• HABARI MPYA

    Monday, March 30, 2009

    TBL, LUNDENGA KUNANI TENA MISS TANZANIA?

    Meneja wa kinywaji cha Redd's, George Kavishe alipokuwa akimtambulisha balozi mpya wa kinywaji hicho, Angela Lubala (kulia), mwingine ni balozi wa kinywaji cha Redds aliyemaliza muda wake, Victoria Martin wa Tanga.

    MKURUGENZI wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), David Minja amesema kwamba wameamua kudhamini mashindano ya urembo kwa ngazi ya vitongoji pekee badala ya kufanya hivyo kwa shindano la Taifa, ili kuinua mashindano hayo kwa ngazi za chini.
    Minja alisema uamuzi huo ulifikiwa tangu mwaka jana na walikuwa hawajatangaza rasmi kwani muda wa kufanya hivyo ulikuwa bado.
    Ingawa hakusema sababu za kufikia maamuzi hayo mazito, habari za ndani zinasema kwamba kampuni hiyo imechukua uamuzi huo kutokana na kukiukwa baadhi ya vipengele katika mkataba wao na kamati ya Miss Tanzania.
    TBL ilichukizwa na kitendo cha Kamati ya Miss Tanzania kukubali kirahisi kitendo cha Balozi wa Redd's, Angela Lubala kuvua taji wakati hilo lipo kwenye mkataba baina yao na Kamati hiyo.
    Angela alichukua uamuzi huo kutokana na imani yake ya dini ya Kikristo, ambapo yeye anaabudu kanisa liitwalo World Alive International Outreach lililopo Sinza, mjni Dar es Salaam, hivyo hawezi kuwa mwakilishi wa pombe.
    “Nachukua fursa hii kuiambia jamii kuwa kutokana na imani yangu katika Yesu Kristo, sitaweza kuwakilisha Redd’s kama Redd’s Fashion Ambassador 2008. “Kwa kuwa mimi si mbinafsi, narudisha taji hili na zawadi zake zote kwa Redd’s, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Vodacom, Lino na Redd’s kwa uelewa juu ya uamuzi wangu huu”, alisema wakati akivua taji hilo.
    Vodacom ndio wadhamini wakuu wa Miss Tanzania. Angela ambaye pia ni Miss Temeke 2008, alisema zawadi anayorudisha ni fedha sh. Milioni 2.5.
    Alipoulizwa kama hakujua wakati anashiriki mashindano hayo tangu mwanzo kama kuna jambo kama hilo, alisisitiza kuwa suala la kuwa Balozi wa kinywaji hicho haliendani na imani yake.
    Mkurugenzi wa Lino International Agency inayoandaa mashindano Miss Tanzania, Hashim Lundenga akiizungumzia hatua hiyo ya TBL alisema ni sawa ana kuleta mtafuruku baina yao na wadhamini wakuu, kampuni ya Vodacom Tanzania.
    Kamati ya Miss Tanzania imesema hatua hiyo ni sawa na kuwaletea vurugu katika mashindano yao kwa kuwa wao kwa sasa wapo katika hatua ya mwisho mwisho kumtangaza mdhamini huyo, hatua ambayo itawakwamisha kampuni ya TBL kudhamini hata kitongoji.
    "Tumesaini mkataba na wadhamini wa mikoa na kanda ambayo inawakataza kuingia mkataba na mdhamini wa kampuni ya bia tofauti na wadhamini wao wasaidizi endapo watampata na kumtangaza, vipengele vipo wazi na hata TBL wanavijua," alisema Lundenga.
    Alisema kuwa wakala ambaye ataruhusiwa kudhaminiwa na kampuni pinzani ya bia ni yule atakayefanya mashindano yake kabla ya wao kumtangaza mdhamini msaidizi na hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha tatu (III) cha mkataba baina ya mawakala na kamati yao.
    "Mdhamini msaidizi wa wine atakayetangazwa atapewa haki pekee ya kudhamini mashindano hayo katika ngazi zote, nadhani ndivyo ilivyokuwa kwa TBL, tulitekeleza mkataba wetu na wadhamini hao na hata kufikia hatua ya kumtoa masindano mshiriki wa wilaya ya Kishapo kutokana na mashindano hayo kudhaminiwa na kampuni ya bia (tofauti) na TBL," alisema.
    Alisema kuwa hata waandaaji wa vitongoji wa Dar es Salaam bado hawajasaini mkataba na kamati yao na watafanya hivyo wakati wa semina elekezi na huo ndiyo utaratibu wao wa kila mwaka.
    "Hizi ni vurugu ambazo zinalenga kuleta mtafaruku katika mashindano yetu, kamwe hatutakubali kwani kuna sheria ambazo zipo kwa mujibu wa mkataba, tumeamua kuweka wazi suala hili kutokana na hali halisi, bora wajue mapema sheria hizi," alisema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TBL, LUNDENGA KUNANI TENA MISS TANZANIA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top