisema Phirri.
    Naye kocha wa Moro United, Fred Felix Minziro alisema mchezo wa leo utakuwa mgumu sana lakini wao wanahitaji ushindi kwa hali yoyote ile ili kukwepa panga la kushuka daraja.
    Moro United iko katika nafasi ya tatu kutoka chini kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 15 hivyo inabidi ifanye kazi kubwa kuhakikisha inashinda mechi zake zote zilizobaki ili ibaki Ligi Kuu msimu ujao.
    Minziro alisema timu yake iko katika hali mbaya sana na wanaomba Mungu awaokoe na kubwa wanalotaka ni kushinda mchezo wa leo.
    "Tunaamini kabisa tukishinda mchezo wa leo tutashinda na mingine yote, mechi ni ngumu sana tunaomba Mungu tu tushinde na tumalize mechi zetu zote zilizobaki vizuri ili tukwepe hili janga ka kushuka daraja," alisema Minziro.
    Ligi Kuu imerejea tena wiki hii baada ya kusimama kwa muda kupisha maandalizi ya timu ya Taifa iliyokuwa ikishiriki michuano ya CHAN nchini Ivory Coast.
    Katika mechi za mwishoni mwa wiki JKT Ruvu iliichapa Villa Squad mabao 5 - 0. Polisi Dodoma ilitoka suluhu na Kagera Sugar na Toto African kuibamiza Prisons magoli 2 - 1.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA UWANJANI NA MORO UNITED LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top