• HABARI MPYA

    Friday, March 20, 2009

    NSSF CUP: Michuano iliyopoteza dira, maana


    ILIKUWA mwaka 2004 katika michuano ya Kombe la Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), wakati nilipofanya kituko kilichowavunja mbavu wengi kati ya waliohudhuria kwenye Uwanja wa TCC, Chang’ombe mjini Dar es Salaam.
    Ilikuwaje? Timu yangu Habari Corporation (sasa New Habari) ilikuwa imetoka kufungwa bao, tukalazimika kuweka mpira katikati tuanze. Akili yangu ilikuwa kwenye kuanzisha shambuolizi la haraka, wakati wapinzani (Business Times) wakiwa bado kwenye furaha ya bao.
    Lakini sasa mwenzangu niliyekuwa naye kwenye eneo la kuanzisha mpira, alikuwa amezubaa, wakati mimi nimeugonga kwa mbele ili autokee tuanzishe shambulizi, yeye alizubaa na mimi nikaamua kuufuata na kuanza kuambaa nao.
    Lilikuwa ni kosa, kwa mujibu wa sheria nilitakiwa kumuanzia mtu, basi refa akapiga filimbi na kuamuru mpira uanzwe tena kwa mujibu wa utaratibu. Watu walivunjika mbavu sana, wengi waliokuwa wakinifahamu walinicheka sana.
    Achana na hilo, kulikuwa kuna vituko vingine vingi kwa wachezaji wengine waliokuwapo uwanjani. Yaani ni burudani kumuona mtu ambaye hayuko fiti, anacheza soka.
    Na watu walikuwa wanafika kwa wingi kwenye Uwanja wa TCC kushuhudia watu wanaowajua, Waandishi wa Habari na watangazaji wakicheza soka.
    Mimi naamini kabisa, NSSF ilikuwa na nia na dhamira nzuri tu kuanzisha mashindano haya, kubwa ikiwa ni kuwakutanisha pamoja Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari kucheza kwa furaha na kupata fursa ya kufahamiana zaidi.
    Lakini pia, michezo ni afya, anayeanza kucheza atapenda kucheza (mazoezi) mara kwa mara na hiyo ni njia mojawapo ya kutunza afya yake.
    Bila shaka, NSSF ilifanya hivyo kwa kujua kabisa mashindano haya yatakuwa na mvuto, yatakutanisha watu ambao miongoni mwao wapo maarufu na wengine na wenye mamlaka makubwa kwenye jamii yetu.
    Kama inavyofahamika, chombo cha habari ni mhimili wa nne wa dola, baada ya Serikali, Bunge na Mahakama, hivyo basi hii ni michuano ya kuheshimika mno mbele ya jamii.
    Kwa Waandishi wa habari, wachapakazi na weledi, lazima wanajijengea umaarufu na kama watu wengine maarufu hivyo basi nao wanakuwa na mashabiki wao.
    Binafsi, nashukuru nina mashabiki na wapenzi wa kazi zangu, kutokana na kile nilichowekeza katika miaka 13 ya kuwapo kwangu kwenye taaluma hii, nikiandika habari za michezo, sanaa na burudani.
    Kwa sababu mashabiki hao na watu wengine ambao unaweza kuwaita marafiki wanaposikia michuano kama hii wanavutia kwenda kuona ikiwa ni moja ua burudani kwao.
    Mtu anaamua kwenda ili kumuona Ibrahim Masoud, yule mtangazaji ambaye hujiita Midfield Mestro kwenye kipindi cha michezo cha Radio Clouds, ama Maulid Kitenge ‘Jezi Namba 9’ wa Radio One, Evans Mhando wa TBC, au Tom Chilala wa Star TV.
    Mtu anaamua kwenda kushuhudia NSSF Cup ili amuone Joel Beda, Edo Kumwembe wa New Habari, amuone Angetile Osiah wa Mwananchi, Amir Mhando wa TSN, Athanas Kazighe wa Uhuru, Gadna Habash wa Clouds FM, kwa sababu hao wote ndio wanaopaswa kuonekana kwenye michuano hiyo.
