• HABARI MPYA

    Monday, March 30, 2009

    AL AHLY YAJIFARAGUA NA NYASI BANDIA ZA UHURU

    MABINGWA mara sita Afrika, Al Ahly ya Misri wamedai hawahofii kucheza kwenye Uwanja wa nyasi za bandia (Uhuru mjini Dar es Salaam) katika mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji Yanga JUmamosi wiki hii. Meneja Mkuu wa Ahly, Hossam Badri alikaririwa kwenye mtandao wa klabu hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita akisema hawana wasiwasi kucheza kwenye nyasi za bandia. “Al Ahly haitachanganywa na kucheza kwenye uwanja wa nyasi bandia kwa sababu siyo mara ya kwanza kwetu kucheza kwenye uwanja kama huo. Tulicheza na ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Dinamuzahrary na kupata matokeo mazuri,” alisema Badri ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Klabu hiyo. Wiki iliyopita Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilikubali ombi la Yanga mchezo huo kufanyika Uwanja wa Uhuru badala ya Uwanja wa Taifa kwa vile Yanga ndiyo uwanja iliouzoea. Awali TFF ilipanga mechi hiyo kufanyika Uwanja wa Taifa, lakini Yanga ilisisitiza kutaka Uwanja wa Uhuru wakiamini utawasaidia kufuta kipigo cha mabao 3-0 katika mechi ya kwanza iliyofanyika Cairo wiki mbili zilizopita. Yanga ilidai ina uzoefu zaidi kucheza Uwanja wa Uhuru ingawa watakabiliwa na upungufu wa mashabiki watakaoingia kutokana na uwanja huo kuingiza mashabiki wasiozidi 25,000 tofauti na Uwanja wa Taifa unaoingiza mashabiki 60,000. Yanga watahitaji kufunga mabao zaidi ya matatu kufuzu raundi inayofuata kwenye michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf). Wakati huohuo, jopo la viongozi wa Al Ahly litatua Dar es Salaam keshokutwa kufanya maandalizi ya ujio wa timu yao. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye mtandao wao viongozi hao wataongozwa na Khalid Aldrndly, lakini hawakuweka wazi siku ya kutua kwa timu hiyo. Katika hatua nyingine kocha wa Al Ahly, Manuel Jose ameonya wachezaji wake kuhakikisha wanashinda mechi yao dhidi ya Yanga. Kocha huyo anafahamu bado mchezo haujamalizika. Aliwaambia wachezaji wake mchezo huo hautakuwa rahisi. “Utakuwa mchezo mgumu kwetu kwa sababu tunacheza ugenini, tunahitaji kuweka mtazamo na kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AL AHLY YAJIFARAGUA NA NYASI BANDIA ZA UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top