• HABARI MPYA

    Friday, March 20, 2009

    KONDIC: KWA NJAA GANI NIIHUJUMU YANGA?

    KOCHA Mkuu wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Profesa Dusan Kondic amesema anasikitishwa na habari zinazozushwa kwamba yeye aliwauzia mechi wapinzani Al Ahly mjini Cairo, Jumapili iliyopita kwani huo ni uongo na yeye hana njaa ya kufanya hivyo.
    “Inanibidi nicheke tu rafiki yangu, wewe ni rafiki yangu, tutazungumza, mimi? Mimi nimeuza mechi! Sina njaa ya kufanya kitu kama hicho, nitakuambia, kaa hapa”alisema Kondic na kumwambia mwandishi wa habari hizi akae chini kwenye benchi la Yanga ili amueleze vizuri.
    Kondic aliyezungumza na DIMBA Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya mechi dhidi ya Polisi Morogoro ambayo timu yake ilishinda 1-0 alisema:
    “Sijawahi kusema Yanga hawaiwezi kuifunga Al Ahly, nilichosema, ile timu inabebwa sana na marefa, marefa waliwapendelea sana kule (Cairo). Goli la kwanza tulilofungwa lilikuwa la kuotea, refa yule yule alikataa penalti yetu halali kabisa.
    Ambani alipiga mpira, beki wao akauzuia kwa mkono, yeyote anayeweza kupata mkanda wa mechi ile, aangalie ataona. Bado marefa walikuwa wakiua mipango yetu uwanjani, walikuwa wakiisaidia sana Ahly.
    Haya ndio yaliyonikera, nikasema kuwafunga hawa ni vigumu, wanabebwa sana na marefa, kule kwao,”alisema Kondic ambaye wakati akizungumza na mwandishi wa DIMBA, Waandishi wengine walitokea kutaka kumsikiliza akawakaripia: “Ondokeni tafadhali, sitaki kuzungumza na nyinyi, mmekuwa mnaandika tu, wakati mimi siongei na nyinyi, nendeni mkaandike mlivyozoea, naomba mtuheshimu sisi ni mabingwa,”alisema.
    Kuhusu mchezo wa marudiano na Al Ahly, Kondic alisema kwamba kama waamuzi watakuwa wanatenda haki uwanjani, ana matumanini makubwa timu yake itaitoa Ahly.
    “Ninao wafungaji kwenye timu yangu, wanaweza kufunga hadi mabao nane kwenye mechi moja, kwa nini washindwe kufunga matatu, tutapigana nao hadi mwisho, tunataka tuwaonyeshe kama na sisi tunaweza kucheza na kushinda nyumbani kwa idadi sawa na ile au zaidi,”alisema Kondic.
    Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Angola na klabu ya Primiero de Agosto ya nchini humo, alisema kwamba anataka mchezo wa marudiano uchezwe kwenye Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam, kwa sababu ndio kama wa nyumbani kwao.
    “Unaposema Uwanja wa nyumbani, ni ule Uwanja ambao umezoea kucheza kila mara, umeuzoea kupita kiasi, na sisi huu ndio Uwanja wetu, nataka tucheze hapa,”alisema.
    Yanga baada ya kulala 3-0 kwenye mchezo wa awali wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Ahly, itakuwa na deni la kulipa kisasi hicho kwa ushindi wa 4-0, ili isonge mbele kwenye michuano hiyo au ilazimishe sare kwa kushinda 3-0, ili mshindi aamuliwe kwa mikwaju ya penalti.
    Mabao yaliyoizamisha Yanga kwenye Uwanja wa International mjini Cairo yalitiwa kimiani na Mohamed Barakat mawili na lingine lilifungwa na Muangola, Flavio Amado.
    Katika mechi tano ambazo Yanga imekutana na Al Ahly, imefungwa tatu ugenini na imetoka sare mara mbili nyumbani na ugenini. Mara ya kwanza Yanga ilikutana na Ahly mwaka 1982, katika michuano hii, enzi hizo ikijulikana bado kama Klabu Bingwa na mchezo wa kwanza mjini Cairo wavaa jezi za njano na kijani walitandikwa mabao 5-0 na mchezo wa pili, uliokuwa wa marudiano mjini Dar es Salaam, walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1.
    Mara ya tatu, Yanga ilikutana na Ahly mwaka 1988 na katika mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam, Aprili 9 mwaka huo, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana na kwenye mchezo wa mwisho kuzikutanisha timu hizo, uliokuwa wa marudiano, Aprili 22, watoto wa Jangwani walitandikwa 4-0.
    Si Yanga tu, hata timu nyingine zote zilizowahi kukutana na Ahly hazikuweza kuvuka, wakiwemo Simba, Pamba FC na Majimaji ya Songea. Mwaka 1985, Simba iliifunga Al Ahly mabao 2-1 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, katika michuano ya Kombe la Washindi, kabla ya kwenda kufungwa 2-0 mjini Cairo. Mwaka 1993, Al Ahly iliifunga 5-0 Pamba mjini Cairo katika Kombe la Washindi pia, kabla ya kuja kulazimisha sare ya bila kufungana mjini Mwanza, wakati mwaka 1999, Waarabu hao walianza kwa kuichapa 3-0 Majimaji ya Songea, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya kwenda kuwaongeza 2-0 mjini Cairo. Na hilo ndilo lilikuwa jicho la mwisho la Watanzania kwa Ahly, ambao wanatarajiwa kuonekana tena nchini wiki mbili zijazo kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
    Wakati huo huo: Katibu wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Emanuel Mpangala amesema kipa Obren Curkovic alitoka usiku wa Jumamosi, siku moja kabla ya timu hiyo kucheza na Al Ahly kwa ajili ya kutafuta kifaa cha kuchajia simu yake.
    “Kule chumbani kwake (Cairo) ile sehemu ya kuchomekea chaja, ilikuwa tofauti kidogo, ndio akatoka na kocha (Kondic) kwenda kutafuta itakayofaa,”alisema Mpangala.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KONDIC: KWA NJAA GANI NIIHUJUMU YANGA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top