    Vivyo hivyo, kwenye mchezo wa mpira wa pete, dada zetu nao wana mashabiki wao na watu wanatamani kwenda kuwaona watu kama Jane John wa TCB, Grace Hoka wa New Habari, Dina Ismail wa Free Media, Dina Marius wa Clouds FM au Salma Jabir wa East Africa TV.
    Pamoja na kwamba hiyo ndio picha inayopaswa kuonekana kwenye michuano hii, lakini mambo yamekuwa tofauti siku hizi na sasa kwenye NSSF Cup hata Marcio Maximo akienda anaweza akapata vipaji vya kuingiza kwenye timu yake ya taifa.
    Au Anna Kibira akienda kwenye Netiboli anaweza kujua maendelezo ya wachezaji wake wa timu ya taifa wanaendeleaje.
    Kwa sasa kuita NSSF Cup ni michuano ya Waandishi wa Habari au vyombo vya Habari ni uongo uliobobea, kwa sababu inashirikisha watu ambao siyo wafanyakazi wa kwenye vyombo vya habari.
    Zipo baadhi ya timu zinashirikisha wachezaji ambao ni wafanyakazi wa kwenye vyombo vyao vya habari watupu, kuna nyingine zinachanganya, lakini nyingine ni aibu tupu, maana kuanzia moja hadi 11 ni Kinesi watupu.
    Juzi nilishuhudia mchezo wa Netiboli kati ya Uhuru na Clouds FM, ulikuwa mchezo mkali uliowashirikisha wacfhezaji maarufu wa Netiboli Tanzania, wakiwemo wa timu za majeshi.
    Timu zote zilikuwa zina wachezaji wasio wafanyakazi wa vyombo vyao vya habari, ingawa baada ya mchezo Uhuru wakiwa wamefungwa, walikata rufani.
    Kwenye soka kadhalika, hadi waamuzi wenyewe wa mashindano haya wanatuona sisi ni wa ajabu na wanatudharau mno.
    Kwa sababu inafikia wakati hata Mhariri Mtendaji wa kampuni anaweza akajikuta anashushwa thamani bila ya yeye kujua, kwani kuna mchezo mmoja unaofanyika, mtu siyo mtumishi wa chombo cha habari, lakini anatengenezewa kitambulisho kinachoonyesha anafanya kazi kampuni husika, ili tu acheze NSSF Cup.
    Kwa mtaji huu, waamuzi na wakaguzi wakishaona hivi, mtu ana kitambulisho, wafanye nini zaidi ya kumruhusu kucheza? Lakini ikumbukwe kwamba waamuzi hawa wanaochezesha NSSF Cup upande wa soka ndio hao hao wanaochezesha mechi za mchangani na wanawajua vizuri wachezaji.
    Mwamuzi mmoja aliniambia juzi, kwamba wanawafahamu vizuri sana wachezaji wengi wanaocheza mashindano haya, huwa wanawachezesha kwenye ligi za michangani. Vivyo kwenye Netiboli, hao waamuzi ni wale wale ambao CHANETA inawatumia kwenye michezo yake, hivyo nao wanawajua wachezaji.
    Kwa hivyo hata kama kuna kitambulisho chenye sahihi ya Meneja Mkuu wa kampuni, kwamba mchezaji husika anafanya kazi kwenye kampuni husika, lakini ukweli unajulikana na zaidi yule aliyedhamiria kuwafanya watu wajinga, anajikuta yeye mwenyewe ndio anaonekana mjinga.
    Ni jambo la ajabu mno kwenye michezo hii ya wanataaluma kuhusisha watu wasiohusika na ndio maana siku hizi NSSF wanapeleka askari polisi kusimamia usalama, kwa sababu hiyo michuano imepoteza hadhi ya kitaaluma.
    Hakika NSSF inapaswa kutazama upya dhamira yake ya kuanzisha michano hii na hali halisi ilivyo sasa, kwani michuano imepoteza dira na maana yake. Ni hayo tu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NSSF CUP: Michuano iliyopoteza dira, maana Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top